ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, October 23, 2012
JINSI VYAKULA TULAVYO VINAVYOTUMALIZA-3
KATIKA makala zetu zilizopita tulieleza madhara ya kula baadhi ya vyakula vya kukaanga kama chipsi na kuku, mkate mweupe. Leo tutaelezea madhara ya mayai na soda lakini tunamalizia mada ya chipsi.
CHIPS
Chips ambayo kwa kawaida hutengenezwa kutokana na viazi mviringo na kukaangwa kwenye mafuta, ni chakula kinachotakiwa kuliwa kwa kiasi kidogo na kwa nadra sana, kwa sababu kiko kwenye kundi la vyakula vyenye mafuta mengi ambavyo huliwa kwa uchache sana. Lakini hali halisi ni kinyume chake.
KUKU
Kwa kawaida, kuku wengi wanaotumika kwenye biashara ni kuku wa kizungu. Nyama ya kuku hawa haina virutubisho sawa na kuku wa kienyeji. Hii inatokana na ukweli kwamba kuku wa kizungu hulishwa madawa mbalimbali ya kuwakinga na magonjwa na hulishwa vyakula vilivyochanganywa madawa ili wakue upesi.
Kwa mazingira hayo, nyama itokanayo na kuku wa aina hii haiwezi kuwa bora. Kiasili kuku huishi mazingira huru kwa kula vyakula ambavyo hujenga na kuukinga mwili wake dhidi ya magonjwa mbalimbali, kuku wa aina hii ndiye anayefaa kuliwa na kuleta faida ya nyama ya kuku inayokusudiwa.
MAYAI
Halikadhalika, mayai yanayopatikana kwa wingi mijini ni yale yatokanayo na kuku wa kufuga. Kiasili, mayai ya kuku wa kufuga, hayawezi kuwa sawa na mayai yatokanayo na kuku wa kienyeji. Huhitaji kuwa mwanasayansi kuona tofauti kati ya yai la kuku wa kienyeji na kuku wa kufuga, kwani mayai hayo yakipikwa huwa tofauti kwa ladha na hata rangi.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kuku wa kufugwa hulishwa vyakula vya kutengeneza ambavyo ndani yake huwekwa kemikali na madawa mbalimbali, wakati kuku wa kienyeji hula vyakula asili kwa kujitafutia wenyewe na mazingira wanayoishi ndiyo yanayowafanya wawe tofauti na bora. Hivyo ni dhahiri kwamba mayai tunayokula ya kuku wa kizungu yana madhara zaidi kuliko faida mwilini.
SODA
Moja ya vinywaji vinavyopendwa na kutumiwa na watu wengi ni pamoja na soda. Matangazo mengi ya biashara yanafanyika kutangaza kinywaji cha soda na kuonesha kuwa ni kinywaji ambacho hakina madhara kabisa kwa mtumiaji. Kwa matangazo hayo na kampeni hizo, familia nyingi zimeamini kuwa soda ni kinywaji bora na hata watoto wetu wamerithishwa imani hii.
Lakini kwa upande wa pili wa kinywaji hiki, siyo kinywaji salama kama ambavyo imekuwa ikielezwa. Siwezi kusema moja kwa moja kuwa mtu huruhusiwi kabisa kunywa soda kama vile ni sumu, lakini watu walitakiwa kuelimishwa na kuelezwa madhara ya kupenda kunywa soda na athari anazoweza kuzipata mtu kiafya. Naamini tahadhari inayotolewa kwa wanywa pombe, hata kwa wanywa soda ilipaswa kutolewa pia.
Utafiti unaonesha kuwa soda, pamoja na vikorombwezo vingine, huwekwa sukari nyingi kiasi kisichopungua vijiko sita katika chupa moja. Kiwango hicho cha sukari ni kingi zaidi ya mara tano ya kile kinachoruhusiwa kwa mtu kutumia kwa siku. Na madhara ya sukari mwilini ni mengi, yakiwemo ya kudhoofisha kinga ya mwili na viungo kwenye sehemu za maungio na pia huongeza uzito wa mwili.
Ukitaka kujua soda ina madhara kiafya, fanya utafiti binafsi na utagundua haya ninayoyaandika. Kunywa soda zisizopungua tatu kwa muda mfupi, kisha lala usiku kama kawaida halafu wakati wa kuamka asubuhi, usikilize mwili wako. Utaamka ukiwa na maumivu mwili mzima, utajihisi uchovu, hasa sehemu za maungio, mfano wa mtu aliyefanya mazoezi mazito au kazi nzito siku iliyopita. Hiyo ni kutokana na kuingiza kiwango kingi cha sukari mwilini.
Itaendelea Jumanne ijayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment