
Hujawahi kuona watu wanaishi, kila mtu anajua ni wapenzi lakini ndani yao ni kama hakuna kupendana. Yaani wanaishi kwa mazoea tu! Moja ya sababu za wapenzi kufikia hatua hiyo ni mmoja kumuona mwenzake ni mzigo mzito kuubeba.
Tabia hiyo ni sumu hatari kwa maana wapo walioshindwa kupata wenzi wa maisha yao, kwani kila mmoja alimkimbia. Maisha magumu lakini wewe hutaki kutambua hilo, badala yake unataka mahitaji lukuki. Unapaswa kujiuliza wewe umefanya nini?
Angalau basi, kama wewe ni wa kupewa, ufanye juu chini kuhakikisha unapunguza matumizi. Ila wewe ndiye mkali wa kuongeza mahitaji. Ni rahisi kuachwa kwa sababu mtoaji atakapoanza kujiuliza, mwisho wa maswali yake atapata jibu kuwa wewe ni mnyonyaji.
CHUKUA MUONGOZO HUU
Hebu ishi kwa mtindo wa kula na kipofu. Yeye anakupa, sasa kazi kwako kuhakikisha unampa faraja na amani. Ana fedha, wewe huna, kwa hiyo mahitaji yako yanamtegemea yeye, jitahidi kujikomboa ili nawe uwe unaingiza kipato cha kukutosheleza na wakati unapigania hilo, hakikisha unakuwa faraja yake.
Inakuwaje uombe vocha ya simu lakini akikupa, simu unawapigia wengine. Akupigie yeye tu. Nani kakudanganya kwamba yeye ni zezeta wa kiwango hicho? Atakuacha katika kipindi ambacho wewe umetunga kiburi kwenye kichwa chako kuwa hawezi kufurukuta mbele yako.
Ni utani kuamini kuwa hana ujanja mbele yako. Asilimia kubwa walioweka kiburi cha namna hiyo, mwisho walipata shida baada ya kuachwa. Mapenzi hujengwa na vimelea vyake ambavyo ni upendo, heshima na utu. Kama kimoja kati ya hivyo hakuna, hayatafika popote. Yatakufa!
Atakupenda kama nawe unampenda. Anapokuwa anaonesha upendo wa hali ya juu kwako lakini yeye humpi, itafika kipindi atakuona hufai. Ataanza kupunguza, mwisho atachoka kabisa. Hii ndiyo sababu ya kukwambia ‘unapopewa, jiulize nawe unatoa nini’. Zingatia kuwa mapenzi ya upande mmoja ni ya kizamani.
Usitarajie heshima kutoka kwa mwenzi wako ikiwa wewe humheshimu. Namna unavyo unamtendea ndivyo unavyokaribisha uhusika wake kwako. Atakuheshimu mno kama nawe unamuonesha utiifu. Hata wasaliti wengi, wamejikuta wakisalitiwa baada ya kuwaonesha wenzi wao jinsi wasivyo waaminifu.
Onesha utu ili uendelee kufaidi upendo na huduma. Mwenzi wako amekuwa akitumia fedha nyingi kukuhudumia, jambo ambalo unalodaiwa kwake ni utu. Hakikisha unampa faraja mpaka hajutii kile anachokitoa kwake. Faraja siyo mapenzi ya kitandani peke yake.
Unapaswa kutuliza akili na ujue mwenzi wako anahitaji nini kutoka kwako. Ukishakifahamu, ni juhudi yako kuhakikisha hakikosi. Kufanya hivyo ndiyo utu na ndivyo utakavyoweza kumteka zaidi na zaidi. Anakapokuwa anakutendea lakini maombi yake huyapokei vizuri, unakuwa unamkatisha tamaa.
Kadiri unavyomkatisha tamaa ndivyo unavyoelekea kumvunja moyo. Tambua kwamba moyo unapovunjika inakuwa ni ngumu mno kuurejesha kwenye hali yake ya kawaida. Kwa maana hiyo unakuwa umepoteza upendo na huduma zote ulizokuwa unazipata kutoka kwake.
Mapenzi ni mchezo wa nipe nikupe. Nipe upendo na wewe nikupende. Inawezekana yeye ndiye alianza kukupenda ndiyo maana akafanya juu chini mpaka mkawa pamoja. Baada ya hatua hiyo ni muhimu kwako kuhakikisha unaonesha upendo kwa sababu mmekubaliana kupendana.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment