Advertisements

Friday, August 31, 2012

IGP Mwema atangaza mwarobaini wa ajali za barabarani


Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ispekta Jenerali (IGP) Said Mwema
Jeshi la Polisi  kwa kushirikiana na Mamlaka ya kudhibiti Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) limewatangazia kihama madereva wa mabasi ya abiria wanaoenda mwendo kasi ambao ndio chanzo kikuu cha vifo vingi na majeruhi.

Limesema  kuanzia sasa litaanza kuwadhibiti kwa  kutumia mfumo wa kisasa wa njia ya Electronic (Vihicle Tracking System) na atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.



Kihama hicho kimetangazwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ispekta Jenerali (IGP)  Said Mwema, wakati akizungumza katika mkutano kati ya maafisa wandamizi wa Sumatra na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabara unaojadili namna ya kupunguza majanga ya ajali nchini.

Alisema kuwa katika kuhakikisha wanafanikisha mpango huo tayari Serikali imeshawatengea Sh. bilioni 2.5 baadhi yake zitatumika kwa ajili ya kuwapa mafunzo  ya teknolojia ya habari na  mawasiliano  (Tehama) maofisa wake na wale wa Sumatra.

IGP Mwema alisema kuwa mfumo huo Electronic utawezesha pia kubaini  mwendo kasi wa madereva kwa kutumia simu maalum za mikononi ambazo watapewa askari wa usalama barabarani.

Alisema mpango huo utakwenda sambamba na wakuu wa vikosi vya usalama barabarani kutengeneza mwiba utakaoweza kudhibiti askari wanaowakamata madereva hao wanaokwenda mwendo kasi wasitoe rushwa ili kukwepa mkondo wa sheria.

“Tunataka kudhibiti kabisa vitendo vya mwendo kasi, askari akibainika amechukua rushwa kwa dereva aliyekwenda mwendo kasi, basi mkuu wa kituo utakuwa mzembe na sehemu ya tatizo, hivyo utakuwa hautufai,” alisema.

Alisema sambamba na hilo jeshi hilo kwa kushirikiana na maafisa wa Sumatra watahakikisha wanayadhibiti mabasi yote mabovu ikiwemo ya kuondoa kabisa barabarani ambayo nayo yamekuwa yakichangia ajali.

Alisema kuwa Jeshi lake linakusudia kuweka askari wa doria katika maeneo hatarishi yanayosemwa maramara kwa mara kutokea ajali ili kuondoa dhana na hofu miungoni mwa abiria.

Aliwataka madereva kubadilika na pale wanapofanya makosa kuacha kutoa rushwa kwa askari wa usalama barabarani kwa kuwa ni kinyume na ni kosa la jinai kwa pande zote na kwamba wakibainika kwa pamoja watachukuliwa hatua za kisheria.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima, alisema Serikali inaunga mkono jitihada hizo za kupunguza vifo vinavyotokana na ajali zinazofanywa baina ya Jeshi la Polisi na Sumatra ambazo alisema  zikisimamiwa kwa pamoja zitasaidia kufikia malengo ya kuepusha vifo visivyo vya lazima.

Alisisitizia Jeshi la Polisi kufanya maandalizi haraka ya mpango huo ili kujiwekea lengo la kuanza kutekelezwa na kuichia Wizara kubaki na majukumu la kufanya maamuzi.

Alilitaka jeshi la Polisi kuhakikisha magari yote yanakaguliwa ipasavyo na kwa umakini kabla ya kwenda kuomba leseni, huku akisisitizia Sumatra kutokutoa leseni kwa gari ambalo halijakaguliwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahamad Kilima, alisema kuwa mkutano huo ni wa kikazi na ni muendelezo wa mikutano mitatu iliyofanyika kati ya maafisa wa Sumatra na Jeshi la polisi kwa lengo la kupunguza majanga ya ajali hapa nchini.



 
CHANZO: NIPASHE

No comments: