ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, September 5, 2012
UMEVUNJWA MOYO KIMAPENZI? ZINGATIA HAYA-2
KARIBU tena mpendwa msomaji wa kona hii ya mahaba ambapo leo tunaendelea na sehemu ya pili ya mada tuliyoianza wiki iliyopita ya kujifunza nini cha kufanya baada ya kuvunjwa moyo na mtu unayempenda. Tuendelee kuanzia pale tulipoishia.
SAMEHE NA SAHAU
Hakuna jambo ambalo hutuliza nafsi kama kuamua kumsamehe na kumsahau yule aliyekuumiza kabla hata hajakuomba msamaha. Yawezekana wengi wakajiuliza inawezekanaje kumsamehe mtu ambaye kwa makusudi ameamua kukusaliti kwa kutoka kimapenzi na mtu mwingine? Inawezekana kabisa na wote waliojaribu waliona mafanikio yake.
Kuendelea kuwa na kinyongo, kufikiria kulipa kisasi au kumdhuru aliyekusaliti ni kuendelea kujiumiza mwenyewe ndani ya nafsi yako. Zingatia kuwa unapochukia na kumkasirikia mtu fulani, humuathiri kwa chochote isipokuwa madhara makubwa yanakurudia wewe mwenyewe.
CHUNGUZA CHANZO CHA TATIZO
Hakuna jambo ambalo hutokea bila kuwa na sababu. Yawezekana mpenzi wake amekusaliti kwa sababu tayari alishakuwa na katabia ka kuwapanga wanaume au wanawake. Yawezekana pia kuwa kilichomponza ni tamaa ya fedha au ni kutafuta faraja kwingine baada ya kuona wewe humpi nafasi ya kutosha katika maisha yako au pengine humjali inavyotakiwa.
Baada ya kupatwa na maumivu, jiulize mwenyewe kilichosababisha ni nini. Ukigundua kuwa mwenzi wako ndiye alikuwa chanzo kwa kuendekeza tamaa ya fedha au kupenda kugawa hovyo penzi lake, basi huyo hakufai na jiambie kuwa utakapokuwa tayari kuanzisha tena uhusiano, ni lazima uwe na muda wa kutosha wa kumchunguza huyo unayetaka kumkabidhi moyo wako ili maumivu yasijirudie.
Pia endapo utabaini kuwa ubize wako, kushindwa kumthamini na kumuonesha mapenzi ya dhati ndiyo jambo lililosababisha akakusaliti, kubali makosa na jiambie mwenyewe kuwa mara nyingine utakapoamua kupenda, utarekebisha makosa yako ili usiwe mtu wa kulia kila siku.
JIJENGE KIIMANI
Yawezekana kwa kipindi kirefu umemsahau Mungu wako na hujashiriki katika ibada au sala za kumuomba kutokana na kuwa bize na huyo mpenzi wako aliyekuumiza. Huu ni wakati wako sasa wa kuanza upya kujijenga kiimani, kama ni Mkristo basi jitahidi kuhudhuria kanisani na kama ni Muislam, jitahidi pia kuhudhuria msikitini na kumuomba Mungu akuvushe salama katika kipindi kigumu ulichonacho. Watafiti wa kisaikolojia wanaeleza kuwa kuamini kuwa kuna nguvu kubwa kuliko vitu vyote (Mungu) husaidia kuyakabili matatizo uliyonayo na kuyaacha yapite huku ukiwa na imani kubwa kuwa huyo aliyekuumiza hakuwa riziki yako na ndiyo maana hayo yametokea.
ONESHA KUWA UNAWEZA KUISHI BILA YEYE
Wengi hukosea sana kujiapiza kuwa ‘siwezi kuishi bila wewe’. Kauli hii hugeuka msumari inapotokea huyo uliyekuwa unambimbia kila siku akakuumiza kwa makusudi. Tumeshuhudia marafiki na ndugu zetu wakijiua kwa kunywa sumu, kujinyonga au kujidhuru kwa namna yoyote kwa sababu wameumizwa na waliokuwa wanawapenda.
Jitofautishe na hao kwa kutambua thamani yako na kilichokuleta duniani. Usikubali kujitoa thamani kwa sababu ya kuumizwa na mapenzi, usifikirie kujiua au kujidhuru kwa sababu ya udhaifu wa mtu mwingine. Jiambie kuwa huyo hakuwa chaguo sahihi kwako na ndiyo maana hayo yametokea.
FUNGUA UKURASA MPYA
Anza maisha yako mapya na hakikisha hurudii makosa kama yaliyokusababishia maumivu hapo awali. Endelea kujipa thamani unayostahili na jiambie ipo siku utampata chaguo sahihi.
www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment