Thursday, August 30, 2012

Mauaji Moro yageuka kitendawili kigumu

  Chadema waelezea hofu yao
Utata umegubika kifo cha kijana mmoja anayedaiwa kupigwa risasi wakati wa maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jumatatu wiki hii mjini Morogoro kutokana na polisi na chama hicho kutoa taarifa zinazokinzana.

Wakati Polisi likitoa taarifa likidai kuwa kijana huyo, Ali  Nzona, aliuawa kwa kutupiwa kitu cha kurusha, Chadema kimeshikilia msimamo kwamba aliuawa kwa kupigwa risasi za moto na askari wa jeshi hilo.



Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa jeraha la marehemu lililokuwa kichwani lilitokana na kutupiwa kitu hicho na sio risasi kama ambavyo watu wanadhani.

 Shilogile alisema hali hiyo imebainika kufuatia matokeo ya uchunguzi uliofanywa na madaktari wawili wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na Dk. Ahmed Makata kutoka jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mwanasheria wa Chadema, Aman Mwaipaja na baadhi ya askari wa jeshi hilo.

 Aliongeza kuwa  baada ya uchunguzi huo, jeshi hilo kwa kushirikiana na timu iliyoundwa, wataendelea kuchunguza kitu hicho kilikuwa ni nini na nani alihusika kukirusha hadi kusababisha kifo hicho.

CHADEMA YATAKA SHERIA YA UCHUNGUZI WA VIFO

Wakati polisi wakitoa taarifa hiyo, Chadema kimesema kimeshtukia mfululizo wa mauaji ya wananchi yanayofanywa na jeshi hilo katika mikutano na maandamano ya chama hicho na kuitaka  serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).

Aidha, kimesema hakina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa  Polisi (IGP), Said Mwema, kuchunguza tukio hilo la mauaji kwa kuwa tayari serikali na jeshi hilo wametoa maelezo yenye kutofautiana na  mashuhuda waliokuwepo  eneo la tukio.

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema, John Mnyika, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mnyika alisema kutokana na kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola, Chadema kinatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati kuwezesha uchunguzi wa kina kwa mujibu wa sheria hiyo.

Alisema wakati wa vikao vya Bunge mwaka jana kufuatia mfululizo wa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola kwa nyakati tofauti, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi kwamba  Sheria ya Uchunguzi wa Vifo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye utata.

“Katika muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Nzona haupaswi kufanywa na timu ya polisi, bali sheria hiyo sasa ianze kutumika ili uchunguzi uwe huru na kufanya wananchi kuwa na imani na serikali na Jeshi la Polisi,” alisema Mnyika.

Alisema kauli zilizotolewa na serikali, Jeshi la Polisi, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi,  zina mwelekeo wa kulilinda jeshi hilo  ambalo askari na maafisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji hayo.

Aliongeza kuwa Chadema haikubaliani na hatua zilizochukuliwa na serikali mpaka sasa kuhusu tukio hilo na maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani Agosti 28, mwaka huu ambayo kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa maafisa wa Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji husika.

Alisema wakati Serikali na Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza kuwa askari walifika jirani na eneo la tukio na ndipo afisa mmoja wa polisi alionyesha ishara na risasi za moto na mabomu ya machozi zilianza kupigwa na kumpata marehemu na kudondoka.

Mnyika alisema baada ya marehemu kupigwa risasi, gari la polisi lililohusika katika mauji hayo liliondoka na gari lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa Morogoro (FFU) ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba mwili wa Ali Zona na kuondoka naye.

Alisema taarifa za kwamba tukio la kupigwa risasi marehemu lilitokea mbali na eneo la tukio zi za kweli,  bali lilitokea pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi walikuwa wakifanya mashambulizi.

Alisema jeshi hilo mkoani humo ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka makao makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni, Simon Siro.

Mnyika alifafanua kuwa Chadema ilipanga kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini Agosti 4 mwaka huu na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.

Alisema hata hivyo, Polisi walikataa kufanyika kwa maandamano na mikutano ya Chadema kwa kisingizio cha sikukuu ya nane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya mikutano ya CCM sababu ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.

Alisema baada ya mvutano na mazungumzo baina ya chama hicho na polisi, Chadema ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya jeshi hilo na kwamba maandamano na mikutano vifanyike baada ya siku ya kuanza kwa sensa Agosti 26 mwaka huu na Chadema ilipendekeza Agosti 27 ambapo Jeshi la Polisi liliikubali.

Alisema Agosti 23, mwaka huu Jeshi la Polisi liliandika barua ya kueleza kwamba imetoa kibali cha mkutano suala ambalo si mamlaka yake kisheria na pia ikakataza maandamano. 

“Chadema iliamua kwa mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Agosti 24 na ndipo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala za kupita  na barabara zikakaguliwa,” alisema Mnyika.

Alisema hata hivyo, katika hali ya kushangaza kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi ya watembea kwa miguu bila sababu zenye misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza kwamba yafanyike maandamano kwa kutumia magari.

DK. SLAA: TUTAWASILIANA NA MABALOZI

Wakati huo huo; Chadema kimesema kitasambaza orodha ya matukio ya unyanyasaji na hujuma zinazofanywa na vyombo vya dola nchini kwa mabalozi wan chi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini.

Uamuzi huo umefikiwa kufuatia polisi kutangaza kufuta vibali vya maandamano na mikutano ya Chadema wakati kikiendelea na ziara mikoa ya Nyanda za Juu kusini kuelezea kampeni yake ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoratibiwa na chama hicho. 

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Willibroad Slaa, alisema hayo wakati akizungumza juzi na viongozi na wanachama wa chama hicho baada ya kuwasili mkoani Iringa.

Alisema Chadema kitaitangazia dunia na Watanzania kwa ujumla kwamba yanayofanywa na vyombo vya dola ni njama za kukidhoofisha ili kionekane ni chama cha vurugu.

Alisema chama hicho kitatumia fursa katika kikao cha pili kitakachoitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, kutoa malalamiko jinsi kinavyofanyiwa hujuma.

Dk. Slaa alisema licha ya jeshi hilo kufuta maandamano na mikutano yao chama hicho kitaendelea na hamasa kwa kufanya shughuli zake za kichama kwa siku nne mkoani Iringa.

Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe, Dar; Idda Mushi Morogoro na  Godfrey Mushi, Iringa.


 
CHANZO: NIPASHE

No comments: