ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 3, 2012

MAPENZI NI MCHAKAMCHAKA, FEDHA NI DEREVA WA MOYO-2


NI wiki nyingine tunapokutana katika ukurasa huu kujuzana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa mapenzi. Tunaendelea na mada yetu tuliyoianza wiki mbili zilizopita. 
Tena wao si gharama, kwa maana ndiyo kazi yao.
Vilevile kwa mwanaume, atampuuza mtu anayempenda na kumvaa mwingine anayemuona anavutia zaidi. Wengi wamefanya hivyo bila kujua kwamba hao wanaovutia barabarani, asilimia kubwa ni magubegube. Unahitaji mwandani wa maisha yako? Tuliza akili.

Sikukatazi kutupa ndoano, ila jaribu kufikiria mara mbili. Uliyenaye hakutoshelezi? Kumuacha mpenzi wa kweli na kujishughulisha na wengine ni sawa na mfano wa mtu aliyepoteza almasi, wakati alipokuwa ‘bize’ akitafuta mawe. Usilie kama wenzako, tuliza akili leo.
Kuna watu wanateseka leo. Wanadai wana mkosi. Eti, mapenzi yanawachapa bakora kwamba hawana bahati nayo. Kama na wewe upo kwenye kundi hili, fumba macho halafu ufikirie ulipotoka. Je, hukumuacha aliyekupenda kwa dhati? Hukuchezea moyo wa yule aliyekuwa anakujali?
Kama jibu ni ndiyo, basi hutakiwi kulia. Mapenzi yalivyo, kupata mwenye moyo mkunjufu katika kupenda ni bahati nasibu. Hivyo basi, kama ulimchezea, ni zamu yako kuteseka kwa maana uliyachezea mapenzi. Ulimpiga teke anayekupenda, sasa unahangaika na wasiokupenda. Wanakuinjoi tu.
Lengo hapa ni kwenda tukifumbuana macho. Wapo watu wanaoamini kwamba ni wajanja sana, huku wakiendekeza staili zao za kuchezea nyoyo za wenzao. Unapaswa kuacha aina hiyo ya maisha kwa maana haitakusaidia, zaidi ya yote itakutesa mbele ya safari.
Nimeshaeleza mfano wa fedha. Nikazie hoja hapa kwamba endapo utaondoka kwa mtu anayekupenda na kuhamishia penzi lako kwa mwingine kisa ana fedha nyingi, hivyo ukaamini maisha yako yatakuwa mazuri sana, kaa ukitambua kuwa huyo naye si tajiri namba moja duniani.
Utakwenda kwa huyo unayedhani ana fedha, ukashikwa na hadaa kwamba atakupa maisha mazuri, lakini kwa vile naye si tajiri namba moja duniani, akija mwingine mwenye fedha zaidi atakung’oa. Matokeo ya jumla ni wewe kugeuka mtumwa wa wanaume wenye fedha.
Ukishaitwa mtumwa wa wanaume wenye fedha, maana yake hakutakuwa na tofauti kati yako na yule anayejiuza. Je, una amani gani kuhamahama? Dunia hii iliyojaa maradhi, ni vizuri sana ukawa mtulivu. Ukiyatendea haki mapenzi yako, ni rahisi kuwa na maisha bora.
Nakupa mfano: Shania ni binti mrembo. Urembo wake ni wa hali ya juu mno. Amesifiwa na wengi kwamba mvuto wake unatosha kumshawishi kimapenzi mwanaume yeyote yule. Sifa zilipokuwa nyingi, kichwa kikavimba, mabega akapandisha. Yeye ndiye yeye, utamueleza nini?
Akiwa A-Level, alikutana na Shadrack, wakapendana. Kila mwanafunzi akajua uhusiano wao. Wenyewe wakapeana ahadi motomoto kuwa watafika mbali, huku wakila viapo vya kufunga ndoa na kudumisha mapenzi yao bila kuachana mpaka kifo kitakapowatenganisha.
Miezi sita ya uhusiano wao, Shadrack alimuona Shania na mwanaume lakini kutokana na namna anavyomuamini, wala hakumfikiria tofauti. Wakati Shadrack hakujali chochote, Shania kwa sababu lilikuwa tukio baya, alipokutana na mwenzi wake akaanza kujikanyagakanyaga.
“Unajua yule ni rafiki wa kaka yangu, hata nyumbani kwetu huwa anakuja,” Shania alishusha utetezi bila kuulizwa. Shadrack akauliza: “Unamuongelea nani?” Alipopewa majibu akashangaa. Akasema: “Hukuwa na haja ya kunifafanulia chochote, sijahisi chochote, wewe kaa na amani kabisa.”
Haikupita muda, Shadrack akagundua kwamba Shania anatoka kimapenzi na yule jamaa aliyemkuta naye. Ilimuuma sana, kwani walikuwa wamepeana ahadi nyingi mno. Mwisho akakubali yaishe kwa sababu maisha yanaendelea bila mapenzi. Akazingatia masomo yake.
Kumbe tabia ya Shania ni kuzingatia fedha kuliko utu. Hata alipoamua kujiweka kwa Shadrack ni kwa sababu alimuona ana unafuu wa kimaisha kuliko wanafunzi wengine wa kiume. Shadrack alikuwa anajiweza kiasi, vilevile darasani alikuwa vizuri, kwa hiyo kuwa naye akaona wanafunzi wenzake wa kike watamkoma.
Japo anajiweza lakini Shadrack alikuwa mwanafunzi, kwa hiyo hakuwa na wigo mpana wa kipato kuweza kumhudumia Shania. Hii ikasababisha Shania ampate huyo jamaa mbaye alikuwa mfanyakazi, ofisi ya Mkuu wa Mkoa. 
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info

No comments: