Tukio hilo lilitokea juzi kati ya vituo vya treni vya Saranda na Manyoni mkoani Singida.
Akizungumzia tukio hilo, Meneja Mawasiliano wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Midladjy Maez, alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 1:00 usiku baada ya injini mojawapo za treni hiyo kuwaka moto wakati dereva akijaribu kuipandisha kwenye mwinuko wa reli.
Maez alisema kuwaka kwa injini kulisababisha mtafaruku kwa abiria na baadhi yao walianza kutokea madirishani na wengine kupoteza mali zao.
Kufuatia tukio hilo, watu 15 ambao wawili kati yao walijeruhiwa vibaya walikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, ambapo juhudi za kuwahamishia katika Hospitali ya Mkoa ya Dodoma zilikuwa zinaendelea kufanyika.
Aliwataja waliojeruhiwa na kuwa katika hali mbaya kuwa ni Sikujua Mtonzi ambaye alivunjika mguu wa kushoto na Bathromeo Raphael ambaye alivunjika mkono wa kushoto.
"Baada ya tukio hilo, mafundi wetu waliizima injini hiyo na kuipeleka Manyoni Mjini ambapo majira ya saa mchana, treni likaendelea na safari kwa kutumia injini iliyobaki. Injini iliyoshika moto ilipelekwa kwenye karakana yetu iliyopo Morogoro kwa ajili ya uchunguzi na matengenezo zaidi,'' alisema.
Baadhi ya abiria walisema kitendo cha abiria hao kutoka kwenye madirisha na kuanguka huku wengine wakikimbia na kukanyagana kiliwasababisha abiria hao kujeruhiwa vibaya.
“Pia tumepoteza mali zetu kwani baadhi ya wenzetu walitumia fursa hiyo kuwaibia wenzao,’’ alisema Mwalimu Nelea Salvatory aliyekuwa akisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Urambo, Tabora.
Aidha abiria walionusurika na ajali hiyo, waliiomba serikali kufanya ukarabati wa injini na mabehewa ikizingatiwa kwamba tukio kama hilo lilitokea hivi karibuni baada ya moja ya mabehewa ya terni abiria lililokuwa likisafiri kutoka Kigoma kwenda Dar es Salaam, kuwaka moto kabla ya kuzimwa kwa mchanga kutokana na matatizo yaliyokuwa kwenye mfumo wa breki.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment