Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry
KAMATI ya Utendaji ya Simba SC
inatarajiwa kukutana kesho katika kikao cha dharula, kupanga tarahe ya Mkutano
Mkuu kwa lengo la kuomba Baraka za wachama wake kujitoa kwenye Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, kutokuwa na kutokuwa na imani na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Zacharia Hans Poppe, Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Simba SC, ameiambia BIN ZUBEIRY usiku huu kwamba,
kutokana na mwenendo huo wa TFF wameona hawatendewi haki na sasa wanaona bora
tu wajitoe ili shirikisho hilo licheze ligi na timu inazozipenda.
Hatua hiyo inafuatia Kamati ya Sheria,
Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa,
kuwaidhinisha Mbuyu Twite na Kevin Yondan kuchezea Yanga katika msimu ujao wa
Ligi Kuu, unaoanza mwishoni mwa wiki.
Kikao cha Kamati hiyo, kilichomalizika
hivi karibuni, pamoja na maamuzi hayo, kimeipa Yanga siku 21 kulipa dola 32,000
ambazo Simba SC ilimlipa Twite ili ajiunge nao, lakini baadaye akaghairi na
kusaini na kuhamia Yanga.
“Kanuni zipo wazi, klabu inapotaka
kumsajili mchezaji lazima kwanza izungumze na klabu yake, lakini katika usajili
wa Yondan, Yanga hawakufanya hivyo,”alisema Hans Poppe.
Uamuzi wa Kamati hiyo leo, unafuatia
kikao cha pamoja baina ya Simba na Yanga Jumatatu iliyopita kuvunjika bila kufikia
makubaliano kuhusu mustakabali wa wachezaji hao.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya
saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki
Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Makamu wake Mwenyekiti, Clement Sanga
na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti,
Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Hans Poppe.
Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko
ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini
mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine
2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo,
mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali
kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi
waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema
viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage
ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite
yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi
hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia
maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba
10, mwaka huu, yaani leo.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni
Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu
yao.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana
Jumapili iliyopita asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo
na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata
suluhu siku iliyofuata.
No comments:
Post a Comment