Advertisements

Wednesday, August 29, 2012

Ochieng anunua mkataba AFC ajiunge Simba




Beki Pascal Ochieng amelazimika kuununua mkataba wake na AFC Leopards ili kupata kibali cha uhamisho wake wa kujiunga na Simba, taarifa iliyotumwa jana katika tovuti ya klabu hiyo ya Kenya ilisema.

Ochieng, beki wa kati ambaye hakuwa na furaha Leopards alijiunga na timu hiyo kwa mkataba wa miezi sita katikati ya msimu akitokea katika klabu yenye matatizo ya kifedha ya Rangers FC.

Taarifa ya tovuti ya AFC ilisema jana kuwa Ochieng anaondoka katika klabu hiyo akiwa hajacheza mechi hata moja ya kimashindano na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyekaa klabuni hapo kwa muda mfupi usiozidi wiki tano. 



Katibu Mkuu wa Leopards, Winston Kitui alithibitisha kwenye tovuti hiyo kuwa Ochieng ameununua mkataba wake, na kuifungulia njia klabu hiyo kuruhusu kutolewa kwa kibali chake cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kutua Simba.

“Tumemuagizameneja wetu wa ITC kukamilisha jambo hilo,” alisema.

Ufafanuzi huo unahitimisha utata uliozunguka hatima ya beki huyo uliokuwapo kwa klabu zote mbili.

Wakati Leopards ilikanusha kufahamu chochote kuhusu mazungumzo ya uhamisho wa mchezaji huyo, Simba ilikuwa ikikaririwa na vyombo vya habari za Tanzania na mitandao ya kijamii kwamba imemsajili Ochieng.

Kitui alisema Leopards imeafikia mchezaji huyo kuununua mkataba wake baada ya kuruhusiwa na kocha Jan Koops ambaye alisema kwamba hayuko tayari kumchezesha mchezaji ambaye mawazo yake yake.

Vyanzo pia vilisema kwamba Ochieng hakuwa na raha baada ya kubaini kwamba kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Leopards ilikuwa ni jambo gumu kwa kuzingatia kwamba wapinzani wake katika nafasi ya ulinzi wa kati Eric Masika na Nahimana Jonas wako katika kiwango cha juu kisichohitaji maswali.

Katika kipindi chake kifupi klabu hapo, alicheza mechi moja tu ya kirafiki ambayo alishindwa kuonyesha kiwango.

“Bado tunamtakia mafanikio mema aendako,” alisema Kitui.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutokea Kenya jana, mjumbe wa kamati ya utendaji ya AFC Leopards, Richard Ekelye, alisema pamoja na Ochieng, walimalizana pia na Salim Kinje baada ya Simba kutoa pesa walizohitaji.

Hata hivyo hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha kilicholipwa na Simba kwa ajili ya nyota hao wawili. 

Ochieng na Kinje wako kambini na klabu yao mpya ya Simba mjini Arusha wakati wakisubiri kuwasili kwa ITC zao.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: