Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar) Ismail Jussa
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Leo asubuhi nimewasilisha kwa
Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba barua ya kuomba
kujiuzulu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kwa upande wa
Zanzibar ,
uamuzi ambao nimeomba uanze kutekelezwa rasmi tarehe 10 Oktoba, 2012.
Nimechukua uamuzi huu baada ya
kuzungumza na kushauriana na viongozi wangu wa juu wa Chama ambao ni
Mwenyekiti, Profesa Lipumba, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Machano Khamis Ali na
Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad takriban miezi miwili iliyopita.
Nawashukuru baada ya kunitaka niwape muda wa kulitafakari walinikubalia lakini
wakaniomba nibakie hadi tutakapokamilisha baadhi ya shughuli muhimu za Chama
katika kipindi hichi.
Sababu kubwa zilizonisukuma
kukiomba Chama kiniruhusu niachie nafasi hii ni kutokana na muda mrefu sasa
kuhisi kwamba majukumu niliyo nayo ya kuwa msimamizi mkuu wa utendaji wa Chama
kwa upande wa Zanzibar na wakati huo huo kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
wa jimbo la Mji Mkongwe hakunipi fursa ya kujifaragua na kutumikia nafasi zote
mbili kwa ufanisi unaotakiwa. Nataka kuona kazi ya kuibana Serikali ndani na
nje ya Baraza ili iwajibike zaidi kwa wananchi inaimarika zaidi.
Sambamba na sababu hiyo ni kwamba
nimekusudia kutumia muda mwingi zaidi kutoa mchango mkubwa zaidi katika
harakati za wananchi wa Zanzibar zinazoendelea za kuhakikisha kuwa Zanzibar
inarejesha mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa itakayofuatiwa na kuwepo
kwa Muungano wa Mkataba kati yake na Tanganyika yenye mamlaka kamili kitaifa na
kimataifa.
Harakati zinazoendelea Zanzibar
kwa njia za amani na za kidemokrasia kwa kutumia mchakato wa Katiba Mpya
zinahitaji kuungwa mkono na kupewa msukumo wa dhati na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi waliochaguliwa na wananchi wa Zanzibar kwenda kusimamia maslahi yao
na ya nchi yao. Nimetafakari na kuona kwamba nikiwa sina majukumu mengine ya
kiutendaji nitakuwa na muda kutosha wa kulifanya hili mimi na Wawakilishi
wenzangu tunaotoka CUF na CCM, vyama viwili vya siasa vilivyomo Barazani.
Nafurahi kwamba leo nimetimiza
azma yangu hiyo. Pamoja na uamuzi huu, naendelea kubaki kuwa Mjumbe wa Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa. Nawahakikishia
viongozi na wanachama wenzangu wa CUF kwamba tutaendelea kushirikiana pamoja
katika shughuli nyengine zote za kisiasa za Chama na kwa pamoja tutafanya kazi
kuyatimiza malengo tuliyojiwekea. Naahidi kumpa ushirikiano kikamilifu mwanachama
yeyote atakayeteuliwa kujaza nafasi ninayoiwacha.
HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
Zanzibar
05 Oktoba, 2012
No comments:
Post a Comment