ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 27, 2012
MAPENZI NI MCHAKAMCHAKA, FEDHA NI DEREVA WA MOYO
NIKIANZA na mada yetu leo, napenda kubainisha hili: Dhana ya mapenzi duniani kote inaelekeza kwamba asili yake ni moyoni. Hii ina mantiki kuwa ndani ya kila mtu kuna vitu ambavyo anahisi kuhitaji mwenzi wake awe navyo. Sura, umbo na tabia.
Wakati ikitambulika hivyo, ni vema pia kufafanua kwamba kuna nakshi nyingi ambazo si za lazima lakini hutokea kuwavutia watu na kufunika hata yale ya msingi. USHAURI: Zingatia sifa muhimu na kuachana na vionjo vya ziada (accessories).
Wakati huohuo, nitoe msisitizo kwamba lazima furaha itimizwe na pande zote mbili (mwanamke na mwanaume). Kila mmoja ana wajibu wa kujituma kugharamia furaha ya mwenzake, vinginevyo itakuwa ni sawa na kucheza kombolela. Wewe unalinda kopo, mwenzako anakuja kulibutua.
Chunga sana, wabutuaji ni wengi. Kuna idadi kubwa ya ndugu zetu ambao wanateseka leo kwa sababu wao walijiamini wanalinda kopo lakini baadaye wanaojua kutumia vizuri nafasi za dhahabu, walifika na kubutua.
Maadili yakiwepo, fedha haitaendesha mapenzi. Simulizi za mateso kwa ndugu zetu hazitakuwepo. Angalau watu watawaheshimu wapenzi wao.
Stamina ameimba kwamba fedha imesomea udereva, inaendesha hadi mapenzi. Utaposoma makala haya, utaona ni kwa namna gani mapenzi yamekuwa dereva wa moyo na kusababisha yawakimbize watu mchakamchaka.
Sasa basi, nakuomba unaposoma makala haya, soma kwa mtindo wa katikati ya mstari (between the line). Kuna somo kubwa mno kwenye mada hii kwa sababu wengi wapo kwenye mateso makubwa ya kimapenzi kutokana na makosa yao wenyewe.
Ukisoma ujasiriamali, utaelekezwa kwamba mafanikio yako yatatokana pia na namna ulivyo na nidhamu katika fursa unazopata. Inawezekana ukawa na bahati kwenye maisha lakini utabaki kuwa si lolote endapo hutatumia nafasi zako vizuri.
Kama maisha, ndivyo yalivyo mapenzi. Hayatanyooka, wala hayatakaa vema upande wako ikiwa hutakuwa na heshima kwa fursa utakazopata. Si suala la ujana au kujipanga, muhimu kwako na kuheshimu kile kilichopo jirani yako. Zingatia: Mapenzi ni changamoto nzito.
Ukichezea penzi lako leo kwa sababu unazozijua wewe, tambua kwamba halitakaa kwako daima. Kama yalivyo maisha kwamba yapo mfano wa kioo, ukiyachekea yanacheka, ukiyanunia nayo yananuna. Ndivyo na mapenzi yalivyo. Ukiyachezea, nayo yatakuchezea kweli.
Unapaswa kuyaheshimu. Heshima ya mapenzi ni kumtunuku mapenzi ya kweli huyo ambaye amekujia na mapenzi yake. Umethibitisha anakupenda kweli, sasa kinachokuwasha nini mpaka uunyanyase moyo wake? Fumba macho, mara nyingi bahati huwa haiji mara mbili.
Inawezekana mwenzi wako wa leo ndiye mwenye mapenzi ya kweli. Ila wewe unausimanga moyo wake kwa sababu hana fedha. Unakwenda kuabudu wenye uwezo. Fimbo ya mbali haiui nyoka, kwa hiyo unaweza kufanya lolote, naye hatakuwa na cha kukufanya zaidi ya kumuachia machozi na sononeko.
Kuna watu hawajiulizi hili; Huyo anayekuja kwako akitumia fedha kukuteka kwenye himaya yake, ameshatumia jeuri hiyo kwa wangapi? Endapo utaujua ukweli, utakuja kufahamu kwamba ni wengi aliwanasa kwa sababu alitanguliza fedha.
Weka akilini kwamba haji kwako kwa sababu anakupenda ila anayo jeuri kuwa hutapindua kutokana na fedha alizonazo. Sasa basi, unapomkubalia unamfanya aongeze kiburi. Kesho atatupa ndoano kwa mwingine na huo ndiyo utakuwa mwendo.
Atakutamani kwa sababu ya muonekano wako, kwa hiyo kutokana na kiburi cha fedha alichonacho, kesho akimuona mwingine atakayemtamanisha, atatumia fedha zake kumnasa. Hii ina maana kuwa mkondo wako, watapita wengi. Mwisho kabisa, utabaini kwamba uliingia katika msafara wa kenge.
Atapita kwa wenye tamaa za fedha, nawe utakuja kuingia humohumo. Wewe utasema unajiheshimu lakini huyo uliyeangukia kwake, hachagui. Popote kambi, baadaye unapata jawabu kwamba umechangia mwanaume na machangudoa wengi wa mjini.
Wapo machangudoa wengi mjini na wanavutia kwelikweli. Kama kavutiwa na wewe na katumia ngawira kukunasa, inashindikana vipi kuvutiwa na machangudoa wengine, nao akatumia fedha kuwanasa?
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment