Friday, August 31, 2012

WALIOANDAMANA KINYUME CHA SHERIA UDSM WAACHIWA HURU

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imewaachia huru wanafunzi 51 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliokuwa wakikabiliwa na  mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali na kukaidi amri halali ya askari wa Jeshi la Polisi iliyowataka watawanyike.

Akiwaachia huru wanafunzi hao jana, Hakimu Mkazi  Waliarwande Lema alisema anawaachia huru washtakiwa hao, kwa mujibu wa kifungu cha 225 (5) cha Sheria ya  Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), sura ya 20 kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.


Wanafunzi hao  waliachiwa huru baada ya Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila kudai kuwa kesi ilikuja kwa ajili ya  kusikilizwa na kubainisha kuwa mahakama ilikwisha toa ahirisho la mwisho Agosti 13, mwaka huu.

Mwangamila alidai kuwa waliwasiliana na mashahidi wao ambao ni askari kupitia kwa RCO wa Wilaya ya Kinondoni, lakini aliwaambiwa  kuwa askari hao ni moja kati ya askari waliopo kwenye Sensa ambayo ni muhimu kama kesi hiyo.
Hivyo  Wakili huyo wa Serikali aliiomba mahakama itoe ahirisho lingine la mwisho  hadi Jumatatu  kwa sababu  askari hao bado  wapo kwenye Sensa ambayo inaisha Jumapili.

Baada ya kutolewa kwa hoja hizo, Wakili wa Utetezi, Regnal Martin alipinga ombi la kuahirishwa kwa kesi hiyo na kuutaka upande wa mashtaka  kuheshimu  amri ya mahakama.

Wakili Martin alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa  kwa sababu tofauti  ikiwemo ya askari hao kuwepo kwenye mgomo wa madaktari wa Julai 12, mwaka huu.

Akitoa uamuzi juu ya hoja hizo, Hakimu Lema alisema baada ya kupitia mwenendo mzima wa kesi , mahakama inajiuliza  swali  kuwa mashahidi pekee ni hao hao maaskari na kama ni hao  upande wa mashtaka ulipaswa kuwasilisha hati chini ya kifungu cha sheria cha 225 (4) cha CPA ambacho kinaeleza tarabu kama shahidi hayupo nini kifuatwe.

Hakimu Lema alisema sababu zilizotolewa na upande wa mashtaka ni  za msingi lakini hazikubaliki  na kwamba walichokifanya wameidharau mahakama kwa kutofuata taratibu zilizopo.

Aliongeza kuwa ana wasiwasi  hata kutoa ahirisho lingine la mwisho kwa upande wa mashtaka  kwa sababu akitoa ahirisho hadi Jumatatu wanaweza kwenda na sababu nyingine kuwa askari hao wapo kwenye matukio yaliyotokea baada ya Sensa.

Baada ya kuangalia  mwenendo mzima wa kesi hiyo, Hakimu aliliondoa shauri hilo kwa mujibu wa kifungu cha 225 (5) sura ya 20  kwa sababu upande wa mashtaka ulishindwa kuliendesha shtaka hilo.

Wanafunzi  walioachiwa huru ni Mwambapa Elias,Evalist Elias, Baraka Monesi, Hellen Mushi, Alphonce Lusako, Matrona Babu, Rolana Wilfred, Godfrey Deogratius , Munisi Denis,Evanos Gumbi pamoja na wenzao 40.

Awali Wakili wa Serikali, Ladslaus  Komanya alidai kuwa mnamo Novemba 11 mwaka huu,  eneo la Mlimani la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio halali na kusababisha uvunjifu wa amani  eneo hilo.

Komanya alidai kuwa  washtakiwa hao wakiwa kwenye mkusanyiko huo haramu kwa lengo la kufanya mgomo, askari wa Jeshi la Polisi waliwataka watawanyike, lakini hata hivyo wanafunzi hao walikaidi amri hiyo na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Hata hivyo washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa jeshi la polisi, walikana mashtaka hayo na waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika ambaye alisaini bondi ya Sh1milioni.

No comments: