MVUTANO kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umechukua sura mpya baada
ya chama hicho kutangaza uhasama dhidi yake kikieleza kuwa hakiko tayari
kufanya naye kazi hadi atakapowaomba radhi.Wakati Chadema
kikisema hayo, Msajili huyo amejibu madai hayo akisema hatakubali kuona
chama hicho kikikaidi maagizo yake, likiwamo la kusitisha Operesheni
Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
Septemba
4, mwaka huu Tendwa alitishia kukifuta Chadema baada ya matukio ya
vurugu katika mikutano yake ukiwamo ule uliofanyika Iringa na
kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha
Televisheni cha Channel Ten, Daud Mwangosi.
Baada ya kauli hiyo, chama hicho kilijibu mapigo na kumtaka msajili huyo aanze kwanza kukifuta Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msimamo wa Chadema
Akizungumza
na waandishi wa habari juu ya maazimio ya mkutano wa dharura wa Kamati
Kuu (CC) ya chama hicho kujadili hali ya siasa nchini, uliofanyika Dar
es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza uadui na
Tendwa akisema chama hicho hakitafanya kazi na Ofisi ya Msajili mpaka
Tendwa atakapoondolewa.
Mbowe alisema Chadema kimefikia uamuzi huo kwa madai kuwa msajili huyo anafanya kazi kwa kuegemea upande mmoja wa CCM.
“Kutokana
na utendaji dhaifu wa Tendwa unaoegemea upande mmoja na uliojaa
‘propaganda’, Kamati Kuu ya Chadema imetangaza kuwa Tendwa ni adui wa
demokrasia na hafai kuwa katika nafasi aliyonayo,” alisema Mbowe na
kuongeza:
“Kamati kuu imeazimia kuendelea kuheshimu sheria ya
vyama vya siasa, lakini Chadema haitashiriki shughuli yoyote
itakayosimamiwa na Tendwa hadi atakapoondolewa katika nafasi yake na
kuteuliwa mtu mwingine.”
Mbowe alisema matamshi na barua
zinazotolewa na msajili huyo dhidi ya Chadema zinaonyesha kuwa yupo
katika nafasi hiyo kwa masilahi ya CCM hivyo akiendelea kushika wadhifa
huo ataliingiza taifa katika vurugu.
Tendwa ajibu mapigo
Tendwa
alisema hatakuwa tayari kuona Chadema kinaendelea kufanya maandamano
ambayo alidai ndiyo chanzo cha kuibuka kwa vurugu nchini. Alisema Sheria
ya Vyama vya Siasa ipo wazi na hatasita kuitumia kukiadhibu.
“Sheria
zipo na taratibu za kufuata zipo, tutachukua hatua, hatuwezi kuona
mikutano inafanyika na watu wanakufa halafu tuendelee kukaa kimya. Wao
si wanapingana na mimi, ngoja tu sheria itachukua mkondo wake, hili si
tatizo maana sheria zipo wazi kabisa.”
Alisema tayari alishatoa tahadhari kwa chama hicho lakini anaona bado kinaendelea kukaidi maagizo yake.
Katika
kauli yake ya Septemba 4, mbali na kutishia kukifuta Chadema pia
alisema atachukua uamuzi huo kwa chama chochote cha siasa ambacho
kitakaidi amri za polisi na kusababisha vurugu.
Alisema mfululizo
wa mauaji ya wananchi katika mikutano ya siasa unatokana na vyama hivyo
kukinzana na polisi na wakati mwingine, kutumia lugha za matusi na
vitisho vingine dhidi ya wabunge halali wa majimbo husika.
Wamshukia Nchimbi, Mwema
Katika
hatua nyingine, Chadema kimewataka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, Mkuu wa
Operesheni ya Jeshi hilo, Kamishna Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile wajiuzulu nyadhifa zao.
Mbowe alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na watu kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi ambao wanasimamiwa na viongozi hao.
Mbowe
alisema kuwa chama hicho hakiko tayari kufanya kazi na kamati ya
kuchunguza tukio zima lililosababisha kifo cha Mwangosi, ambayo
iliteuliwa na Dk Nchimbi.
Sambamba na hilo, chama hicho pia
kimeitaka Serikali kuwakamata na kuwafungulia mashtaka ya mauaji Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, Mkuu wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Morogoro na askari waliohusika katika
vurugu za Morogoro na Iringa ambazo zilisababisha vifo.
Mbowe
alisema kukamatwa kwa maofisa hao kutawafanya viongozi na watawala
wengine kufanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na taratibu
zilizopo, ikiwa ni pamoja na kutambua na kuthamini uhai wa binadamu.
“Kutokana
na mfululizo wa mauaji yanayofanywa na polisi katika shughuli za
kisiasa za Chadema na mipango ya baadhi ya viongozi wa Serikali ya
kudhibiti Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), kwa mbinu haramu, Kamati Kuu
imezingatia masuala mbalimbali na kupitisha azimio la kumwandikia barua
Rais Jakaya Kikwete,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Lengo la barua
hiyo ni kumshauri achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka
yake na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, aunde tume huru ya kuchunguza
vifo vyenye utata.”
Mbowe alisema iwapo Serikali haitazingatia
ushauri huo, Chadema kitawaongoza wananchi kwa njia za kidemokrasia
ikiwamo maandamano ya amani, kushinikiza hatua za haraka kuchukuliwa kwa
masilahi ya taifa.
Alisema Kamanda Kamuhanda na wenzake wanatakiwa kushtakiwa kwa kuwa tukio la mauaji ya Mwangosi lilitokea wakiwa eneo la tukio.
“Waziri
Nchimbi ambaye ndiye anayesimamia jeshi hili pamoja na wenzake tunataka
wawajibike au kuwajibishwa kwa kuwa wananchi wamekufa chini mikono ya
askari polisi. Mkuu wa FFU wa Mkoa wa Morogoro na Kamanda wa Polisi
Iringa nao walihusika kwa kuwa mauaji yalitokea wao wakiwa eneo la
tukio,” alisema Mbowe.
“Kamati Kuu imejadili kwa kina mfululizo wa
mauaji ya watu wetu ambayo hutokea kwenye mikutano na shughuli za
Chadema. Vifo ni vingi lakini sisi tumeelekeza katika vifo vilivyotokea
Arusha Mjini, Arumeru, Igunga, Singida, Morogoro na Iringa,” alisema
Mbowe.
Alisema lengo la uchunguzi ni kutaka kupatikana kwa
wahusika walioshiriki mauaji hayo bila kujali nyadhifa zao, ili
wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua kwa kuwa hilo
ndilo litakalojenga msingi wa taifa kubaki katika hali ya amani.
..Yawatimua madiwani wake Mwanza
Chama
hicho kimetangaza kuwavua uanachama madiwani wake wawili wa Mwanza,
Adamus Changulani (Igoma) na Henry Matata (Kitangile) kwa madai ya
kukiuka kanuni na maadili ya chama.
Mbowe alisema hatua hiyo
imetokana na uchunguzi kubaini kuwa walitumiwa na Serikali pamoja na
wale wa CCM, kushiriki katika tukio la kumwondoa aliyekuwa meya wa jiji
la Mwanza.
“Suala la kuondolewa kwa meya kama taratibu zimefuatwa
hakuna tatizo na hicho ndicho Chadema inachokipigania. Lakini hatua
zilizochukuliwa dhidi ya meya wa jiji hilo hazikufuata taratibu na
tulibaini kuwa viongozi wetu wamehusika. Tumechukua hatua bila kujali
wadhifa wa wahusika,” alisema Mbowe.
CHANZO :MWANANCHI
No comments:
Post a Comment