ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 2, 2012

Zitto, Lissu wang’aka Karatu


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto na mwenzake wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), wamewaonya viongozi na madiwani wa chama hicho wilayani Karatu kuwa hawatavumiliwa endapo watashindwa kutatua tatizo la maji wilayani humo.
Vigogo hao walitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wakiwahutubia wakazi wa mji wa Karatu wakiwa wameongozana na Mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Israel Natse, katika mkutano wa kuhamasisha maendeleo pamoja na ushiriki wa wananchi katika utoaji wa maoni ya Katiba mpya.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, alisema akiwa kama kiongozi wa chama pamoja na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Lissu, wametoa maagizo kwa viongozi wao wa wilaya chini ya Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Lazaro Maasai, kwenda kuzungumza na wananchi kwenye vijiji ambavyo mradi wa maji wa Kaviwasu unapita.
Alifafanua kuwa lengo la kwenda kuzungumza na wananchi hao ni kujua matatizo yaliyopo ambayo yanasababisha mradi huo kutotoa huduma kwa kiwango kilichokusudiwa na kuyapatia ufumbuzi mara moja ili watu waendelee kupata maji safi na ya kutosha.
“Naomba niwambie wazi kama hawatatekeleza maagizo haya tutawafukuza wote kwa kuwa hatutakubali kuona mradi huo wa maji ulioasisiwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, wakati akiwa mbunge wa jimbo hili unaharibiwa na watu wachache wenye tamaa ya fedha,’’ alisema.
Aliongeza kuwa wametembelea maeneo hayo na kukutana na malalamiko mengi juu ya viongozi kushindwa kusimamia vema majukumu yao na kuwataka wananchi wawaambie viongozi hao kuwa katika miradi ya maendeleo hakuna siasa na ikibidi wawawajibishe kama watashindwa kutekeleza majukumu yao.
Akizungumzia kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi unaofanywa na baadhi ya watendaji wa serikali, Zitto alisema tayari wana orodha ya Watanzania 27 ambao wanamiliki mamilioni ya dola nje ya nchi ambayo waliyapata kwa njia zinazotia shaka.
Zitto alitaja kuwa miongoni watuhumiwa hao yumo ofisa mmoja wa jeshi mstaafu ambaye hata hivyo hakumtaja jina, akisema anamiliki akaunti nje ya nchi ikiwa na kiasi cha dola milioni 56.
Aliitaka serikali iwataje wote wanaomiliki fedha nje na kuchukua hatua haraka, vinginevyo wao watawaweka hadharani kwa umma ili nguvu ya wananchi ichukue mkondo.
Naye Lissu akizungumza katika mkutano huo, aliwaonya wananchi wa Karatu wasikubali kuanza kurubuniwa kwa kuchukua visenti vidogo vidogo na kuharibu historia yao nzuri ya mfano kwa nchi hii.
Alisema vitendo vya kuendekeza njaa katika masuala ya utendaji si desturi na mfumo wa chama hicho, hivyo kuwatahadharisha wananchi kuwa kama kunatokea kiongozi ama mwanachama ana matatizo hayo basi hakuna kufichaficha waelezane hadharani.
Kuhusu utoaji maoni kwenye tume ya Katiba, Lissu aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kama wanavyojitokeza kwenye mikutano ya chama hicho ili kutoa maoni yao.
“Naomba niwaambie wananchi nyie mna historia kubwa toka nchi inapata uhuru mliishawahi kuchagua kiongozi bila kupitia chama chochote, Chifu Sarwatt na mkambwaga mgombea wa TANU lakini leo miaka 50 ya uhuru tunaambiwa bado hatujakomaa kuwa na wagombea binafsi, kwa kutumia uandikwaji wa Katiba mpya jitokezeni mtoe maoni yenu,” alisema Lisu.
Alifafanua kuwa wasipojitokeza kutoa maoni kwa tume hiyo watakuwa wamechangia kuruhusu watu wachache kuwaandikia Katiba ama vipengele vingi vya Katiba ya zamani inayolalamikiwa vitabaki vilevile.

Tanzania Daima

No comments: