ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 30, 2012

Operesheni ya wavamizi ardhi Dar yabaini raia 10 wa kigeni


Watu 10 kati ya 126 waliokamatwa kwenye operesheni iliyofanywa na Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi toka katika mkoa wa kipolisi wa Kinondoni kwa ajili ya kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo ya wengine katika kata za Wazo na Mabwepande, wamegundulika kutokuwa raia wa Tanzania.

Hali hiyo ilibainishwa jana jijini Dar es salaam na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kuwajulisha hatma ya operesheni hiyo ilipofikia hadi sasa.

Aidha, Kamanda Kenyela alisema kwamba watu wengine 116 waliobakia tayari wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwashambulia polisi kwa silaha za jadi kama pinde, mishale, mapanga, shoka,vipande vya nondo, bisibisi na visu kwa lengo la kuwazuia wasitekeleze kazi yao.

“Kulikuwepo na taarifa kwamba baadhi ya watuhumiwa tuliowakamata toka katika maeneo hayo si raia na kwa hivyo tukashirikiana na Idara ya Uhamiaji, ndipo ilipothihirika kwamba kuna utata wa uraia kwa hawa watu 10,” alisema.

Kamanda Kenyela alisema kuwa operesheni hiyo ilifanyika ili kutekeleza agizo la Mahakama na vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa, lakini pia kutokana na kitendo cha wavamizi kuwapiga, kuwafukuza, kuharibu mali, kufanya vitendo vya udhalilishaji vya ubakaji na ulawiti kwa wamiliki halali pale walipoenda kwenye maeneo yao,” alisema Kamanda Kenyela.



Alisema kwamba katika operesheni hiyo, jeshi lake mbali na kukamata kiasi kikubwa cha silaha za jadi,  lilikamata vile vile lita 315 za pombe haramu ya gongo, mitambo sita ya kutengenezea pombe hiyo na kilo 105 za bangi.

Aidha alisema vitu vingine walivyokamata ni pamoja na mihuri bandia ya kuuziana viwanja na kutambulishana kuhusu maombi ya uraia kupitia viongozi batili wa wavamizi waliokuwa wakijifanya ni viongozi wa serikali ya mtaa na karatasi zenye ajenda za vikao vyao vya kupinga operesheni na katiba yao.

Kamanda Kenyela alisema kwamba operesheni hii ya awali ilifanyika kuanzia Agosti 22 hadi 25, mwaka huu, katika  maeneo ya Kinondo, Kazaroho, Mbopo, Boko Magereza na Benaco Salasala yaliyoko katika kata hizo za Wazo na Mabwepande.

“Ninawaasa wananchi wote waliovamia maeneo ya watu katika Manispaa ya Kinondoni, ikiwa ni pamoja wa wale wa Chasimba na Kunduchi kwenye machimbo ya kokoto, kuondoka mapema kabla hawajafikiwa na operesheni hii, kwa kuwa ni endelevu na haitasimama mpaka wavamizi wote watakapoondolewa,” alisema Kamanda Kenyela, ambaye aliongoza opereseheni hiyo mwenyewe.

Kamanda huyo pia alithibitisha kukamatwa kwa askari mmoja wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika operesheni hiyo na kufafanua kuwa baada ya hapo walimkabidhi jeshini.
CHANZO: NIPASHE

No comments: