NI KESHO ASUBUHI, LENGO NI KULAANI MAUAJI YA DAUD MWANGOSI, KUTOA MATAMKO
Frederick Katulanda
WAANDISHI
wa habari nchini kesho wataandamana nchi nzima kwa amani kulaani kuuawa
kwa mwandishi mwenzao, Daud Mwangosi aliyeuawa Septemba 2, mwaka huu
katika Kijiji cha Nyololo, Iringa.
Maandamano hayo ambayo yatakuwa
ya kimyakimya yatafanyika katika mikoa yote nchini kuanzia saa 2:00
asubuhi na waandishi watakaoshiriki katika maandamano hayo watavaa ama
nguo nyeusi au watafunga vitambaa vyeusi mkononi ikiwa ni ishara ya
kuomboleza na kulaani kuuawa kwa mwenzao.
Kaimu Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Theophil Makunga alisema kuwa uamuzi
wa kufanyika kwa maandamano hayo ulifikiwa katika kikao cha jukwaa hilo
kilichofanyika Dar es Salaam juzi.
Alisema kwa Mkoa wa Dar es
Salaam, maandamano hayo yamepangwa kuanzia katika Kituo cha Televisheni
cha Channel Ten, Mtaa wa Jamhuri ambacho Mwangosi alikuwa akikitumikia
na kupita katika Mtaa wa Azikiwe, Barabara ya Bibi Titi hadi katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja ambako maandamano hayo yatahitimishwa.
Alisema
baada ya kufika katika viwanja hivyo, yatapokewa na viongozi wa TEF na
kisha baadhi ya waandishi waliokuwapo katika eneo la tukio watatoa
ushuhuda wa kilichotokea na kufuatiwa na mjadala kuhusiana na mauaji
hayo na kutoa tamko la pamoja.
“Kutatolewa ushuhuda kutoka kwa
waandishi wa habari ambao walishuhudia tukio la kuuawa kwa mwandishi
mwenzao, wataeleza kwa kina hali halisi na ukweli waliouona siku ya
tukio,” alisema Makunga.
Alisema tayari wamekwishawasiliana na
Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ambako wamepeleka barua ya kuomba
ulinzi kesho wakieleza njia watakazopitia siku hiyo.
“Tunafanya
matembezi ya amani, kimyakimya kwa lengo la kulaani tukio la kusikitisha
la kuuawa kwa Mwangosi. Ni mwandishi wa kwanza hapa nchini kuuawa akiwa
kazini na doa kubwa kwa nchi yetu na vyombo vya dola, hivyo lazima
tulilaani tukio hilo.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha
Minangi alisema, hajapokea barua hiyo na kusema kwamba inawezekana ipo
kwa wasaidizi wake na hivyo kuahidi kuifanyia kazi.
“Sijaiona
barua yao, inawezekana ipo kwa maofisa wangu au wameipeleka kwa Kamanda
wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, nitafuatilia kujua ili kuona jeshi
langu litafanya nini,” alisema.
Makamu wa Rais wa Umoja wa Klabu
za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Jane Mihanji alisema kwamba
lengo la maandamano hayo ni kulaani mauaji ya Mwangosi na zaidi ni
kufikisha ujumbe kwa Serikali.
“Hatukupendezwa na mauaji hayo,
yametuumiza na hatutopenda yatokee tena, tunayalaani na kuomba hatua
kali zichukuliwe,” alisema Mihanji.
Maandamano mikoani
Mkurugenzi
wa UTPC, Abubakar Karsan alisema, sambamba na maandamano hayo Dar es
Salaam, pia waandishi wengine mikoani nao wataandamana kuungana na
wenzao kulaani mauaji hayo ya mwenzao.
Maandamano ya mikoa yote
nchini yatasimamiwa na klabu zote za waandishi wa mikoa husika na kwamba
maandalizi yake ni pamoja na kubainisha njia watakazopitia kwa upande
wa mikoani, yamekwisha kamilishwa. Alisema maandamano hayo yatapokewa na
wenyeviti wa klabu ambao watatoa matamko mbalimbali kuhusiana na kifo
cha Mwangosi.
“Kila mkoa hapa nchini utashiriki maandamano,
wataandamana kwa amani kuungana na wenzao kulaani kifo cha mwandishi
mwenzao, nao kama ilivyo kwa Dar es Salaam watavaa nguo nyeusi au
vitambaa vyeusi mkononi,” alisema.
Alisisitiza kwamba kama
itakavyokuwa kwa yale ya Dar es Salaam, maandamano hayo hayatahusisha
kiongozi yeyote wa Serikali, chama cha siasa au wanaharakati, bali
waandishi wa habari wenyewe viongozi wao.
Mratibu wa Klabu ya
Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko alisema kuwa maandalizi
kwa ajili ya maandamano hayo yamekamilika. Alisema yataanzia katika
Viwanja vya Ghand Hall, kupitia Barabara za Uhuru, Mlango Mmoja, Nyerere
na kuingia katika Barabara ya Miti Mirefu, Pamba, Barabara ya Kenyatta
hadi Uwanja wa Nyamagana.
Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari
Mkoa wa Dodoma, Habel Chidawali alisema, ofisi yake ilikuwa katika
maandalizi ya kufanikisha maandamano hayo akisema kwamba hadi leo jioni
watakuwa katika nafasi nzuri ya kutangaza njia watakazopitia na mahali
yatakapoishia.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa
Mbeya, Christopher Nyenyembe alisema kwamba pia wako katika maandalizi
ya kukamilisha maandamano hayo.
“Tunazo sababu za kuandamana
kuungana na wenzetu nchi nzima, tulikwisha toa tamko letu kulaani mauaji
hayo ikiwa ni pamoja na kususia kuandika habari za polisi, lakini
katika maandamano hayo tutatoa tena tamko,” alisema
No comments:
Post a Comment