abiria wakijisaidia maarufu kama kuchimba dawa wakiwa kati ya moja ya safari za mikoani
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imesema kuanzia kesho abiria na wamiliki wa mabasi yanayosafiri umbali mrefu ambayo yatakutwa porini wakichimba dawa (kujisaidia), watakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Bw. Ahmed Kilima, imesema hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, alilolitoa hivi karibuni katika Mkutano wa Bunge la nane mjini Dodoma.
Alisema katika agizo lake. Dkt. Mwakyembe aliwataka wasafiri na wasafirishaji, kusitisha utaratibu huo ambao ulizoeleka kuanzia leo hivyo kuanzia kesho, wote ambao watakamatwa kwa kuendeleza utaratibu huo, watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema baada ya kutolewa agizo hilo, SUMATRA ilifanya mkutano na wasafirishaji ili kuweka mikakati pamoja ya utekelezaji wake ili kuwepo maeneo maalumu ambayo wasafiri na wasafirishaji watayatumia kwa ajili ya kuchimba dawa.
“Mamlaka inawaagiza wasafirishaji wote kutekeleza agizo hili kwa kuwatangazia abiria kabla ya kuanza safari na wakati wa safari, vituo ambavyo vimeainishwa kwa ajili ya huduma kwa wasafiri ni njia ya Dar es Salaam kwenda Mbeya.
“Kwa wasafiri wa mikoa hii, huduma ya kuchimba dawa itapatikana katika eneo la Ruvu, Chalinze, Kituo Kikuu cha Mabasi Msamvu, Ruaha Mbuyuni, Kitonga, Stendio ya Ipogoro, Mafinga na Makambako,” alisema.
Kwa njia ya Dar es Salaam kwenda Mwanza, huduma zinapatikana Kituo Kikuu cha Mabasi Msamvu, Gairo, eneo la Baduel na Kituo Kikuu cha Mabasi Singida Mjini.
Maenmeo mengine ni Kituo cha Mabasi Nzega Mjini, Kituo Kikuu cha Mabasi Tabora Mjini, Kituo Kikuu cha Mabasi Shinyanga Mjini, Kituo cha Mabasi Kahama na Kituo Kikuu cha Mabasi Mwanza.
Wasafiri wa wanaokwenda mkoani Kagera kutokea Kahama, vituo vitakuwa Ushirombo, Chato, Muleba, Bukoba ambapo wasafiri wanaokwenda Kigoma kabla ya kufika Kahama, vituo vitakuwa Kasulu, Kibondo, Runzewe.
Njia ya Dar es Salaam kwenda Tanga, vituo vitakuwa Mizani Msata na Segera ambapo njia ya Dar es Salaam, Moshi, Arusha na Manyara vitakuwa Korogwe, Mombo, Same, Mwanga, Himo, Moshi Mjini, Boma Ng'ombe, Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha pamoja na Kituo Kikuu cha Mabasi Manyara.
Alisema njia ya Dar e Salaam kwenda Lindi na Mtwara, vituo vitakuwa Nangurukuru, Lindi na Mtwara. Hata hivyo taarifa hiyo imesema katika baadhi ya vituo kutakuwa na huduma inayotolewa kati ya sh. 100 hadi 200 lakini maeneo mengine zitakuwa bure.
No comments:
Post a Comment