ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 16, 2012

Barazani Leo


Salma Said, Zanzibar
Mswada wa kudhibiti vitambulisho wawasilishwa
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewasilisha mswada wa kudhibiti utoaji wa ovyo wa vitambulisho vya mzanzibari mkaazi (ZanID) na kuwadhibiti wageni wenye kupewa vitambulisho hivyo kinyume na sheria.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Mwinyihaji Makame Mwadini wakati akiwasilisha mswada wa marekebisho ya sheria ya Usajili wa Mzanzibari Mkaazi Namba 7 ya mwaka 2005, na mambo mengine yanayohusiana na hayo katika kikao cha baraza la wawakilishi jana kinachoendelea Chukwani Mjini Zanzibar.

Dk Mwadini alisema lengo la serikali kufanya marekebisho hayo ni kutokana na sheria iliyopo kutokidhi haja ya wakati huu na kuwa hairuhusu kuwasajili wageni na sasa chini ya sheria mpya wageni wataweza kusajiliwa na kupewa vitambulisho.

Sababu kubwa ya kuandaliwa kwa marekebisho hayo serikali Dk Makame amesema imeonekana hivi sasa mtandao wa kusajili Wazanzibari Wakaazi kwa kutumia mbinu za udanganyifu umekuwa mkubwa na unaendelea kukuwa siku hadi siku jambo ambalo linaigharimu fedha kubwa serikali.
  


Alisema pia wapo baadhi ya wageni ambao wamekuwa wakipewa vitambulisho kinyume na sheria ya usajili wa vitambulisho hivyo jambo ambalo limekuwa likiwanyma fursa wenyewe kupata vitambulisho hivyo.

Waziri huyo alisema kwa wale ambao wamepatiwa vitambulisho hivyo kinyume na sheria tayari taarifa zao hivi sasa zipo uhamiaji na wanashughulikiwa na mamlaka zinazohusika.

Sababu nyengine ni kuwa watahesabiwa na kuifanyia marekebisho sera ya vitambulisho na utoaji wa viambulisho kwa wageni ambapo tayari sera imeshakubaliwa.

Waziri huyo alisema Serikali sasa itaweza kuwatambua wageni wote wanaoingia nchini na kuwatambua wanapoishi, wanapofanya kazi na kama wameingia kinyume na sheria ambapo kwa kiasi Fulani kunachangia kuwepo kwa vitendo vya kihalifu na ukiukwaji wa maadili.

Aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba katika hali ya sasa ni vigumu kudhibiti wageni wenye kuishi kinyume na sheria na hivyo kushindwa kuwadhibiti na kusababisha uhalifu lakini chini ya sheria hiyo itawezekana kudhibitiwa na kupunguza uhalifu na kuweka usalama.

Aidha Dk Mwadini alisema vitambulisho hivyo havitakuwa na ruhusa ya kuishi nchini bali vitambulisho vya kuishi nchini ni vile vitakavyotolewa na idara ya uhamiaji.

Akizungumzia vitambulisho hivyo vitakavyoisaidia serikali Dk Mwadini alisema chini ya sheria hii serikali itaweza kupanga mipango yake ya maendeleo kwa kuwatambua wakaazi wake ikiwa pamoja na kusaidia mamlaka zake za kodi.


Dk mwadini alisema chini ya sheria hiyo Serikali inaendelea na shughuli zake kwa mtandao (database) na pia kuendelea na kuwa na utaratibu wa vizazi na vifo, ambapo marekebisho ya sheria hiyo itawezesha serikali kuwatambua wageni waliopo nchini pamoja na wenyeweji wote. 

Taarifa hizo zitasaidia katika uchumi na maendeleo na itasaidia kuokoa fedha nyingi zinazopotea katika kufanya sensa ya watu ambapo chini ya sheria hiyo hakutakuwa na sababu ya kutumika fedha nyingi kwa ajili ya kuhesabu watu.
Mswada huo unakuja ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maoni mbali mbali ya Wananchi wa Zanzibar wakiwemo viongozi wa Baraza la Wawakilishi kudai kuwapo kwa vitendo vya utoaji ovyo wa Vitambulisho Mzanzibari Mkaazi.

Kwa nyakati tofauti wajumbe wa baraza la wawakilishi wamekuwa wakilalamikia utoaji wa vitambulisho vinavyotolewa kwa wageni na kunyimwa wazanzibari wanaohusika kupewa.
Miongoni mwa wawakilishi waliotoa ushahidi wa vielelezo vya wageni waliopewa vitambulisho ni Mwakilishi wa Jimbo la Kitope (CCM), Makame Mshimba Mbarouk ambapo alisema kumekuwepo watu wenye asili ya Kenya wamekuwa wakimiliki vitambulisho hivyo kwa wingi na kuonesha orodha ya wageni hao.

Mwakilishi huyo na wengine walidai ni mambo ya kusikitisha kuona baadhi ya watu ambao wana asili ya Zanzibar, lakini wamekuwa hawana vitambulisho hivyo baada ya kunyimwa barua kutoka kwa masheha.

Hata hivyo viongozi hao baada ya kuukagua mfumo wa utoaji wa Vitambulisho hivyo katika taasisi husika wajumbe hao walipendekeza kuwapo kwa marekebisho ya sheria ili kuweza kuwabana wanaoonekana kwenda kinyume na sheria hiyo.
  Tatizo la umeme ni baharini na sio transfoma

NAIBU waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Makame Mwadini amesema kuwa tatizo la uhaba wa umeme katika baadhi ya maeneo linatokana na laini kubwa ya umeme iliyopo baharini na sio transfoma.

Katika suali lake la nyongeza Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Hussein Ibrahim Makungu (CCM) alitaka kujua sababu zinazosababisha kuzorota kwa umeme ambapo katika jimbo lake kumekuwepo na usumbufu mkubwa wa wananchi kutokana na kukosekana huduma hiyo mara kwa mara.
Akijibu suali la nyongeza la Naibu waziri huyo alisema kwamba laini hiyo ya umeme iliyopo baharini ina uwezo wa kuchukuwa umeme megawati 45 ambazo hazitoshelezi kwa umeme wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema kuwa tatizo hilo litaweza kuondoka muda mfupi kuanzia sasa mara baada ya kukamilika kwa ulazaji wa laini mpya ya umeme ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukuwa umeme megawati 100.
Aidha Mwakilishi wa jimbo la Wawi, Nassor Saleh Juma (CUF) alitaka kujua ni lini Serikali itawapunguzia wananchi gharama za uungaji wa umeme ili wapate huduma hiyo na hatimae waende samabamba na utandawaji.

Akijibu suali hilo msingi alisema kuwa  Serikali inaendelea na mpango wake wa kuwaungia umeme wananchi kwa njia ya mkopo ili kuwapunguzia mzigo wananchi wa kulipa gharama zote kwa pamoja.
 Mwadini alisema kuwa Shirika la umeme linaendelea kujenga umeme wa mbali kwa wale wananchi wanaounda vikundi katika vijiji kwa gharama za Shirika na wananchi kulipia gharama ndogo ya kuungiwa umeme ndani ya nyumba zao.

Wizara ya uvuvi kuimarisha ufugaji
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar imeandaa waraka maalumu kuhusu mpango wa kuimarisha ufugaji wa kuku Zanzibar kwa kuwaombea kusaidiw akwa pembejeo za uzalishaji wa mifugo ikiwemo chakula na madawa ili wafugaji hao waweze kuzalisha kwa gharama nafuu.

Waziri wa wizara hiyo Abdilahi Jihadi Hassan akijibu suali la mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM), Jaku Hashim Ayoub alisema kuwa hatua hiyo pia itaweza kuwasaidia wafugaji hao kuuza bidhaa zao kwa bei ya kuvutia ili waweze kushindana na wazalishaji kutoka nje ya nchi.

Alisema kuwa waraka huo umekwisha wasilishwa kwenye kamati ya makatibu wakuu kwa matayarisho ya kuwasilishwa Serikalini.

Hata hivyo alisema kuwa Serikali imepanga mpango wa kuwasaidia wafugaji hao wa kuku kwa kuwapatia taaluma ya uzalishaji wa bidhaa bora zinazovutia  soko kwa ufanisi.

Mapema mwakilishi huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwalinda wafugaji wa ndani ya nchi kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la nyama ya kuku kutoka nje.


Tiketi kwa vitambulisho
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea na utaratibu wake wa kutumia vitambulisho wakati wa ununuzi wa tiketi za kusafiria.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Ussi wakati akijibu suali la Mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM),  Jaku Hashim Ayoub katika kikao cha baraza hilo kilichoendelea Mjini Zanzibar.
Mwakilishi huyo alihoji ni kwa nini serikali imeshindwa hadi sasa kutekeleza ahadi yake ya kutumia utaatatibu wa vitambulisho wakati mtu anapotaka kununua tiketi na kusafiri kwenda Dar es Salaam au Pemba.

Ussi aliwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba kimsingi serikali haijashindwa na azma hiyo ya kutekeleza ahadi yake ya kutumia utaratibu wa abiria kuuziwa tiketi baada ya kuonyesha kitambulisho.
Na kuongeza kwamba utaratibu huo ndio unaotumiwa na hivyo itaendelea nao kwani unasaidia kwa kuweza kuwatambua waliosafiri hasa wakati wa kutokea majanga kama yale ya meli ambayo yalitekeleza mamia ya abira.

Naibu Waziri huyo alisema kwa kuzingatia umuhimu wa kitambulisho katika kumtambua mtu yanapotokea majanga kama ajali na kusimamia ahadi zake Serikali kupitia kitengo cha Mrajisi wa Meli kabla ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Usafiri Baharini ilikutana na wamiliki wote wa meli zinazosafirisha abiria na kukubaliana kuanzisha utaratibu wa kuuza tiketi kwa kutumia vitambulisho.

Naibu Mwakilishi huyo alisema kwamba utaratibu huu ndio unaotumika kwa hivi sasa ili majina ya abiria yaende kuandikwa katika orodha ya abiria wanaosafiri katika chombo pamoja na idadi yao.

Hata hivyo alisema kwamba Serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa tangu kutangaza kupiga marufuku uuzwaji wa tiketi mitaani na hivi sasa Mamlaka ya Usafiri Baharini kwa kushirikiana na Makampuni ya Meli imeanza kuwasajili mawakala wa kuuza tiketi pamoja na kuwa na ofisi zenye kuridhisha, ingawa alisema kuwa bado kuwa watu wachache hawataki kufuata utaratibu.

Utalii haina takwimu sahihi
WIZARA ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo imesema kuwa inashindwa kupata takwimu sahihi katika sekta ya utalii kutokana na baadhi ya wawekezaji kukataa kutoa ushirikiano wakati maafisa wao wanapotaka takwimu za wafanyakazi katika taasisi zao.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Bihindu Hamad Khamis katika kikao cha baraza la wawakilishi wakati alipokuwa akijibu suali la mwakilishi wa jimbo la Muyuni (CCM) Jaku Hashim Ayoub katika kikao cha baraza hilo kilichoendelea jana Zanzibar.

Hata hivyo alisema kwamba Wizara ya Kazi, Uwezeshaji wananchi kiuchumi na Ushirika inalifanyia kazi tatizo hilo na ripoti itakapokamilika italetwa katika baraza hilo.

Kuhusu wawekezaji kuajiri wageni alisema kuwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa madai kuwa hakuna wazalendo wenye sifa na uzoefu katika nafasi ambazo wanaajiri.

“Sheria ya uwekezaji ianwapa uwezo wa kuajiri watendaji wa kigeni wa ngazi za juu na wataalamu pale ambapo hakuna wazalendo wenye sifa katika nafasi hizo”, alisema Bi Hamad.

Hata hivyo alisema kuwa wafanyakazi kutoka Tanzania Bara idadi yao ni kubwa ikifuatiwa na wazanzibari na wafanyakazi wachache kutoka nchi jirani na nje ya bara la Afrika.

Katika suali lake mwakilishi huyo alitaka kujua ni wazanzibari wangapi wameajiriwa katika sekta ya Utalii Zanzibar.
Diaspora sasa kupatiwa vitambulisho

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshauriwa kuweka utaratibu wa kisheria wa kuwapatia vitambulisho wazanzibari wanaoishi nje ya nchi ili kuendeleza uzalendo wao.

Utaratibu huo umetakiwa wende sambamba na kuweka kifungu cha sheria kitakachoweza kumpa uwezo Mkurugenzi wa Idara ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZanID) wazanzibari wote ambao hawapo nchini  (DIASPORA).
Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma  alitoa ushauri huo wakati akiwasilisha maoni na kamati hiyo  juu ya Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Mzanzibari Mkaazi ya 2005 na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo mbele ya wajumbe wa baraza hilo linaloendelea Chukwani Mjini Unguja.

Juma alisema kuwatambua wazanzibari waishio nje ikiwa watawawekewa utaratibu maalum nchi itafaidika hasa kwa vile kuna baadhi ya nchi ikiwemo Sirikali na nchi nyengine huchangia pato la taifa kwa kuwekea utaratibu maalum wa kutumia pesa kwa jamaa zao na Serikali kufaidika na kodi kupitia utaratibu huo.
“Kamati yangu inashauri Serikali pamoja kuwa mswaada huu unawalenga wale wakaazi waliopo ZNZ tu lakini ni vyema kikawekwa kifungu cha sheria kitakachoweza kumpa uwezo Mkurugenzi wa Idara ya vitambulisho kuandaa utaratibu maalum wa kuwapatia vitambulisho wale Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (DIASPORA) ili na wao wajihisi kuwa wanathaminiwa na Serikali yao ya Mapinduzi ya Zanzibar ili wazidishe mapenzi yao kwa nchi yetu na kuondoa zile fikra mbovu kwa nchi yao na Serikali yao na tunaamini itakuwa jambo hili ni chachu ya kusaidia maendeleo kwa nchi yetu. kwani tunawahitaji sana mchango wao wa hali na mali kwa maendeleo ya nchi yetu” Alisema Juma.
Mwakilishi huyo alisema kamati yake inaamini kwamba ombi hilo kwa Serikali litakuwa sio jambo gumu kutekelezwa kwani hivi sasa tayari Serikali imeshaanzisha idara maalum katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inachoshughulikia na kuratibu masuala ya Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (DIASPORA) na pamoja na upya wake lakini kimeanza kazi yake vizuri kwa kuwasiliana na wale Wazanzibari walioko nchi za nje ili kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.
Alisema ni lazima wazanzibari wanaoishi nchi za nje kuwapa utambulisho maalum ili kuwajuwa wapi walipo na shughuli zao na kuweza wasiliana nao kwa jambo lolote litakaloweza kuwawezesha wakatoa mchango wao wa mawazo, fikra, busara na hata msaada wa mambo mbali mbali katika serikali yao.
Alisema kuwa ni matumaini yake kuwa ombi hilo kwa Serikali halitakuwa jambo gumu kutekelezwa kutokana na kuwa hivi sasa tayari imeshaanzisha idara maalum katika Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi inachoshughulikia na kuratibu masuala ya Wazanzibari wanaoishi nchi za nje (DIASPORA), ambayo pamoja na upya wake lakini kimeanza kazi yake vizuri kwa kuwasiliana na wale Wazanzibari walioko nchi za nje ili kushiriki katika maendeleo ya nchi yao.
 “Lazima ndugu zetu hawa kuwapa utambulisho maalum ili kuwajuwa wapi walipo na shughuli zao na kuweza wasiliana nao kwa jambo lolote tunalohisi wanaweza wakatoa mchango wao wa mawazo,fikra,busara na hata msaada wa mambo mbali mbali, naamini Serikali yetu itaona umuhimu wa ndugu zetu hawa waishio nchi za nje.
Sambamba na hilo alisema kuwa sheria hiyo inalenga kuwapatia vitambulisho wakaazi wote waliopo Zanzibar wakiwemo wageni wote sio kutoka Baraza peke yake lakini hata kutoka nje ya nchi kama vile Italy,Marekani,Ufaransa,Uingereza,Kenya,Uganda,Ghana, hivyo sheria ina nia nzuri na kuwaomba kwa wale wenye fikra potofu au kupotoshwa kuachana na fikra hizo wajue kuwa lengo ni kuwatambua wote.

No comments: