ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 15, 2012

mswada wa usajili wa taasisi za biashara wapita...


Wajumbe wa baraza la wawakilishi wamepitisha mswada wa usajili wa taasisi za biashara ambao lengo lake kubwa ni kuziwezesha taasisi mbali mbali za biashara na makampuni kusajiliwa zanzibar na hivyo kuongeza pato la taifa.

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Abubakar Khamis Bakari alisema mswada huo umelenga kuliwezesha taifa kuingiza mapato na kuondowa urasimu wa usajili wa taasisi za biashara pamoja na vikwazo vyake.

“Mswada huu lengo lake kubwa kuweka mazingira mazuri ya kusajili taasisi za biashara nchini huku vikwazo na urasimu wa kusajili makampuni hayo ukiondolewa mara moja'alisema Abubakar.

Waziri huyo alisema kuja kwa mswada wa sheria ya kuanzishwa kwa wakala wa usajili wa Biashara na Mali Zanzibar na mambo yanayohusiana na hayo, kutaweza kupunguza usumbufu kwa waananchi wanaotaka kuanzisha makampuni hapa Zanzibar.

Alisema kukosekana kwa chombo hicho hivi sasa kumekuwa kukisababisha baadhi ya watu wanaotaka kufungua makampuni kulazimika kufanya hivyo Dar es Salaam na Zanzibar kuwa matawi ya kampuni hizo.

Wakichangia mswada huo wajumbe wa baraza la wawakilishi wamesema kwamba vikwazo na urasimu wa kusajili makampuni ya kibiashara kwa sasa umekuwa ukilikosesha taifa fedha nyingi za kigeni.

Akichangia mswada huo mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu alisema kwa muda mrefu  serikali ya mapinduzi ya zanzibar imekuwa ikipoteza fedha nyingi katika kusajili makampuni kutokana na urasimu uliokuwepo awali.

'Mswada huu unatakiwa kuondosha urasimu wa kusajili makampuni ya biashara kwa lengo la kutoa nafasi kwa taasisi mbali mbali kusajili biashara zao nchini...urasimu umekuwa ukitukosesha kusajili makampuni nchini na kukosa mapato'alisema Jussa.

Mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura (CCM), Hamza Hassan Juma alisema Zanzibar inayo nafasi kubwa kimataifa kusajili makampuni mbali mbali ya kibiashara na kuweza kutoa huduma kwa wageni na wananchi.

'Huu ni wakati muafaka kwa zanzibar kuweza kutoa huduma mbali mbali katika sekta ya biashara kwa makampuni kusajili biashara zao visiwani hapa na kuongeza mapato'alisema.

Alisema wakati umefika kwa serikali kuondosha vikwazo na urasimu kutoka kwa watendaji mbali mbali katika kusajili makampuni yatakayotoa huduma mbali mbali za kibiashara kwa wananchi.

No comments: