ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 14, 2012

MAALUM KWA WANAWAKE WANAOHITAJI KUOLEWA! - 2

ACHA kulalamika kila siku, kwa nini huolewi, jiangalie na ujiulize: “Hivi ni kwa nini siolewi?” kwa kupata jibu la swali hili, itakuwa rahisi kwako kuelekea kwenye ndoa.

Kuna wengine wanachanganyikiwa kabisa, kila wanaume wanaokuwa nao, wanawaacha baada ya muda mfupi. Wapo wanaokwenda mbali zaidi na kuhisi labda wamelogwa, hapana rafiki! Hujalogwa.
Inawezekana kuna mahali unakosea bila kujua. Katika mada hii tunajifunza mambo ya muhimu kuzingatiwa kama ni kweli unahitaji kuingia kwenye ndoa yako. Leo namalizia sehemu ya mwisho. Karibu darasani tuendelee kujifunza.

STAHA
Wanaume wanapenda kuheshimiwa, naomba nieleweke wazi hapa, nazungumzia juu ya heshima na si kuogopa! Kumuogopa mtu na kumheshimu ni vitu viwili tofauti, kwahiyo ni vyema ukawa na heshima kwa mpenzi wako. Ninaposema staha, ninakuwa na maana pana zaidi.
Hapa nazungumzia juu ya kutambua thamani yake, kumpa nafasi ya kwanza katika mapenzi na kumnyenyekea kama mumeo mtarajiwa. Ni nani anapenda kuwa na mwanamke wa mabishano, majibizano?
Utakapokuwa na staha, msikivu na unayekubali kuelekezwa, tiketi yako ya kuolewa unakuwa nayo mkononi kabisa. Anza na hatua hii na kwa hakika utakuwa katika ile cheni ya kuelekea katika ndoa, ambayo bila shaka ndiyo inayokuumiza kichwa.

JITOE KWA AJILI YAKE
Zipo sifa ambazo ni za lazima mwanamke kuwa nazo ili kumshawishi mchumba wako afunge ndoa na wewe, lakini ukiwa na sifa za ziada inakuwa bora zaidi, maana unakuwa na asilimia kubwa zaidi ya zile zilizotegemewa.
Sifa ya kujitoa ni kubwa sana, mathalani ana matatizo ya kifamilia, kikazi au binafsi. Kuwa wa kwanza kuyajua na kumsaidia.
Haina maana msaada wako lazima uwe pesa pekee bali hata ushauri wako tu, unaweza kuwa dawa ya kinachomsumbua na hapo ukazidi kuwa na sifa ya kuwa naye kama mkewe. Hilo linawezekana kabisa, lipo mikononi mwako.

ULIZIA NDOA
Ukimya wako wakati mwingine unaweza kumfanya jamaa aone upo naye kwenye uhusiano wa kupoteza muda, halafu baada ya muda kila mtu ‘ajipotezee’ kivyake. Ili kuondoa dhana hiyo, ni vyema nawe ukawa unaanzisha mjadala juu ya kuoana.
Usiwe mshawishi usiye na hoja, angalia mazingira kwanza na ni vyema kama utaandaa mazingira sahihi kwa wewe kuzungumza na mwenzi wako juu ya suala nyeti kama hilo, siyo kukurupuka hata katika muda ambao unamuona hayupo katika hali ya kawaida.
Tafuta mazingira tulivu, naye awe katika hali nzuri kifikra, kisha muulize: “Baby vipi kuhusu ndoa? Tumekuwa katika uchumba kwa muda mrefu sasa, unajua natamani sana kuwa mama, lakini siwezi kufanya hivyo nikiwa nje ya ndoa, ndiyo maana nimeona nikukumbushe. Unaonaje dear?”
Kauli hiyo laini itatosha kumfanya aone kwanza haupo naye kwa muda mfupi, lakini pia unajitambua. Wanaume wengi wanapenda kuwaoa wanawake wanaojitambua.

JIACHIE..
Hupaswi kumuogopa sana mpenzi wako, mheshimu lakini usimuogope. Ukifanya hivyo utaweza kupata mwanya wa kuonesha utundu wako hata mnapokuwa faragha.
Kuwa mbunifu kwa kiwango cha mwisho. Utundu huo hauishii hapo, jenga tabia ya kumtumia meseji za kumfurahisha, mtakie mchana mwema, kazi njema, usiku mwema nk.
Kuwa karibu na mwenzi wako kwa njia ya mawasiliano kutamsogeza jirani na wewe na mara nyingi atakuwaza.

ACHANA NA MANENO YA WATU
Hili liwe la kwanza kabisa katika fikra zako, achana na maneno ya waswahili, hata kama unahisi jamaa anatoka na msichana mwingine mtaa wa pili na mashoga zako wamekuhakikishia hilo, usilipe nafasi moja kwa moja. Fanya uchunguzi kwanza.
Siku zote maamuzi ya kukurupuka huwa yana majuto baadaye. Fuatilia kwanza kabla ya kukubali kukatishwa tamaa. Lakini pia wapo marafiki zetu wengine, kazi yao kubwa ni kukatisha wenzao tamaa, pima maneno ya watu kabla ya kuchukua uamuzi.
Ni kweli hupaswi kuwapuuza wote, lakini wapo wasio wema. Pima maneno yao halafu yafanyie kazi. Wenyewe wanasema; akili za kuambiwa, changanya na zako!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

1 comment:

Anonymous said...

hiyo ni kweli kwa akina dada,na kwa wanaume je?kwani uhusiano si ni two way communications?