Habel Chidawali,Dodoma
KANISA Anglikana Tanzani limepanga kuwaburuza mahakamani, waumini wake ambao wamekuwa wakimpinga Askofu Mteule wa Kanisla hilo Dayosisi ya Lake Rukwa, Mathayo Kasagara, kama watashindwa kurudisha mali za kanisa hilo.
Aidha Anglikana imewaita waumini hao kuwa ni waasi kwa kuwa wanafanya kazi ambayo iko nje ya utaratibu wa Anglikana, huku likieleza kuendelea kumtambua Askofu Kasagara kuwa askofu halali wa jimbo hilo.
Tamko hilo lilitolewa juzi na Katibu Mkuu wa Anglikana Jimbo la Tanzania Mchungaji Dk Dickson Chilongani, wakati akitoa kauli ya maaskofu wa kanisa kwa waandishi wa habari mjini hapa.
Dk Chilongani aliwataka kundi linalopinga ushindi na kutokumtambua Askofu Kasagara kuachana na malumbano hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume na kanuni na katiba ya Anglikana Tanzania.
Kwa muda mrefu kumekuwapo na malumbano kati ya Askofu Kasagaaa na wafuasi wake, ambao wamekuwa wakipingana na kundi linaloonyesha kutomtambua linaloongozwa na John Mahinya.
Septemba 23 mwaka huu, Askofu Kasagara alizuiliwa kuongoza ibada katika Kanisla la Watakatifu wote la Sumbawanga baada ya vurugu hizo na kusababisha jeshi la polisi kuingilia kati.
Moja ya sababu wanazolalamikia waumini hao ni pamoja na kueleza kuwa askofu huyo wa kwanza katika Dayosisi ya Lake Rukwa alichaguliwa kwa njia ya rushwa, jambo lililopingwa na nyumba ya maaskofu.
Juzi Chilongani alisema kuwa nyumba ya maaskofu wa kanisa hilo ilifanya kikao chake mjini hapa na kupitia mambo kadhaa ambayo walijiridhisha kuwa kundi hilo halikuwa na mamlaka ya kuzuia ibada hiyo na wala kauli ya kutomtambua askofu kuwa ni batili.
“Kikao cha maaskofu kilichokutana Septemba 26 mwaka huu huko Mtumba, Dodoma kilitafakari kwa pamoja juu ya fujo zilizojitokeza katika kanisa la Watakatifu Wote huko Sumbawanga, na kubaini mambo mengi ambayo dhahiri yalionyesha kuwa Kasagara ni mtumishi na askofu halali wa kanisa hilo,’’alisisitiza Chilongani.
Kati ya sababu ambazo zimetolea na nyumba ya maaskofu ni kutokana na waumini hao kulifikisha suala hilo katika mahakama, kitendo wlichosema kuwa ni kinyume na utaratibu mzima wa kanisa hilo.
Sehemu ya tamko hilo ilisomeka “Hivyo basi masuala ya uchaguzi wa askofu hayawezi kupelekwa katika mahakama za kidunia, Anayefanya hivyo au anayekusudia kufanya hivyo, kama ni mkristo au mhudumu anavunja katiba ya kanisa Anglikana Tanzania.”
Katibu mkuu huyo aliwataka kundi hilo kukabidhi mara moja mali za kanisa, ambazo wamekuwa wakizishikilia kwa muda mrefu kwa kuwa si vema wao kuupinga uongozi ili hali wakabaki kukumbatia mali za kanisa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment