ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 8, 2012

Okwi atua Dar, aikana Yanga

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, aliwasili jijini Dar es Salaam jana na kuzima uvumi uliozagaa kwamba yuko mbioni kujiunga na Yanga au Azam huku akifafanua kwamba hakufanya majaribio kwenye klabu ya Redbull Salzburg inayoshiriki Ligi Kuu ya Austria kwa sababu tangu alipotua huko alikuwa mgonjwa.

Akizungumza na NIPASHE mara baada ya kuwasili nchini jana mchana, Okwi alisema hakufanya majaribio hata siku moja na klabu hiyo iliyotolewa katika hatua za awali za Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, jambo linalomaanisha kwamba taarifa zilizokuwa zikitolewa na uongozi wa Simba kwamba amefanya majaribio na kufuzu hazikuwa za kweli.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, aliuambia mkutano mkuu wa wanachama Jumapili kuwa Okwi amefuzu majaribio hayo.



Okwi alisema kwamba baada ya kufika katika jiji la Salzburg alianza kusumbuliwa na malaria hivyo akashindwa kufanya mazoezi aliyopangiwa na benchi la ufundi la timu hiyo.

Aliongeza kuwa baada ya kushindwa kujifua huko, uongozi ulimueleza arejee nyumbani na ataitwa tena hapo baadaye mwaka huu kwa ajili ya kufanyiwa upya majaribio. Hata hivyo, alikiri kuwa hajui ataitwa lini.

Alisema kwa sasa anaweka nguvu zake Simba katika maandalizi ya msimu mpya na kutetea ubingwa wao wa Tanzania Bara katika Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza Septemba na pia michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.

"Nimerejea nchini na sasa kikubwa ni kujipanga upya katika kutetea ubingwa wetu wa Tanzania na kujiandaa na mashindano ya Afrika, kutolewa mapema katika mashindano ya Kombe la Kagame si mwisho wa Simba, tunaelekeza nguvu zetu ili kurejesha heshima ya timu," alisema Okwi.

Mshambuliaji huyo alisema kwamba hana mipango yoyote ya kuihama Simba na kamwe hajafanya mazungumzo na klabu nyingine kwa sababu anaheshimu mkataba wake ambao unatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwakani.

"Siwezi kuzungumza na timu yoyote, mkataba wangu hauniruhusu kuzungumza na klabu nyingine, mimi bado ni mchezaji wa Simba na nawaomba wote tujipange ili kuipa Simba mafanikio zaidi ya msimu uliopita. Waambie Simba watulie, kesho (leo) wataniona katika tamasha la Simba Day,"  aliongeza mshambuliaji pia wa timu ya taifa ya Uganda (Cranes).

No comments: