Advertisements

Saturday, September 8, 2012

Serikali yasalimu amri


Yaagiza Waislamu wote waliozira kuhesabiwa waachiwe kwa dhamana ukamataji usitishwe.

Serikali jana imesalimu amri kwa kuwaagiza Makamanda wa Polisi wote nchini kuwaachia kwa dhamana waumini wa dini ya Kiislamu waliokuwa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukataa kushiriki kwenye zoezi la Sensa ya Watu na Makazi linalomalizika rasmi leo nchini.

Aidha, imealiagiza jeshi hilo kusitisha ukamataji wa watu kutokana na zoezi hilo.

Tamko lililotolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi , Mbarak Abdulwakil, kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo ambaye yuko nje nchi kikazi, liliagiza Waislamu hao wanaoshikiliwa kuachiwa kwa masharti ya dhamana baada ya majadiliano na viongozi wa Kiislamu.



Hii inafuatia maelfu ya Waislamu kutoka Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, jana kuvamia majengo ya ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kushinikiza kuachiwa huru kwa wenzao waliokamatwa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa sababu ya kukataa kuhesabiwa katika zoezi hilo.

Tamko hilo lililosomwa mbele ya Waislamu hao pia lilieleza kuwa mambo mengine yaliyotajwa kwenye risala ya Waislamu yatashughulikiwa mara baada ya Waziri mwenye dhamana na Naibu wake kurejea nchini.

Waumini hao wanawake kwa wanaume, walianza kumiminika katika maeneo hayo kwa nyakati tofauti kwa mafungu, kuanzia saa 7.30 mchana, baada ya Swala ya Ijumaa, wakitokea katika misikiti mbalimbali ya jijini Dar es Salaam na vitongoji vyake.
Waliongozwa na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na Sheikh Rajabu Katimba.

Kuanzia muda huo, barabara nyingi zilifungwa kupisha makundi ya waumini hao waliokuwa wakiandamana kwa amani kwenda katika maeneo hayo, huku wakipaza sauti kwa kutamka: “Takbiyr, Allaahu Akbar’, “Laa ilaaha Illallah.”

Baada ya kufika, walikusanyika nje ya majengo ya ofisi hizo na kuanza kuhamasishana pamoja na mambo mengine, kupinga hatua ya kukamatwa kwa wenzao.

Wakati hayo yakiendelea, waumini hao waliokuwa watulivu, walitumia wawakilishi wao wanne kwenda kuwasilisha risala yenye madai yao kwa uongozi wa wizara na Jeshi la Polisi.

Viongozi wa waumini hao waliokwenda kuonana na viongozi wa wizara pamoja na Jeshi la Polisi, ni pamoja na Amiri wa Umoja wa Wahadhiri wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Kondo Juma Bungo na Amiri wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kiislamu Tanzania (Tamsiya), Jafari Mneke.

Wengine ni Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, Sheikh Suleiman Abdallah na Mdhamini wa Taasisi ya Almallid, mzee Amani Mushi.

Kwa mujibu wa Sheikh Kondo, wakiwa katika ofisi hizo, walikutana na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbaraka Abdulwakil, pamoja na maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu na Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Alisema mazungumzo yao yaliyochukua zaidi ya saa tatu, yalifikia tamati baada ya Katibu Mkuu huyo kukubali kwa maandishi kwamba, Waislamu wote waliokamatwa kwa sababu ya kukataa kuhesabiwa katika sensa wataachiwa huru bila masharti yoyote.

Sheikh Kondo alisema Katibu Mkuu huyo pia alikubali kwamba, hakuna muumini yeyote atakayekamatwa tena kwa sababu ya kukataa kuhesabiwa katika sensa.

Alisema katika maandishi hayo, Abdulwakil aliahidi kuwa atawaagiza makamanda wa polisi wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha wanaagiza mara moja kuachiwa huru kwa Waislamu wote waliokamatwa na kushikiliwa kwa sababu hizo.

Awali, akisoma risala hiyo katika kikao hicho, Mneke alisema wanalaani vitendo vyote alivyoviita vya ‘unyama’ na ‘unyanyasaji’ alivyodai kuwa vimekuwa vikifanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya Waislamu na kutaka vikomeshwe mara moja.

Alisema wanapinga vitendo hivyo kwa kuwa wanaamini vinakwenda kinyume cha haki za raia na haki za binadamu.

Waislamu kupitia jumuiya na taasisi zao, wamekuwa wakipendekeza mambo matatu yatekelezwe katika sensa; ikiwamo kipengele cha dini kirejeshwe katika dodoso la sensa.

Mapendekezo mengine, ni kuwapo wawakilishi wa dini zote katika ukusanyaji wa takwimu na majumuisho na kuundwa tume huru ya sensa.

Kwa mujibu wa Mneke, mapendekezo hayo waliyasilisha serikalini sambamba na kutoa msimamo wa Waislamu kwamba, hawatawakabili watendaji wa sensa kuwazuia kufanya kazi yao wakati wa zoezi la sensa.

Pia Waislamu hasa walio chini ya Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania hawatashiriki sensa ya watu na makazi.

Hata hivyo, serikali kupitia Rais Jakaya Kikwete, ilitoa tamko la kutokukubaliana na mapendekezo hayo ya Waislamu.

Risala hiyo ilisomwa pia mbele ya umati wa waumini waliokusanyika katika maeneo hayo.

Baada ya wawakilishi wa Waislamu kurejea, walitoa taarifa kwa umati wa waumini waliofurika nje ya majengo ya ofisi hizo juu ya kilichojiri na mwafaka uliofikiwa katika kikao hicho kati yao na ujumbe wa wizara na Jeshi la Polisi.

Baada ya kupokea taarifa hizo, wauminin hao walilipuka kwa kupaza sauti kali za “Takbiyr, Allahu Akbar” na kuanza kuondoka katika eneo hilo kwa maandamano ya amani.

Walipita katika Barabara za Bibi Titi Mohamed na Morogoro na kwenda moja kwa moja hadi katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni, ambako pamoja na mambo mengine, walipeana taarifa zaidi kuhusiana na mustakabali wa haki na maslahi yao kama Waislamu.

Hata hivyo, Waislamu hao wamesema wanatarajia kufanya maandamano mengine katika siku watakayoitaja, kwenda Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) ya kumng’oa  Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Joyce  Ndalichako.

Imeandikwa na Muhibu Said, Hadija Kitwana na Aziza Adinani.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

hivi ndo inavyotakiwa mpaka kieleweka, haki ya rai yeyote katika nchi yake anayoishi awe na ID na passport,Europe mbwana na paka wanazo passport zao ukibisha fanya uchunguzi utaona, so inakuwaje sisi watanzania,hatuna najua uchumi wetu na wa Europe ni tafauti lakini si walikuja kwetu kuja kututawala tulikuwa tuna mali zetu wakaziiba na kukuza kwao kwa nini sasa sisi tusiweze sisi hatujawahi kwenda kwao kuwatawala na kuiba mali zoa kama tupo kwao basi tupo tu kwa kusaidia family zetu.

hivi ndo inavyotakiwa ndugu zangu waislamu tume lala mnoo mpaka tunaonekana wajinga hatukusoma hatujui umuhimu wa shule ila madrasa lakini waulize bila madrasa na kujui dini yetu ustaarabu wote ungetoka wapi,spain waliuliwa wangapi waislamu, knowledge imetoka wapi kama si kwa waislamu

tunachopinga hapa siyo kuhesabiwa ila zulma na njama wanazotufanyia kila siku na kila leo toka karne na karne lakin sasa mungu kishatufungua masikio na macho yetu na kutuzindua katika usingizi wetu na alhamdulillahi si haba.

hatupingi kuhesabiwa na hatupingi sheria za nchi ila tunachopinga njama zenu, msitufanye wajinga na watoto wadogo daima.

kama hakuna sheria ya kuwapa wananchi wake ID NA PASSPORT BASI KUSIWE NA SHERIA YA KUKAMATA MTU NA KUTIA NDANI ETI KISA KAKATA KUHESABIWA.

HATULALI TENA MPAKA KIELEWEKE NA UNYONGE WETU USICHUKULIWE KWAMBA NI UJINGA HATUNA SHULE TOKA ALIPOTUA MKOLONI SOMENI HISTORIA MUIJUYE WALIKUWA WANACHAGULIWA WAISLAMU KUFANYA KAZI ZA OKARANI OFFISINI NA HATA JESHINI ETC MLIKUWA WAPI NA SHULE YENU NA SISI MNAO TUCHEKA MADRASA YETU.
WADANGANYENI HAWA HAWA KIZAZI CHA LEO CHA AKINA DJ LUKE LAKINI SI KIZAZI CHA ZAMANI,MKITAKA UKWELI HIVI SASA TUTAKUPENI.

MADRASA DAIMA NA USILAMU MILELE AMIN.

KAZI KWAKO MKUU KUWEKA HII COMMENT AU KUBANIA