
Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa kwenye soka ya Tanzania pamoja na kuchangia kupinduliwa kwa uongozi wa Yanga uliokuwa chini ya Mwenyekiti Llyod Nchunga.
Pia, wachezaji wa Yanga, Stephano Mwasika na Jerryson Tetege walifungiwa huku Nadir Haroub, Haruna Niyonzima, Omega Seme na Nurdin Bakari wenyewe wakipewa adhabu pamoja na kutozwa faini ya Sh500,000 kila mmoja.
Hata hivyo, ukiacha suala hilo la vurugu, jambo ambalo mashabiki wa Yanga hawataisamehe Azam ni kitendo cha kuinyima timu hiyo nafasi ya kucheza michezo ya Afrika mwakani.
Yanga ambayo tangu ipate kipigo kutoka kwa Azam mwezi Machi tayari imebadilisha makocha mara tatu, Kostadin Papic, Felix Minziro, Tom Saintfiet na sasa yupo Ernest Brandts yote katika kuhakikisha msimu huu wanachukua ubingwa wa Ligi Kuu.
Azam pamoja na mafanikio yao ya kupata nafasi ya kucheza kwa mara ya kwanza mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, walimtimua kocha Stewart Hall na kumpa jukumu hilo Mserbia Boris Bunjak, lakini wiki iliyopita walimfukuza kocha Bunjak na kumrejesha kocha Hall.
Mwingereza Hall amerejea Azam kwa kishindo kwani tangu amerudi tayari ameiongoza timu yake kuichapa Coastal Union mabao 4-1 na kuipandisha mpaka nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu.
Lakini kocha Hall anajua kabisa mchezo wa leo ni mgumu kwani Yanga itaingia uwanjani ikiwa na rekodi ya kushinda mechi nne mfululizo na wakati huohuo ikitambua fika kuwa ushindi wa leo utaiweka kileleni rasmi.
Tayari kocha wa Yanga, Brandts amesema wachezaji wake hawana wasiwasi na wamejiandaa vizuri kwa mchezo leo.
"Timu yangu imekuwa ikibadilika kila siku na wachezaji wote wameonyesha moyo wa kujituma na lengo lao ni kutwaa ubingwa," alisema Brandts.
Naye kiungo wa Yanga, Athumani Iddi ëChujií alisema Azam ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri, hususan katika nafasi ya kiungo, hivyo wanatarajia upinzani mkali.
ìAzam wazuri, wana viungo vizuri na mbaya zaidi wanapokuwa wanacheza na sisi wanatukamia sana, mchezo utakuwa mgumu kwetu na kwao pia,'' alisema Chuji.
Endapo Yanga yenye pointi 23 itapoteza mchezo wa leo itatoa nafasi kwa Azam (21) kupanda kupanda kileleni kama Simba (23) itaendeleza rekodi yake ya kutoka sare dhidi ya Mtibwa Sugar leo.
Imedaiwa matokeo yasiyoridhisha ya Simba kwa sasa yanatokana na mgomo baridi miongoni mwa wachezaji, pia baadhi ya viongozi walikuwa wametengwa.
Imedaiwa kuwa wachezaji wa Simba wamekuwa wakisotea posho zao na wale chipukizi waliopandishwa kuichezea timu kubwa maisha yao yamekuwa magumu kabisa kutokana na kutopewa stahiki zao ipasavyo.
Hata hivyo Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alikanusha madai hayo akisema,"Hakuna kitu kama hicho na wachezaji wa Simba ndiyo wanaolipwa vizuri Tanzania."
"Kilichopo hivi sasa ni kwamba kuna watu wanaeneza fitina na chuki binafsi, lakini mimi nakwambia kama ni fedha basi hakuna mchezaji hata mmoja anadai, hayo mambo mengine ni siasa tu za mpira na kutafutiana sababu,"alisema Kamwaga.
Naye kocha wa Simba, Milovan Cirkovic akilizungumzia pambano lao la leo dhidi ya Mtibwa alisema wamejipanga vizuri kwa pambano hilo.
"Nimewataka wachezaji wasahau matokeo yaliyopita tujipange upya, tunahitaji kushinda leo ili tuendelee kuongoza ligi, kinyume chake hatutaongoza ligi,"alisema Cirkovic.
Hata hivyo, Simba leo inapewa nafasi kubwa ya kupata ushindi kutokana na udhaifu wa Mtibwa Sugar msimu huu.
Mtibwa inayofundishwa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Mexime imeshinda michezo mitatu tu hadi sasa na wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wakiwa na pointi 13.
Mafanikio makubwa ya Mtibwa msimu huu ni ushindi wao wa mabao 3-0 dhidi ya Yanga, lakini baada ya hapo walipoteza mwelekeo kabisa na huenda isimalize kwenye nne bora kama ilivyozoeleka.
Mchezo mwingine wa Ligo Kuu leo utafanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba wakati wenyeji Kagera Sugar watakapo wakaribisha Prisons ya Mbeya.
Imeandaliwa na Jessca Nangawe, Clara Alphonce na Vicky Kimaro wa Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment