YACHUKUE mapenzi halafu itazame timu ya mpira wa miguu, kikapu na hata pete (netiboli) inavyocheza. Utaona kwamba ni lazima kupeana pasi mpaka mpira unapomfikia mfungaji. Hakuna mwenye uwezo wa kutoka na mpira golini kwake, akawapita wapinzani 10 na kufunga.
Mpira ni pasi, yaani kushirikiana kutafuta ushindi. Haitakiwi kutegeana. Jinsi unavyoona mpira unavyochezwa, ndivyo na uhusiano wa kimapenzi unavyojengwa. Wewe na mwenzi wako ni timu moja, sasa mnachezaje kutafuta ushindi?
Je, anapokuwa na mpira, nawe unajipanga vizuri ili akupe pasi halafu umrudishie afunge au kazi yako ni wewe kumtazama anavyokatiza na kumshangilia? Anapokabwa na maadui, unakwenda kumsaidia au yako yanabaki macho tu, yaani akidhibitiwa ubaki unasonya, akishinda mshangilie pamoja?
Akikupa mpira kwenye sehemu nzuri, unafunga goli au utangoja kumrudishia kwa sababu hutaki lawama baada ya kukosa goli? Mtu anayefanya hivi, huyo si mtu sahihi kwenye timu. Ni mtegeaji, kwa maana hiyo kama wewe unakuwa na sifa hii kwenye uhusiano, huhitajiki kabisa.
Uhusiano wa kimapenzi hujengwa na watu wawili wanaoamua kucheza kama mbio za vijiti. Mmoja anakimbia umbali wake halafu anamkabidhi mwenzake ili amalizie. Hupaswi kukimbia peke yako ili mwenzako abaki mtazamaji au mshangiliaji, vilevile hutakiwi kuwa mtegeaji. Nendeni pamoja.
Hata kama mwenzi wako ameonesha kuwa na kasi kubwa kwenye utafutaji na anafanikiwa, hebu hakikisha nawe unakuwa sehemu ya hayo mafanikio. Wanasema nyuma ya kila mwanaume aliyefanikiwa, yupo mwanamke jasiri na imara.
Kadhalika, nyuma ya mwanamke mwenye mafanikio, yupo mwanaume shupavu, muungwana, mwana demokrasia. Wanaume wa mifumo dume, mara nyingi huwa hawataki wanawake wao wapambane na kufanikiwa. Eti, badala ya kufurahia mafanikio ya mwenzi wake, huona wivu.
Nakubaliana na ukweli kwamba wanawake wengi waliofanikiwa, hugeuka mwiba wa kuumiza kwa wenzi wao. Hii inasababishwa na udhaifu wa kisaiokolojia ambao upo ndani ya vichwa vya wanawake kuwa wao hupaswa kuhudumiwa zaidi.
Nakubali kuwa kuna wanaume wavivu, eti nao hutaka kuhudumiwa na wapenzi wao. Muda wote wanashinda wamelala halafu ikifika usiku, wanataka wabadili viwanja vya starehe wakajirushe. Naunga mkono watu wa aina hiyo kuadhibiwa. Wavivu hawatakiwi.
Hata hivyo, sijawahi kuona mwanaume anamuacha mke kwa madai kwamba hachangii chochote kwenye pato la familia. Hii inatokana na ukweli kwamba imeshajengeka hivyo na ni ngumu kutengua kuwa mwanaume ndiye mtoa huduma, hata kama mke atakuwa anashinda nyumbani na kubadili saluni kwa kujipamba.
Wapo ambao hawataki wapenzi wao watoke kwenda kutafuta. Anataka akatafute peke yake halafu arudishe nyumbani akatumie na mama watoto wake. Ukweli ni kuwa aina hii ya watu, ni wale wanaosumbuliwa na wivu wa kupindukia. Anaogopa mpenzi wake akifanya kazi, ataibiwa.
Hata wanawake, wengine hawataki kuwa mbali sana na wenzi wao. Anachotaka ni muda mzuri wa kupumzika na mpenzi wake japo kipato kitakuwa kidogo. Anamaanisha wakiingiza kidogo tu kinatosha. Mwenzi wake akiwa mbali ni mgogoro. Atauliza: “Kazi sawa lakini na mimi nikae na nani muda huu?”
Siku zote nasimamia mapenzi na maisha. Inatakiwa wanaopendana wawe mstari wa mbele kupigania maendeleo yao. Hivyo basi, sikubaliani na mtindo wa kujifungia muda mwingi, badala ya kushirikiana katika kuongeza kipato. Inawezekana leo kinawatosha kwa sababu mpo wawili, mtoto akija je?
Ni lazima watu wafanye kazi kwa bidii.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment