ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 3, 2012

WAANDISHI NA WANANCHI DODOMA WALAANI KIFO CHA MWANDISHI WA HABARI WA CHANEL 10

Marehemu Daud Mwangosi.

SEPTEMBER 03.2012   
CHAMA cha waandishi wa habari mkoa wa Dodoma (CPC) wamelaani vurugu zilizotokea jana mkoani Iringa na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari wa kituo cha utangazaji cha Chanel Ten Daud Mwangosi.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa chama hicho Habel Chidawali alipokuwa akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari mkoani hapa. Chidawali amesema kuwa kamwe chama hicho hakikubaliani na nguvu kubwa iliyotumiwa na jeshi la polisi kwa ajili ya kumwaga damu ya mwandishi huyo ambaye hakuwa na hatia na kamwe jeshi la polisi haliwezi kujitetea kwa kudai kifo cha mwandishi huyo ni bahati mbaya.
 Amesema kuwa jeshi la polisi limekuwa likionyesha wazi wazi kuwa linatumia nguvu,ubabe na matumizi mabovu ya silaha za moto ambayo hayajaweza kusaidia siku zote na badala yake kinachoachwa ni maumivu na vilio kwa wananchi.
Katibu huyo  amesema kama jeshi la polisi linatuliza ghasia hakuna siku hata moja haijatokea wakamuua kiongozi yoyote wa siasa ambao ni vinara wa mikutano mbalimbali.
Kwa upande wao wananchi mbalimbali mkoani hapa wamekemea nguvu kubwa inayotumika na Polisi katika vurugu mbalimbali zinazotokea.
Wamesema tabia ya jeshi la polisi kutumia nguvu na silaha za moto ambazo zinasababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia.
 Catheline Muhinte, amesema kuwa tukio lililofanywa na jeshi la polisi la kumuua mwandishi wa habari linaonyesha dhairi kuwa kwa sasa jeshi hilo linafanya kazi kwa kukiuka maadili ya malengo yao.
 Amesema katika mwonekano wa picha ambazo zinaonekana katika vyombo mbalimbali vya habari  inaonyesha dhairi kuwa polisi walihusika moja kwa moja na kifo cha mwandishi huyo.

No comments: