
Dk Shukuru Kawambwa
WAKATI Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili ukianza leo nchini kote, Serikali imesema kuanzia sasa, mtihani huo utakuwa ni wa mchujo kuanzia sasa, hivyo atakayefeli atatimuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema mtihani wa mwaka huu, matokeo yake yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
"Mtihani wa kidato cha pili kama ilivyo mitihani mingine ya taifa ni muhimu sana. Matokeo ya mtihani huu hutumiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kama sehemu ya matokeo katika mtihani wa taifa wa elimu ya sekondari kidato cha nne," alisema Dk Kawambwa.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Dk Kawambwa alisema kurudishwa kwa mchujo katika mtihani huo ni moja ya njiia ya kuboresha elimu nchini na kupata wanafunzi walio bora nchini.
Alisema hayo ni mabadiliko ya kawaida na yataendelea kuwapo katika sekta hiyo kila mwaka
"Tunachopambania hapa ni ubora wa elimu nchini na hii itasaidia kuondoa wanafunzi wanaosemekana wanamaliza shule hawajui kusoma, japokuwa mimi siamini kama ni kweli," alisema Dk Kawambwa.
Alisema mtihani huo utamalizika Novemba 16, mwaka huu na idadi ya shule na vituo vilivyosajili watahiniwa mwaka huu ni 4,242 ikiwa ni ongezeko la vituo 55 ikilinganishwa na vile vilivyosajiliwa mwaka 2011 ambavyo vilikuwa 4,187.
"Kwa hiyo kwa mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 1.3," alisema Dk Kawambwa
Alisema watahiniwa 442,925 wamejiandikisha kufanya mtihani. Kati yao wasichana ni 214,325 (sawa na asilimia 48.39) na wavulana ni 228,600 (sawa na asilimia 51.61).
"Wizara inaagiza wadau wote wa elimu katika kanda, manispaa na halmashauri za wilaya pamoja na wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote walioandikishwa kufanya mtihani wanafanya bila kukosa," alisema Dk Kawambwa.
Januari mwaka huu Serikali iliamua kurudisha mtihani huo kwa lengo la kupunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa uamuzi wa Serikali wa kurudisha mtihani huo, umezingatia vigezo katika kuboresha matokeo ya kidato cha nne.
Mulugo alisema kuwa kuwapo kwa mtihani huo kutapunguza idadi ya wanaoshindwa kufaulu kidato cha nne.
“Kumekuwa na wanafunzi wazembe ambao wamefanya kupungua kwa idadi ya ufaulu kutokana na kukosekana kwa mtihani wa kidato cha pili, ambao ndiyo mwongozo wa mwanafunzi kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali,” alisema Mulugo.
1 comment:
Hawa mawaziri wa siku hizi wanatoka wapi??? Matokeo ya form4 na Form 6 ni wake-up call kwa wizara hii kuona kuwa hawa watoto hawapati elimu inayostahili! Hata mimi nilichukua sayansi (PCB) enzi za 80's lakini hakukuwa na mabuyu kama niliyoyaona matokeo ya form six, how could a child go to high school for 2 years and he or she can not pass exam??? badala ya kutoa lugha za vitisho kuwa mtawatimua watoto you need to sit down with headmistress wakuambie what the hell is going on in the schools???? labs nasikia hakuna tena, angalia Tambaza, azania na Jangwani yaani i cried nilipokwenda nyumbani last year, yamebaki magofu hata rangi kupaka inakuwa tabu, vyoo eti havifanyi kazi, OMG hii wizara ni wizara muhimu sana na mkiendelea kuwapa mawaziri kama hawa kuongoza ndiyo watoto wetu wataishia kuuza mihogo watoto wao wapo Nairobi, Uganda or London you do your investigation, watoto wote wa viongozi siku hizi hawasomi shule za serikali siyo enzi zetu mimi baba yangu alikuwa waziri wakati wa nyerere na nimesoma na watoto wa mawaziri, waziri mkuu primary enzi hizo alikuwa msuya. THAT IS THE COUNTRY WE WANT THATS WHY THEY DO NOT GIVE A DAMN ABOUT THIS SCHOOL CAUSE THEIR KIDS ARE IN FOREIGN COUNTRY GETTING 1ST CLASS EDUCATION NA WANARUDI WANAKUWA MADIRECTOR AND WANAWARITHI WAZAZI WAO. ANGALIA LAST NAMES ZA VIJANA WALIO KWENYE SIASA NA ANGALIA HISTORIA YAO YA MASOMO WOTE WAMESOMA NJE SISI WENGINE TUMESOMEA MACHAME, WERUWERU, OLD MOSHI TUNAKULA MAKANDE NA WATOTO WA VIONGOZI ENZI HIZO ZA NYERERE!
Post a Comment