ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 10, 2012

Video mauaji ya Mwangosi yaliza Kamati Kuu Chadema

Picha za video ya tukio la kuuawa kwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliyeuawa kinyama na polisi Jumapili iliyopita, jana ziliwaliza wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliokutana jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine kujadili tukio la kadhia iliyotokea Iringa katika operesheni yao ya Vuguvugu la Mabadiliko nchini (M4C).

Picha hizo zilionyeshwa katika ufunguzi wa kikao hicho zikiwamo za mnato ambazo zilizorekodi matukio ya vurugu zilizosababisha mauaji ya Mwangosi, zilisababisha wajumbe wengi wa CC kuangua kilio na wengine kububujikwa na machozi.

Mwangosi aliuawa kwa kupigwa na bomu na polisi, wakati wakizuia viongozi na wafuasi wa Chadema kufungua tawi la chama hicho, katika Kijiji cha Nyololo, Wilaya ya Mufindi, mkoani humo, Jumapili wiki iliyopita.



“Tumeingia katika mgogoro mpya kama taifa, mgogoro, ambao raia hatuliamini Jeshi la Polisi, jeshi lenye dhamana kubwa ya kulinda raia na mali zao. Jeshi, ambalo ndiyo kimbilio kubwa la kila mmoja anayedai haki linakuwa sasa ni jeshi la kuogopwa na kila mtu,” alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo na kuongeza:

“Na tunaona kwa makusudi kabisa jeshi lenyewe, taasisi nyingine za kiserikali kama Msajili wa Vyama vya Siasa, wanakazana kila njia itumike kufunika ukweli, ambao umefanywa kwa misingi ya kiovu sana na jeshi letu la polisi.”

Alisema taifa limeingia katika mgogoro mpya wa raia kutoliamini Jeshi la Polisi, ambalo amesema badala ya kuwa kimbilio la watu wanaodai haki zao, sasa limekuwa la kuogopwa na kila mtu nchini.

Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema) na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema mgogoro huo umehamishiwa sasa kuwa wa kati ya Jeshi la Polisi na Chadema.

Alisema mbali ya mgogoro huo kuwa kati ya polisi na raia, pia unakusudia kwa nguvu zote na kwa gharama yoyote kuzima Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) linalosimamiwa na chama hicho.

Mbowe alisema Chadema wana taarifa za kina na za undani kwamba, baadhi ya viongozi wa serikali, ambao hawajajitokeza hadharani wamekuwa wakifanya kazi ya makusudi ya kuwasukuma polisi kuzuia mikutano ya chama hicho isifanikiwe.

Hata hivyo, alisema maazimio ya nini Chadema watafanya yatatolewa na CC, lakini akasema mkakati wowote wa kukizuia chama hicho kisiendeleze M4C hautafanikiwa.

Alisema Chadema wanaipenda sana Tanzania na kuithamini amani ya nchi na kwamba, wana uwezo wa kutafakari mustakabali wa taifa kuliko uwezo alionao Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.

Hivyo, akamtaka Tendwa asitoe vitisho vya kukifutia usajili chama chochote cha siasa nchini, na kuongeza kuwa kama anataka kufanya hivyo, aanze kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Na tunamwambia Tendwa kauli zake zinahatarisha usalama wa taifa. Chadema siyo chama cha mfukoni. Chadema ni chama kinachoaminiwa na Watanzania kwa mamilioni. Anapofikiri yeye ana mamlaka ya kuifuta Chadema ama chama kingine, acheze na vyama vingine, lakini asicheze na Chadema, Chadema is a way of life (Chadema ni njia ya maisha). Tunaipenda nchi yetu, hatupendi Tendwa atuingize kwenye matatizo,” alisema Mbowe.

Alisema msajili wa vyama vya siasa na sheria mbovu zilizotungwa kudhibiti vyama zisitumike kuvrugua amani ya taifa na kumtaka Tendwa kutolewa madaraka ya kuwa msajili wa vyama kwa kuwa kiranja wa CCM.

Mbowe alisema wanachotaka kukifanya ni kutengeneza ushindani wa kisiasa uliokuwa wa haki kwa faida na mustakabali mwema wa taifa.

Alisema bila kujali wataingizwa kwenye matatizo kiasi gani, operesheni za M4C zitaendelea kama kawaida nchi nzima sambamba na hatua, ambazo baada ya kikao hicho watakuwa wamekubaliana na viongozi wenzake kuchukua ili kuhakikisha amani, haki ya kusema na kusikilizwa zinapatikana.

Aliwapa pole na kuwapongeza wanahabari wote waliokuwa kwenye eneo la tukio wilayani Mufindi wakati matukio yote ya vurugu hizo yanatokea.

Alisema wanahabari hao walionyesha ujasiri uliosaidia kuliokoa taifa, Chadema na dhamira yake nzuri iliyokuwanayo dhidi ya mkakati wa makusudi uliokuwa umepangwa wa kukichafua chama hicho.

Mbowe alisema wanahabari hao walipiga picha katika mazingira ya vita na picha hizo zimeokoa usalama wa taifa.

"Polisi wameua mfululizo kwa muda mrefu, lakini wamekuwa wana-get away with it (bila kuwajibishwa). Wanaunda tume ambazo zinawalinda wao wenyewe huku wakiendelea kuiua Chadema na kuua viongozi wa Chadema. Lakini tunashukuru sana,” alisema Mbowe.

CHANZO:NIPASHE

No comments: