ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 6, 2012

JINSI VYAKULA TULAVYO VINAVYOTUMALIZA - 5

TUNAENDELEA kuwaletea mfululizo wa mada ihusuyo jinsi vyakula tunavyokula vinavyotumaliza, leo tuanze na mada ya nyama choma.

NYAMA CHOMA
Miongoni mwa vyakula vinavyopendwa na kuliwa na watu wengi ni pamoja na nyama za kubanika maarufu kama ‘nyama choma’ zitokanazo na wanyama (Red Meat). Kiuasili wake, nyama ni chakula muhimu kwa mwili wa binadamu kutokana na kuwa ndiyo chanzo kikuu cha protini. Na kwa kawaida, nyama choma huwa bora zaidi kuliko nyama za kukaanga au kuunga kwa mafuta.
Hata hivyo, ukiukwaji wa kanuni za mpangilio wa ulaji vyakula umeifanya nyama kuwa hatari kwa afya za watu wengi. Katika kundi la vyakula, nyama hasa nyekundu, imewekwa katika kundi la vyakula vinavyotakiwa kuliwa kwa kiasi kidogo kwa lengo la kuupatia mwili protini.
Lakini katika hali halisi, hali haiko hivyo. Watu wanapenda sana kula nyama kupita kiasi na kwa kiwango ambacho kiingiapo mwilini hugeuka kuwa sumu inayokimbilia kwenye ‘joints’ za miguu na kuwafanya walaji kupatwa na matatizo ya kuumwa miguu. Pia ulaji wa nyama kupita kiasi, huchangia ukosefu wa choo kwa muda mrefu kwa mlaji.
Ieleweke kwamba ulaji wa nyama siyo jambo la kuonyeshea ufahari au kujivunia, mtu anayekula mboga za majani au dagaa ni bora zaidi kuliko yule anayekula nyama kila siku. Hivyo kwa kujali afya zetu, tunashauriwa kula nyama kwa nadra na kwa kiasi kidogo.Badala yake tupende zaidi kula mboga za majani, au samaki, kuku na dagaa.
Aidha, hata ulapo nyama choma au ya kukaanga au kupika, ikiwa ni jamii ya nyama nyekundi, ni lazima ujue jinsi ya ‘kubalansi’ mwilini. Itafaa zaidi ulapo nyama ukala pamoja na mboga za kutosha, zikiwemo nyanya, vitunguu na kisha kunywa maji mengi. Hii itakusaidia kuondoa sumu iliyopo kwenye nyama kwa urahisi zaidi pindi iingiapo mwilini.
Lakini kwa bahati mbaya sana, watu wengi hupenda kula nyama choma au mishikaki ya nyama nyekundu kisha kushushia na bia. Kwa mtindo huu wa maisha, watu hawa hutia mwilini vitu hatari ambavyo huleta madhara ya kiafya makubwa baadaye na hata tatizo lolote la kiafya likitokea, si rahisi kujua limetokana na staili hii ya maisha. Tunatakiwa kujiepusha na mtindo huu wa maisha.

MKATE
Wote tunakula mkate na tunapenda, kutokana na ukweli kwamba ndiyo chakula kikuu cha asubuhi kwa familia nyingi za mijini. Mkate unaopendwa na walaji wengi ni mkate mweupe ambao hutengenezwa kutokana na ngano iliyokobolewa, kusafishwa na kutiwa vikorombwezo vingine ikiwemo sukari. Kwa ladha ni mitamu na limekuwa ndiyo chaguo la wengi.
Lakini kiafya chakula hiki ni miongoni mwa vyakula vinavyochangia matatizo mengi ya kiafya. Kinachofanya chakula hiki kuwa hatari ni kwa sababu kinatengenezwa kutokana na ngano iliyokobolewa na kuondolewa virutubisho vyake muhimu vya asili na kuongezewa vitu vingine vya kuongeza ladha ambavyo siyo salama kiafya.
Mkate mweupe unapoliwa kwa wingi kila siku huchangia matatizo ya ukosefu wa choo kwa mlaji na huchangia matatizo ya ugonjwa wa kisukari. Inaelezwa kuwa vyakula vyote vinavyotengenezwa kutokana na nafaka iliyokobolewa, ukiwemo ugali wa sembe nyeupe, viingiapo mwilini hugeuka na kuwa sukari, hivyo ulaji wa vyakula vya aina hii kwa wingi ni sawa na mtu anayekula sukari kwa wingi.
Itaendelea wiki ijayo. (GPL)

2 comments:

Anonymous said...

Huo weusi unaotokana na kuungua unachagia sana kansa ya utumbo mmpana (colon cancer). Tujitahidi kula nyama isiyo nyekundu, kama vile kuku na samaki. Pia tule matunda baada ya chakula na tule steamed brocoli. Inazuia sana kansa. Pia matunda yanafanya uchafu usikae kwenye utumbo mpana. tunywe maji kila siku.

Anonymous said...

Tuache magari. Tufanye mazoezi ya kutembea japo mara tatu kwa wiki. Ukiangalia TV wakati wa matangazo utaona matangazo ya vyakula, magari na madawa. Yaani ukishakula kaendeshe gari ili uugue ukatibiwe. Hizo biashara zinahusiana.