ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 27, 2012

Simba, Yanga zaua



Mshambuliaji  mpya Daniel Akuffor aliyesajiliwa kutoka Stella Abidjan ya Ivory Coast ameanza kuitumikia klabu yake mpya ya Simba kwa kishindo baada ya kuiongoza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Mathare United ya Kenya katika mechi yao ya kirafiki kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Mjini Kigali, Yanga ilipata ushindi wa pili mfululizo katika ziara yake ya nchini Rwanda wakati ilipoibwaga timu ya Polisi ya huko kwa magoli 2-1 katika mechi ya kirafiki pia.

Polisi walitangulia kupata bao kupitia kwa Fabrice Twagizimana, kabla ya Yanga kucharuka na kupata magoli mawili ndani ya dakika tatu kupitia kwa mabeki watupu, Stephano Mwasika (dk.58 na Nadir Haroub 'Cannavaro' aliyefunga la ushindi katika dakika ya 60.



Ushindi huo ulikuwa ni wa pili kwa Yanga ambayo imealikwa nchini Rwanda na Rais wa nchi hiyo Paul Kagame kwa ajili ya kwenda kumtembelea Ikulu kama mabingwa wa Klabu wa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwa mara ya pili mfululizo. Katika mechi yao ya kwanza waliyoicheza Ijumaa, Yanga walishinda 2-0 dhidi ya Rayon Sport ya Rwanda pia.

Akuffor aliyejiungana Simba katika kipindi hiki cha usajili, aliifungia timu yake goli la kuongoza katika dakika ya 58 kufuatia krosi ya beki wa kushoto anayepanda kushambulia Amir Maftah.

Goli hilo lilidumu kwa dakika tatu tu kwani beki wa Simba, Juma Nyosso alijifunga wakati akijaribu kuokoa shuti la Daniel Mwaura katika dakika ya 61.

Huku mechi ikionekana kama ingemalizika kwa sare, Kigi Makasi aliyetua Simba akitokea kwa mahasimu wao Yanga, aliipatia goli la pili timu hiyo inayofundishwa na Mserbia Milovan Cirkovic kwa njia ya penalti baada ya kiungo Uhuru Selemani kuchezewa madhambi ndani ya 18 katika dakika ya 81.

Simba ilipata pigo la mapema baada ya mchezaji wake mpya raia wa Mali, Komabil Keita, kutoka kutokana na kuumia 'enka' katika mechi hiyo ambayo wenyeji walipoteza nafasi nyingi za kufunga huku mshambuliaji Mzambia Felix Sunzu na Abdala Juma wakiwa miongoni walioinyima timu yao ushindi mnono zaidi.

Kikosi cha Simba kilichoanza jana kilikuwa: Wilbert Mweta, Nassoro Said 'Chollo', Amir Maftah, Pascal Ochieng, Komabil Keita, Salum Kinje, Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi 'Boban', Felix Sunzu, Abdala Juma na Daniel Akuffor. 

Wakati huo huo, Somoe Ng'itu, anaripoti kuwa beki tegemeo wa Simba, Shomary Kapombe, bado anasumbuliwa na maumivu ya goti yanayomfanya ashindwe kuanza mazoezi ya pamoja na nyota wengine wa timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijini Arusha, daktari wa Simba, Cosmas Kapinga alisema kuwa Kapombe bado anauguza maumivu ya goti na mazoezi anayofanya ni mepesi chini ya uangalizi wake.

Kapinga alisema kuwa endapo hatajitonesha sehemu hiyo ya goti, kuanzia keshokutwa Jumatano anaweza kuungana na wenzako na jana hatapangwa kwenye mechi ya kirafiki wa kimataifa dhidi ya Mathare United kutoka Kenya.

"Kapombe ndio majeruhi, anasumbulia na goti, aliumia baada ya kurejea kwenye klabu, yale maumivu ya nyama za paja ambayo yalimfanya ashindwe kuongozana na Taifa Stars kwenda Botswana alishapona," alieleza daktari huyo.

Alimtaja mshambuliaji, Felix Sunzu, kwamba yuko 'fiti' na anaendelea kujinoa kwa ajili ya msimu ujao.

Alisema kwamba wachezaji wengine waliosalia wanaendelea vyema na mazoezi na kila mara wamekuwa wakifanyiwa uchunguzi ili kuhakiki afya zao.

"Tunataka kuingia kwenye msimu mpya wa ligi tukiwa kamili kila idara," aliongeza Kapinga.

Simba iko Arusha kwa ajili ya kambi maalumu na imepanga kurejea jijini Dar es Salaam siku chache kabla ya kuanza kwa ligi ambayo hadi sasa haijajulikana itaanza ligi.

Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia, Milovan Cirkovic, ameridhishwa na kambi yake na hali ya hewa ya Arusha ambapo hata mechi za kirafiki anapendekeza zichezwe jijini humo.

Mabingwa hao wa ligi watafungua msimu mpya kwa kuvaana na Azam katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayochezwa wiki moja kabla ya ligi kuanza.

Aidha, kikosi cha wachezaji wa Yanga kinatarajia kurejea nchini leo saa 9:00 mchana kikitokea Kigali ambako walikwenda kwa ajili ya mwaliko wa Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Wakiwa Kigali Yanga walionana na Rais Kagame, kutembelea Makumbusho ya Taifa ya nchi hiyo na kucheza mechi mbili za kirafiki.

Magoli ya Yanga dhidi ya Rayon yalifungwa na washambuliaji wake, Mganda, Hamis Kiiza na Simon Msuva ambaye alianza kuifungia timu yake hiyo mpya wakati ilipocheza mchezo mwingine wa kirafiki na African Lyon siku chache kabla ya kwenda Kigali ambauo Yanga walishinda 4-0.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Binkleb, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kwamba kambi yao ilikwenda vizuri na wanaamini imesaidia kuimarisha timu.

Binkleb aliwataja wachezaji ambao ni wagonjwa na hiyo imetokana na mabadiliko ya hali ya hewa kuwa ni Rashid Gumbo na Idrissa Rajab ambao jana hawakupangwa kwenye mechi dhidi ya Polisi.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: