ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 5, 2012

Uchaguzi uliofutwa kwa rushwa wafanyika


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdala Bulembo Majura, akisalimia na mmoja wa makada wa chama hicho Juma Simba, wakati wa sherehe za kumpongeza kwa ushindi katika uchaguzi w ajumuia hiyo uliofanyika mjini Dodoma, zilizofanyika katika viwanja vya mnazi Mmoja Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwenyekiti wa  Jumuiya hiyo Mkoa wa  Dar es Salaam  Angela Kizigha. Picha na Emmanuel Herman 
HATIMAYE Mkutano wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Pwani uliositishwa hivi karibuni kwa madai ya kugubikwa na mazingira ya rushwa, umefanyika jana mjini Kibaha.
Uchaguzi huo ulishuhudia baadhi ya makada maarufu wa chama hicho wakianguka katika uchaguzi huo, wakati akiwamo waziri na wabunge walipeta katika nafasi za uwakilishi katika kamati ya siasa ya mkoa huo.
Uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Oktoba 17, uliahirishwa na hivyo mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao baada ya kuwapo kwa taarifa za kugubikwa na vitendo vya rushwa.

Siku hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo,  Mwantumu Mahiza, aliwaeleza wajumbe hao kuwa alipata taarifa kutoka vyombo vya usalama kuwa uchaguzi huo umegubikwa na rushwa.

Hata hivyo, juzi uchaguzi huo ulirudiwa kwa ajili ya kuwachagua Katibu wa Uchumi, Fedha na Mipango, Katibu Mwenezi na wajumbe wa Halmashauri ya Mkoa, ambapo Mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Imani Madega ambaye aliangukia pua.

Madega alikuwa akiwania nafasi ya Katibu wa Uchumi, Fedha na Mipango dhidi ya Mbaraka Dau na Haji Abuu Jumaa ambaye ni Meneja wa Mradi wa Benki ya Kijamii ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa, iliyozinduliwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete mjini  Dodoma.

Jumaa ndiye aliyeibuka kidedea katika uchaguzi wa awamu ya pili baada ya wagombea wote kutopata kura za kutosha kumtangaza mmojawapo kuwa mshindi. Mlao alisema katika awamu ya kwanza, Madega akipata kura nane, Dau kura 30 wakati Jumaa aliongoza kwa kupata kura 34.

Katika awamu ya pili, Dau alipata kura 34 na Jumaa kura 37 na hivyo mjumbe huyo kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya Katibu wa Uchumi, Fedha na Mipango wa CCM mkoani Pwani.

Katika nafasi ya Katibu Mwenezi,  Mbunge wa zamani wa Kibaha Mjini, Dk Zainab Gama, aliibuka kidedea katika uchaguzi ambao pia ulirudiwa kwa awamu mbili.

Katika awamu ya kwanza Dk Gama alipata kura 32 dhidi ya wapinzani wake na kura walizopata wakiwa ni Mohamed Kiaratu (kura mbili), Philemon Mabuga kura 14 na Jabir Masenga kura 16.

Matokeo hayo ya kura hayakutoa mshindi na kulazimika kurudiwa ndipo Dk Gama aliweza kuibuka mshindi kwa kupata kura 43 dhidi ya 28 za Masenga aliyekuwa akitetea nafasi yake.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Mbunge wa Kisarawe, Selemani Jafo na Mbunge wa Viti Maalumu, Subira Mgalu waliungana na makada wengine  kwa kushinda nafasi za ujumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa wa Pwani.

Mlao aliwatangaza wengine kuwa ni Katherine Katele na Madega ambaye hata hivyo alikubali nafasi hiyo kwa shingo upande, huku akidai kwamba hakuwa amepanga kuwania.

Bulembo alakiwa Dar
Wakati huohuo, mamia ya makada wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, jana walijitokeza kumlaki Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah
Bulembo aliyewasili akitokea  Dodoma alikoibuka mshindi kwa nafasi hiyo.

Bulembo aliyeambatana na viongozi wengine wa jumuiya hiyo alilakiwa kwa maandamano yaliyojaa mbwembwe na kila aina ya pilikapilika za  wanaCCM waliofurika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Akizungumza baada ya mapokezi hayo, Bulembo aliwataka wanaCCM kuhesabu wanachama wao ili kuweza kuwa na programu za kukijenga chama kuanzia ngazi za chini.

"Tunataka kuhakikisha upinzani unaambulia patupu katika uchaguzi unaohusisha vyama vya siasa," alisema Bulembo.

Alisema safu ya viongozi wa jumuiya hiyo waliochaguliwa hivi karibuni, kazi yao kubwa itakuwa kuzunguka mikoani kwa lengo la kukijenga chama na kuwataka viongozi wa chama na jumuiya hiyo. Pia kuacha tabia ya kuwachangisha fedha wanachama anapofika kiongozi kufanya mkutano na wananchi.

"Hapo ndipo ambako rushwa inaanzia na kuwafanya baadhi ya wanachama kufanya usaliti," alisema na kuongeza kuwa kuna ambao wanatoa fedha nyingi kufanikisha ziara za viongozi wa chama, ambao hawana nia nzuri na matokeo yake ndiyo kama ambayo yanaonekana hivi sasa.
Mwananchi

No comments: