ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 2, 2012

Washtakiwa, polisi wapambana nje ya korti


ames Magai
WATU watano waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya, juzi walizua tafrani mahakamani, kufuatia hatua yao ya  kupambana na askari polisi na kufanikiwa kutimua mbio, ili kuepuka kukamatwa tena baada ya kuachiwa huru.

Hata hivyo, washtakiwa wawili miongoni mwa hao,  walifanikiwa kuponyoka baada kuwazidi mbio askari polisi na kutokomea mahali kusikojulikana. Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika Mahakama Kuu ya Tanzania,  Kanda ya Dar es Salaam, baada ya  Jaji Lawrence Kaduri, kuwafutia kesi na kuwaachia huru washtakiwa hao kufuatia maombi yaliyowasilishwa na upande wa mashtaka.  Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa juzi lakini Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila aliiarifu mahakama kuwa, Jamhuri haioni haja ya kuendelea kuwashtakiwa watu hao.

Wakili Mwangamila alidai kuwa  Mkurugenzi wa Mashtaka chini ya kifungu cha 91[1] cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, ameomba kuwafutia mashtaka watu hao.
Kufuatia ombi hilo, Jaji Kaduri aliamua kuwaachia huru washtakiwa hao, lakini mara baada ya Jaji kutoka mahakamani, askari polisi ambao haikujulikana kuwa walitoka wapi, waliwafuata ili kuwakamata tena. Hali hiyo ilizua mapambano makali baina ya washtakiwa hao na ndugu zao dhidi ya askari hao.


Katika tukio hilo washtakiwa watatu waliwazidi nguvu na ujanja askari polisi na kufanikiwa kutimua mbio kutoka katika chumba cha mahakama.  Kitendo hicho kilizua taharuki na hofu miongoni mwa watumishi na wananchi waliokuwa wamekwenda mahakamani kupata huduma.   Wananchi hao  walianza kukimbia huku na kule wakidhani kuwa kulikuwa na tukio la hatari. 

Hata hivyo baadaye, ilibainika kuwa walikuwa washtakiwa waliokuwa wameachiwa, walikuwa wakiwakimbia askari ili wasiwakamate tena. Watu wawili kati ya waliotimua mbio, walifanikiwa kujinusuru baada ya kuwazidi mbio askari  polisi na badala yake, askari waliweza kumkamata mmoja na kumrudisha katika mahabusu ya mahakamani kuungana na wenzake. Waliofanikiwa kuponyoka ni pamoja na aliyekuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, Rajabu Hamisi Ally na John Robert Nswima.

 Walioachiwa lakini wakakamatwa tena ni Mohamed Shaban, Hakimu Omary na Kiemba Mtamamchungu. Wakati hao yakiendelea, ndugu wa washtakiwa walikuwa wakipiga kelele kupinga hatua ya askari hao kuwakamata tena ndugu zao.  “Hatukubali, hatukubali kabisa, watu mliwakamata wenyewe kisha mkawaachia wenyewe, sasa iweje muwakamate tena? Kama ni hivyo tutafia hapa wote,” alisikika mmoja wa ndugu hao. .

Baadaye askari hao waliondoka na watuhumiwa huku baadhi ya ndugu wakihangaika wasijue la kufanya wala pa kuanzia, kuwatafuta ndugu zao hao. Hata hivyo, askari mmoja wa mahakama, aliwashauri waanzie katika Kituo Kikuu cha Polisi.

Habari zilizolifikia Mwananchi baadaye zilieleza kuwa kufuatia tukio hilo, maofisa wa usalama kutoka Ikulu walifika mahakamani na kufanya uchunguzi wa kisiri kujua kilichokuwa kikiendelea.

Katika kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2011 washtakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sita ya dawa za kulevya. Mashtaka mengine yalikuwa ni  kufadhili shughuli za usafirishaji wa dawa za kulevya, kusaidia kutenda kosa, kutenda kosa na kushawishi kutenda kosa.

2 comments:

Anonymous said...

Tanzania yetu hiyo, hakuna haki

Anonymous said...

Huo ni uonevu tu,askari wamezowea kupewa rushwa na ndiyo maana walifanya hivyo,Tanzania hakuna haki.