ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 30, 2012

WATU 50 WAKAMATWA WAKIPANGA KUWADHURU POLISI


Na Benjamin Masese, Dar es Salaam
WATU 50, wakiwamo Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kukutwa wakipanga njama za kuwadhuru polisi.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alisema watu hao walikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika eneo la Mabwepande, Kata ya Bunju kunakofanyika operesheni ya ubomoaji wa nyumba zilizojengwa kinyemela.

Alisema baada ya shughuli hiyo kuanza wiki moja iliyopita, baadhi ya wananchi wa eneo hilo, hususani wale waliovamia viwanja vya watu wengine walianza kupambana na polisi kwa kutumia silaha za jadi, zikiwamo upinde na mishale, panga na mawe.

Alisema katika mapambano hayo, polisi walifanikiwa kuwakamata watu 73 na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Wakati tukiendelea kusimamia usalama katika shughuli ya ubomoaji, tulipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kwamba kuna kikundi cha watu kinajiita Mungiki kinafanya kikao cha siri eneo la Mabwepande.

“Polisi walifanya mbinu zao na kufanikiwa kuwakamata wote 50, tulipoanza kuwahoji tumebaini kati yao kuna wanajeshi wa JWTZ, pia wengine wanadai ni kabila la Wamanyema, Wahaya kutoka Mkoa wa Kigoma, Kagera na mingine ya pembezoni mwa nchi.

“Lakini kutokana na kikundi hicho kuwa na makabila mengi pia tumebaini wengine si raia wa Tanzania, hivyo tumeunda jopo la wataalamu kutoka Uhamiaji na polisi kuwachunguza uraia wao, kwa wale wanajeshi tunafuata taratibu za kuwakabidhi kunakostahili ili wawashughulike wenyewe,” alisema Kenyela.

Alisema amechukizwa na kitendo cha polisi kusimamia usalama wa raia huku upande mwingine ukiandaa mipango ya kuwapinga na aliwataka wananchi wote kuhama wenyewe kabla ya kufikiwa.

Alisema viwanja vilivyovamiwa vilikuwa vinamilikiwa na watu kihalali, lakini katika hali isiyo ya kawaida kuna watu walianza kuvamia na kujenga nyumba zao.

Alisema kutokana na uvamizi huo, wenye viwanja waliamua kwenda mahakamani na kudai haki yao na kuamriwa zibomolewe.

Wakati huohuo, JWTZ imetoa kauli kuhusu askari wake kuungana na wananchi na kuwapinga polisi ikiwa ni pamoja na kufanya kikao cha siri.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe, alisema askari hao watafikishwa katika mahakama ya jeshi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Taarifa rasmi ya wanajeshi hao haijafika kwangu rasmi ila nimesikia hivyo, unajua askari wetu wakifanya kosa taarifa hupelekwa katika kikosi chao na kufanyiwa kazi na wakubwa wake.

“Baada ya hapo ndipo ninapoletewa taarifa rasmi kwa ajili ya kuisemea katika vyombo vya habari kama inahitajika kufanya hivyo na kama haihitajiki inatunzwa kama kumbukumbu, sasa kwa hili ikibainika kweli wamehusika lazima wachukuliwe hatua kali.

“Hatutakuwa na huruma kwa askari wetu anayekwenda kinyume na taratibu za kijeshi kwa sababu hatukuwalea kufanya vitendo vya namna hiyo,” alisema Kanali Mgawe.
Chanzo: Mtanzania

No comments: