Maelfu ya waombolezaji jana walijitokeza kushiriki mazishi ya msanii Hussein Ramadhan maarufu kwa jina la Sharo Milionea, huku mamia wakizirai baada ya kushindwa kujizuia wakati mwili wake unawekwa kaburini
MAELFU ya waombolezaji jana walijitokeza kushiriki mazishi ya msanii Hussein Ramadhan maarufu kwa jina la Sharo Milionea, huku mamia wakizirai baada ya kushindwa kujizuia wakati mwili wake unawekwa kaburini.
Mwili wa msanii huyo ulizikwa jana kijijini kwake Lusanga wilayani Muheza saa 7 mchana, katika tukio lililomshirikisha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Waombolezaji walianza kumiminika kijijini Lusanga tangu juzi jioni na idadi yao iliongezeka zaidi jana asubuhi. Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi.Sala ya mazishi iliongozwa na Sheikh Twaha Juma ambaye baadaye aliamuru jeneza hilo kupelekwa makaburini, ambako waombolezaji kadhaa walipoteza fahamu.
20 wapelekwa hospitali
Miongoni mwa matukio yaliyojitokeza katika msiba huo ni baadhi ya waombolezaji kupoteza fahamu msibani.Matukio tofauti ya watu kuzirai yalitokea wakati mwili wa msanii huyo ulipokuwa unapelekwa nyumbani kwao kijijini Lusanga ukitokea Hospitali Teule ya Wilaya ambako ulihifadhiwa tangu alipopata ajali Jumatatu usiku na wakati wa mazishi.
Miongoni mwa waliopoteza fahamu katika msiba huo ni wasanii na waigizaji wa filamu waliokuwa wakiigiza na Sharo Milionea wakati akiwa katika kundi la AL Riyam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na MC wa shughuli hiyo, Steve Nyerere, zaidi ya watu 20 walipoteza fahamu katika msiba huo na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Muheza.
DC Mgalu aliwaomba waombolezaji kutokuwa na shaka juu ya waliopoteza fahamu kwa kuwa madaktari maalumu walikuwa wameandaliwa hospitalini hapo kwa ajili ya kuwapa huduma.
Mwananchi lilifika katika hospitali Teule na kukuta waliokuwa wamepoteza fahamu, wengi wao wakiwa ni wasichana, wakipata huduma huku wengine wakiomba kupewa ruhusa ili wakahudhurie maziko.
JK atuma rambirambi
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara kutokana na vifo vya wasanii watatu vilivyotokea hivi karibuni, kikiwamo cha Sharo Milionea.
Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, ilisema kuwa Rais Kikwete ameshtushwa na vifo hivyo vya ghafla.
Wasanii hao ambao walifariki dunia katika mazingira tofauti ni Mwigizaji wa Kundi la Kaole, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ aliyefariki dunia hivi karibuni kutokana na maradhi yaliyokuwa yanamsumbua kwa muda mrefu.
Msanii mwingine ni mwigizaji wa filamu, John Maganga aliyefariki Novemba 24, 2012 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
“Nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno kutokana na taarifa za vifo vya wasanii hawa ambao kwa hakika mchango wao mkubwa katika tasnia ya muziki na maigizo hapa nchini ulikuwa unatambuliwa na kuthaminiwa na wananchi wengi,” ilisema taarifa hiyo ya Ikulu.
Vile vile, mke wa Rais Kikwete, Mama Salma alituma salamu za rambirambi zilizosomwa na DC Mgalu, kuwa ameguswa na msiba huo na kuwataka ndugu wa marehemu na wasanii wengine kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu.
Kwa mujibu wa Mgalu, Mama Salma alituma salamu hizo akiwa Mwenyekiti wa Mfuko wa Wanawake na Maendeleo (WAMA).
“Mke wa Rais kama mnavyojua ni mama wa Watanzania wote na ni mama wa wasanii, hivyo msiba huu wa Sharo Milionea umemgusa sana na ameitaka familia ya marehemu kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha majonzi,” alisema Mgalu.
Wenye sare za CCM
wazomewa
Katika msiba huo watu waliokuwa wamevalia sare za CCM walijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na waombolezaji ambao walisema hakukuwa na haja ya kujitambulisha kiitikadi katika msiba huo.
Kundi la vijana waliokuwa kando ya barabara ielekeayo kitongoji cha Jibandeni, nyumbani kwa mama mzazi wa marehemu, waliwazomea watu hao huku wakisema kuwa huo haukuwa msiba wa CCM bali ni wa wasanii wa filamu.
Vijana hao walieleza kushangazwa kwao na kitendo cha makada hao kuvaa sare katika msiba huo wakati kiongozi wao ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwasili msibani hapo akiwa amevaa nguo za kawaida.
“Ondokeni hapa, mnajipendekeza kwa wasanii, mnatuvalia maguo ya magamba hapa mmesikia hapa kuna mafisadi? Nendeni huko mbona bosi wenu Nape hakuvaa nguo hizo?” walisikika wakisema baadhi ya waombolezaji waliokuwapo msibani hapo.
Kitendo hicho kilisababisha baadhi ya askari polisi kuwafuata vijana waliokuwa wakizomea na kuwataka kuacha kufanya hivyo, la sivyo wangechukuliwa kuwa wamekwenda kufanya vurugu na kuharibu shughuli za msiba.
Wakizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina baadhi ya waliozomewa walisema wameamua kuvaa sare hizo baada ya kupewa taarifa kuwa Nape angekuwapo.
Walaani waliomwibia marehemu
Siku moja baada ya Sharo Milionea kufariki katika ajali, kubiwa vitu alivyokuwa navyo huku mwili wake ukivuliwa nguo, wananchi mbalimbali wamelaani kitendo hicho na kukiita kuwa ni cha kinyama.
Kitendo hicho kilisababisha baadhi ya askari polisi kuwafuata vijana waliokuwa wakizomea na kuwataka kuacha kufanya hivyo, la sivyo wangechukuliwa kuwa wamekwenda kufanya vurugu na kuharibu shughuli za msiba.
Wakizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina baadhi ya waliozomewa walisema wameamua kuvaa sare hizo baada ya kupewa taarifa kuwa Nape angekuwapo.
Walaani waliomwibia marehemu
Siku moja baada ya Sharo Milionea kufariki katika ajali, kubiwa vitu alivyokuwa navyo huku mwili wake ukivuliwa nguo, wananchi mbalimbali wamelaani kitendo hicho na kukiita kuwa ni cha kinyama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wananchi hao walisema kuwa ubinadamu umetoweka kwa watu na kukumbwa na roho za kinyama, hivyo kuitaka jamii na Serikali kuhakikisha wahusika wanakamatwa.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba alisema, “Sidhani kama wanaotenda kosa hilo ni binadamu waliokamilika, watu utu umewatoka sana siku hizi, ebu wamrudie Mungu wawe na utu, wawe na roho za huruma.
“Kuiba kama kuiba ni vibaya na mwizi akikamatwa adhabu yake ni kifungo, mbaya zaidi anamwibia mwathirika wa ajali kama ilivyotokea kwa kijana wetu msanii aliyeanza kuwa na mafanikio, kitendo walichofanya ni cha kinyama sana.
“Haiwezekani mwenzio amekutwa na tatizo badala ya kusaidia unamwibia mpaka nguo aliyoivaa jamani, hiyo ni mbaya sana kwa kweli. Wahusika wakijulikana wachukuliwe hatua kali za kisheria sababu ni sawa na uuaji,” alisema.
Naye kada maarufu wa CCM ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela akizungumzia suala hilo alisema, “Suala la watu kuwaibia waathirika wa ajali, kwanza tulitambue kuwa ni unyama na ukatili wa hali ya juu.
“Serikali inabidi kutoa elimu na kukemea kwa nguvu zote vitendo vya namna hiyo, vitendo kama hivi vichukuliwe sawa na uharamia, hivyo watu hawa wakikamatwa sheria za uharamia zichukue mkondo wake ili kuwa fundisho kwa wengine.
