Waandishi Wetu
TUKIO la kuuawa kwa mwandishi wa habari wakati polisi wakipambana na wafuasi wa Chadema mkoani Iringa, limelitikisa jeshi hilo na jana Mkuu wake (IGP), Said Mwema alilazimika kujifungia na vigogo wa polisi Mkoa wa Iringa kujadili suala hilo.
Wakati IGP Mwema akifanya mkutano huo, uliodumu kwa zaidi ya saa mbili na nusu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi amelazimika kukatisha ziara yake ya kikazi Afrika Kusini na kurejea nchini kushughulikia suala hilo.
Mwema alienda Iringa jana na kuitisha mkutano huo uliowahusisha pia viongozi wa Chadema, akiwamo Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa katika mazingira yaliyoelezwa kuwa na ulinzi mkali.
Hii ni mara ya kwanza IGP Mwema kwenda mwenyewe kwenye mikoa kunakotokea vurugu kati na vyama vya siasa na baadaye mauaji ya raia.
Julai 15, mwaka huu vurugu za aina hiyo zilitokea mkoani Singida ambako Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Kata ya Ndago wilayani Iramba, Yohana Mpinga aliuawa kwa kupigwa na silaha za jadi.
Pia mkoani Morogoro, Ally Zona aliuawa katika vurugu zilizoibuka baina ya polisi na wafuasi wa Chadema katika haraka za jeshi hilo kuwasambaratisha wafuasi hao kwa kile ilichoeleza kuwa maandamano yao yalipigwa marufuku.
Katika vurugu zote hizo, IGP amekuwa akituma wawakilishi au kutumia polisi kwenye mkoa husika kushughulikia matatizo hayo.
Makubaliano ya kikao
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa polisi imekubaliana na Chadema na Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kusitisha majadiliano yote yanayohusu kifo cha mwandishi huyo hadi mazishi yake yatakapokamilika.
Mwenyekiti wa UTPC, Kenneth Simbaya alisema baada ya mkutano huo kuwa wamekubaliana kuwa na mkutano mwingine baada ya shughuli za mazishi kukamilika.
“Tulichoomba kifanyike ni kwamba, tumzike mwenzetu halafu majadiliano mengine juu ya ilikuwaje kwa nini na nini kifanyike kwa siku za usoni yatakuja,” alisema Simbaya.
Alisema sasa wanasubiri mwili wa Mwangosi ufanyiwe uchunguzi na wataalamu kutoka Dar es Salaam kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maandalizi ya mazishi.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Francis Godwin alisema uchunguzi wa awali wa IPC unapingana kwa asilimia zote na taarifa ya jeshi hilo kwa kuzingatia taarifa zilizotolewa na baadhi ya waandishi waliokuwapo katika tukio hilo.
“Taarifa kutoka katika vyanzo vyetu zinaonyesha kwamba Mwangosi alipigwa kwa virungu kabla ya kulipuliwa na bomu hilo ambalo kwa vyovyote vile mhusika wake mkuu anaweza kuwa jeshi hilo na ili taarifa hiyo potofu isiendelee kuugubika umma, IPC imeamua kutoa tamko linalolenga kuviarifu vyombo huru viingilie kati uchunguzi,” alisema Godwin.
Nchimbi akatisha ziara
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi jana alilazimika kukatisha ziara yake ya kikazi, Afrika Kusini na kurudi nchini ambako pamoja na mambo mengine, atazungumza na waandishi wa habari leo kuhusu tukio hilo.
Nchimbi anarejea nchini wakati Naibu wake, Pereira Ame Silima akikataa kulizungumzia akisema uchunguzi umeshaanza.
Silima alisema tukio hilo linachunguzwa kwa pamoja kati ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba na IGP Mwema... “Mwema na Manumba wanaelekea Iringa ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa tukio hilo na baadaye ndipo jeshi la polisi litaweza kueleza ni kitu gani hasa kimetokea.”
Alisema kwa sasa lolote litakalozungumzwa juu ya tukio hilo litakuwa ni hisia tu na ukweli utajulikana baada ya uchunguzi huo kukamilika.
Channel Ten yanena
Uongozi wa kampuni ya Africa Media Group ambao wanamiliki Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, umeitaka Serikali kuanzisha uchunguzi huru ili kubaini sababu na mazingira ya kuuawa kwa mwandishi huyo ambaye alijiunga na kampuni hiyo mwaka 2006.
Taarifa iliyotolewa na kampuni na kusainiwa na Mhariri Mkuu wa Channel Ten, Dina Chahali imetaka uchunguzi huru kufanyika na kuhakikisha wahusika wa tukio hilo wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Tunalaani vikali tukio hili ambalo halikubaliki kwa jinsi yoyote ile, tunataka kuanzishwa uchunguzi huru na hatimaye nguvu za kisheria zitumike,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment