ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 2, 2012

Kwenye mapenzi kuna virusi, unapaswa kujua ‘kuskani na kudiliti’-3

MAISHA yanakwenda mbio sana, kwa hiyo utapoteza muda wako bure kukaa umejiinamia kwa ajili ya mpenzi asiyekufaa. Usilie, bali mshukuru Mungu kwamba sasa umejifunza kitu kwa maisha yako yajayo. Tuliza akili halafu jipange kumpa furaha mwenzi wako ajaye. 
Ni maisha yako, ukifeli maana yake ni hasara yako mwenyewe. Utashindwa kufanya kazi zako vizuri kwa sababu ya kulilia mapenzi. Ni sawa una haki ya kuumia kwa sababu umetendwa lakini hiyo haiwezi kuwa dawa. Piga moyo konde halafu tazama mbele. Maisha yanakudai.

Siku zote unatakiwa kujua namna ya ‘kuskan na kudiliti’, virusi ni vingi na vipo katika sura nyingi kwenye mapenzi. Hakikisha unakuwa mwangalifu.
Aghalabu, huwezi kukitambua kirusi bila kufanya uchunguzi. Narudia kama ambavyo nimekuwa nikieleza mara kwa mara kuwa mapenzi hayachunguzwi kwa kumfuatafuata mpenzi wako. Tuliza akili, tega, macho na masikio halafu uandae moyo wako kwa matokeo yoyote.
Ukishamjua mwenzi wako kirusi, hapo utakuwa umeshamskani, utakapomuonesha njia ya kutoka, maana yake umefanikiwa kumdiliti. Tafadhali sana, usijiinamie peke yako mkono ukiwa shavuni. Unakipa faida kirusi. Je, unakubali adui yako ajue udhaifu wako?
Mpenzi anayekuja kwako kwa ajili ya kutimiza matakwa yake binafsi huyo ni kirusi. Maana yake, ulichonacho ndiyo kimemvuta. Siku hicho kitu kikiondoka, hawezi kuwa nawe tena. Ipo mifano mingi ya watu wanaolia leo hii, angalia nawe usije kuingia kwenye orodha.
Mathalan, amekupenda kwa sababu ya cheo chako. Siku hicho cheo kikiondoka hawezi kukupenda tena. Zaidi ni kwamba si kweli kuwa alikupenda, ila aliingia kwako kwa mtego wa fedha, kazi na kadhalika. Wewe siyo ATM wala daraja la ajira, usikubali kutumiwa.
Unatakiwa kuulinda moyo wako usitoneshwe, kwa hiyo fuatilia uhusika wa mwenzi wako katika matukio mbalimbali. Kama ni hasi, basi tazama mahali uliposimamia. Ikiwa wewe upo chanya, basi iwe ni sababu ya kumtambua kwamba ni kirusi, kwa hiyo mdiliti haraka.
KUNA AINA YA VIRUSI
Kwa kupitia tangu mwanzo wa makala haya, nimekuwa nikieleza virusi kwa jumla. Ni vizuri sasa kuvichambua kimoja baada ya kingine kwa lengo la kukuwezesha kukijua kirusi ndani ya uhusiano wako. Kirusi kinaweza kuwa wewe mwenyewe, mpenzi wako au watu wa pembeni.
KIRUSI NO. 1, MPENZI ADUI
Kuna falsafa inayoeleza kuwa rafiki wa rafiki yako ni rafiki yako. Rafiki wa adui yako ni adui yako. Adui wa adui yako ni rafiki yako. Hii iwe sababu ya wewe kuchunguza jinsi mpenzi wako alivyo kisha upate majibu ya kukusaidia mbele ya safari. 
Siku zote mpenzi anatakiwa awe adui wa adui yako, ikiwa ni rafiki wa adui yako, huna sababu ya kuendelea naye. Fikiria kwamba mtu fulani kwako ni adui na hapendi mafanikio yako kiasi kwamba amejionesha hivyo waziwazi. Inakuwaje mwenzi wako awe rafiki yake?
Hatua ya kwanza muonye. Siku zote napenda uamini katika kufundisha. Muelekeze mara kwa mara kuwa anachokifanya siyo sahihi kwa afya ya uhusiano wenu. Maelekezo yako ndivyo unavyoskani kirusi. Akishindwa kubadilika, basi mdiliti.
Naomba uelewe kuwa unapomdiliti unakuwa umejiokoa. Kuwa na mpenzi rafiki wa adui yako ni sawa na kuzungukwa na maadui wawili. Huwezi kujua faida anazopata kutoka kwa huyo adui yako, kama hakuna faida, basi angeachana naye. Tazama mbele kwa faida ya maisha yako.
Kirusi pia unaweza kuwa wewe pale unapokuwa rafiki wa adui wa mpenzi wako. Iweje kuwa rafiki na mtu ambaye hampendi mwenzi wako? Unapaswa kumlinda na kumtetea mwandani wako mahali popote na wakati wowote. Achana na huyo mtu ili kumfanya mpenzi wako awe na furaha.
KIRUSI NO. 2, RAFIKI MLETA MATESO
Una rafiki wa jinsia tofauti. Mwenzi wako ameambiwa kwamba wewe una uhusiano naye wa kimapenzi. Unachotakiwa kufanya ni kugundua kwamba huyo rafiki yako anamsababishia mateso mwandani wako. Jaribio la kwanza ni kuhakikisha unamtoa hofu mpenzi wako.
Ikitokea umejaribu kufanya hivyo lakini bado mpenzi wako hana imani na huyo rafiki, haraka sana mdiliti. Tambua kwamba amani ya mpenzi wako inajenga mara 100  usalama wako. Uking’ang’ania kotekote, utapata shida mno mbele ya safari.
Wakati mwingine hutokea mwenzi wako anakuwa na wivu wa kupitiliza. Hata ukimwambia vipi hataelewa uhusiano wako wa kirafiki na mtu wa jinsia tofauti. Basi cha kufanya ni kupima faida. Inawezekana pia mpenzi wako mwenye wivu ndiye kirusi.
Sasa basi, kwa maslahi ya maisha yako ya leo na kesho, unatakiwa kufanya uamuzi sahihi. Je, kuendelea kumuendekeza mpenzi wako mwenye wivu au  kuachana na rafiki anayemsababishia mateso mwandani wako? Ukichekecha na kupima vizuri, utajua nani wa kumdiliti.
Pengine huyo rafiki ni mshirika wako kikazi au kibiashara. Tangu umeanza kushirikiana naye, kuna unafuu mkubwa wa kimaisha na hatua kubwa umepiga. Hapo sasa jukumu ni lako, kusuka au kunyoa. Palipo na hasara, ujue ndiyo kwenye kirusi. Hebu diliti haraka.
KIRUSI NO. 3, WIVU
Kila mtu anatakiwa awe na wivu ili mambo yaende sawasawa. Itashangaza sana pale umeambiwa mpenzi wako anasaliti na umethibitisha halafu ukaendelea kuwa na tabasamu lilelile. Kukosa wivu maana yake una kasoro za kibinadamu. Inatakiwa uchunguzwe.
Hata hivyo, wivu ukizidi hasa ule wenye kuibua matatizo ni hatari mno. Kisa wivu ndiyo umfanye mwenzi wako ashindwe kutimiza majukumu yake ya kila siku? Hutaki awasiliane na watu, unaonesha wivu mpaka unaonekana kiherehere? Wewe ni kirusi, nashauri udilitiwe. 
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

nimeipenda sana huu ushauri niliopata na faida nyingi sana katika hii story ni poa sana na daima ubarikiwe luke and have bless day

mdau yule yule NY