“Tukikaa kimya watu kama hawa wanaweza kwenda mbali zaidi hata kuwaua majeruhi ili waweze kuchukua vitu vyao.
Naye mchezaji wa Mtibwa Sugar, Hamis Mroki alisema “Binadamu hatufanani, aliyefanya kaona sawa na kusahau kuna Mungu, binafsi nilijisikia vibaya yaani badala ya kumsaidi wanaanza kumwibia mpaka nguo aliyovaa mwilini, ni unyama gani huo, tunaenda wapi hata kama hali ya maisha ni ngumu tusifike huko.”
DC aahidi msako nyumba kwa nyumba
Akizungumzia suala hilo, DC Mgalu alieleza kusikitishwa kwake na wezi hao kwa kitendo chao cha kinyama.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona wakazi wa Muheza wamemtendea vitendo vya kinyama ndugu yao ambaye naye ni mkazi wa wilaya hiyo badala ya kumsitiri.
Aliwataka waliopora vitu vya marehemu kuvirejesha kabla ya jana jioni, na kwamba ifikapo leo atatuma kikosi maalumu cha askari kwenda kufanya msako wa nyumba hadi nyumba.
“Nawapa nafasi hadi leo jioni wale waliopora fedha na vitu vyote vya marehemu wavirejeshe haraka leo jioni vionekane, la sivyo kesho nitatuma kikosi maalumu kitakachofanya ‘ambushi’ kuvisaka,” alisema Mgalu.
Taarifa hiyo ya mkuu wa wilaya ilishangiliwa na waombolezaji waliohudhutria msiba huo ambao walisikika wakisema kuwa ni vizuri kufanya msako huo ili liwe fundisho kwa wengine.
Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya aliwashukuru wakazi wa Kijiji hicho cha Songa Kibaoni waliomsitiri msanii huyo baadaye hadi mwili wake kuupeleka hospitalini.
“Namshukuru sana Mwenyekiti wa Kitongoji cha Songa Kibaoni kwa kuusitiri mwili wa msanii huyu, napenda kusema mlilolifanya mtalipwa na Mungu,” alisema Mgalu.
Sharo Milionea ni miongoni mwa wasanii maarufu waliofariki na kuzua taharuki na huzuni kubwa miongoni mwa jamii na kufanya nchi kuzizima kutokana na umaarufu ambao wamejizolea.
Kauli ya mwisho ya Sharo
Kifo cha msanii hiyo kilitokea saa chache baada ya kuwasiliana na rafiki yake maarufu kwa jina la Kitale katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), Mwananchi imeelezwa.
Kitale aliliambia gazeti hili juzi kuwa walichozungumza katika mawasiliano hayo ya mwisho ni kuhusu mpango wa kuingia mkataba na kampuni moja ambayo wangeifanyia shoo ndani na nje ya nchi.
Kitale alisema walikubaliana kukutana mapema katika msiba wa mwigizaji mwingine aliyefariki siku mbili kabla ya mauti yake kwa maongezi zaidi.
“Kuna dili ambalo nilimdokeza Sharo, nikamwambia kuna mtu anataka tufanye naye shoo 12, yaani shoo tatu zitakuwa za nje ya nchi na shoo zingine zote tutafanyia hapa nchini, nilivyomwambia basi alifurahi akasema mchongo (mpango) huo ni mzuri,” alisema na kuongeza kuwa;
“Siku hiyo mimi nilimwambia tukutane pale msibani kwa John, akasema yeye anakwenda kumwona Bi Mkubwa (mama yake), nikamwambia sasa unaondoka itakuwaje jamaa anataka tuzungumze, alikuwa ni mtu ambaye analazimisha sana kuondoka tena akaniambia lazima tuondoke wote.”
Wakati wa mazungumzo hayo Kitale aalisema yeye alikuwa akitokea Mkoani Iringa ambapo Marehemu Sharo alikuwa Dar es Salaam akijiandaa kwa safari ambapo alimsisitiza aondoke naye kwenda Tanga lakini Kitale alikataa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment