ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 5, 2012

Yanga mbele daima,nyuma mwiko' Simba yaloa, Kaseja amwaga chozi

Mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu (kushoto) akijaribu kutuliza mpira kifuani, kulia ni kiungo wa Yanga, Frank Domayo wakiwa wamembana kiungo wa Azam Jabir Stima (katikati),katika mechi ya kuwania Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa jana. Yanga ilishinda 2- Picha na Michael Matemanga 
MABINGWA mara 22 wa Tanzania, Yanga wamekalia usukani wa Ligi Kuu baada ya kuichapa Azam mabao 2-0, huku Simba ikipokea kipigo kama hicho kutoka kwa Mtibwa Sugar.

Washambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu na Hamisi Kiiza kila mmoja alifunga bao katika kila kipindi na kuifanya Yanga kufikisha pointi 26 na kuiacha Simba kwenye nafasi ya pili ikiwa na pointi 23 na Azam ya tatu (21).


Rekodi ya kutofungwa kwa mabingwa watetezi Simba ilivunjwa rasmi jana kwenye Uwanja wa Jamhuri baada ya washambuliaji Mohamed Mkopi na Hussein Javu kutumia vizuri makosa ya nahodha Juma Kaseja kuipa Mtibwa Sugar ushindi huo mnono.

Katika mechi hizo mbili zilizohusisha Yanga na Azam na Mtibwa Sugar dhidi ya Simba jumla ya wachezaji 12 wa kigeni walianza kwenye vikosi vyao.  

Yanga iliyoanza na wachezaji wanne wa kulipwa ambao ni Kavumbagu,  Kiiza, Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite ilisubiri kwa dakika tisa kabla ya mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kavumbagu kufunga bao la kwanza akimalizia mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki wa Azam baada ya Simon Msuva kupiga shuti lililomgonga Aggrey Morris kabla ya kumkuta mfungaji aliyeuweka mpira nyavuni kirahisi.

Hilo ni bao la sita kwa Kavumbagu msimu huu tangu alipojiunga na Yanga akitokea Atletico ya Burundi.

Wakati Mburundi huyo akijinasibu, nyota wa Uganda, Kiiza aliihakikisha Yanga pointi tatu muhimu kwa kupachika bao la pili katika dakika ya 67 akimalizia krosi nzuri ya Athuman Idd 'Chuji'.

Yanga walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo na kumkaribisha rasmi kocha Stewart Hall nchini tangu waliposababisha atimuliwe kutokana na Azam kufungwa na Yanga kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame.

Vijana wa Hall walijitahidi kufurukuta kusaka bao la kusawazisha kwa kufanya mashambulizi kupitia kwa washambuliaji wao John Bocco na Hamisi Mcha katika dakika ya 17 na 19, lakini ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya Nadir Haroub na Kelvin Yondani ilikuwa makini kuokoa hatari hizo.

Yondani alicheza kwa mara ya kwanza tangu alipoumizwa mguu na Haruna Moshi wa Simba Oktoba 3 na alionyesha uhai mkubwa kwenye safu ya ulinzi wa Yanga katika kuwakabili washambuliaji wa Azam.

Katika mechi hiyo mshambuliaji Msuva wa Yanga alipiga shuti kali katika dakika ya 46, lakini kipa Mwadini wa Azam akalidaka na Azam walijibu mapigo dakika tatu baadaye baada ya  Kipre Tchetche kupitisha pasi nzuri kwa Bocco, lakini Idd Chuji aliwahi na kuokoa mpira huo.

Kocha wa Azam, Hall aliwatumia nyota watatu wa kimataifa Kipre Tchetche, Kipre Boluo na Ibrahim Shikanda katika mechi hiyo.

Kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, mabingwa watetezi, Simba waliingia uwanjani wakiwa na wachezaji watano wa kulipwa Paschal Ochieng, Koman Keita, Felix Sunzu, Daniel Akuffo na Emmanuel Okwi, lakini walishindwa kuisaidia timu yao baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0.

Katika mechi hiyo mabingwa wa 2000, Mtibwa Sugar walianza mchezo kwa kasi na dakika ya 15, Jamal Mnyate alipiga shuti lililopanguliwa na kipa Juma Kaseja.

Simba walijibu mapigo katika dakika ya 23, lakini shuti la mshambuliaji Daniel Akuffo lilipaa juu akiwa yeye na kipa.

Katika mechi hiyo Mtibwa walipata bao la kuongoza katika dakika ya 3 ya mchezo ambalo lilifungwa na Mkopi akitumia vizuri mpira uliotemwa na kipa Kaseja wakati akijaribu kupangua shuti la Vincent Barnabas.

Mwamuzi Judith Gamba kutoka Arusha na wasaidizi wake Saad Tibabimale (Mwanza) na Elen Mduma (Dar es Salaam) walijikuta kwenye wakati mgumu baada ya mashabiki wa Simba kuwarushia chupa wakati wa mapumziko.

Baadhi ya mashabiki wa Simba waliingia uwanjani na chupa za vioo na kurusha uwanjani na kuhatarisha maisha ya waamuzi hao kwenye Uwanja wa Jamhuri kabla ya polisi kuingilia kati na kumkamata shabiki mmoja.

Simba iliwapumzisha Akuffo, Ochieng na kuwaingiza Said Nassoro na Mrisho Ngassa, mabadiliko hayo hayakutosha kuifanya safu ya ushambuliaji ya Simba kumfunga kipa Hussein Shariff aliyekuwa kikwazo kwao.

KASEJA AMWAGA CHOZI
Mshambuliaji Javu aliyeingia kuchukua nafasi ya Mkopi katika dakika ya 80 aliifungia Mtibwa bao la pili baada ya Kaseja kufanya makosa.

Baada ya filimbi ya mwisho Kaseja aliangua kilio na kuchana jezi yake uwanjani na kusababisha azongwe na mashabiki huku wachezaji wengine wa Simba wakiingia kwenye basi lao na kubadilisha nguo halafu wakaondoka wakitembea kwa miguu wakitoka uwanjani.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime aliwasifu wachezaji wake kwa kucheza vizuri na kutumia nafasi walizopata kufunga mabao hayo.

Katika mchezo mwingine uliofanyika Uwanja wa Mabatini, Ruvu Shooting walilazimishwa sare 0-0 na Toto African, huku Kagera Sugar ikiichapa Prisons 2-0 mabao yaliyofungwa na Themi Felix na Welfred Emmeh kwa mkwaju wa penalti.

Imeandaliwa na Calvin Kiwia, Lilian Lucas na Kalunde Jamal ( Morogoro), Msafiri Sanjito (Pwani) wa Gazeti la Mwananchi

No comments: