Mpenzi msomaji wangu, machozi kwa binadamu yana maana tofauti. Wapo wanaojikuta wakitoa machozi pale furaha inapozidi kipimo, wengi wanayaita machozi ya furaha.
Kuna wanaotoa machozi haya pale wanapofanikiwa kuingia kwenye ndoa na watu waliotokea kuwapenda lakini pia kuna wanaotoa machozi haya pale wanapopata furaha waliyoitarajia.
Machozi haya sina tatizo nayo na nasisitiza wapenzi kupeana furaha katika kila siku ya maisha yao kwani kwa kufanya hivyo amani itatawala.
Wakati nikisisitiza hilo, niseme tu wazi kwamba hakuna kitu ambacho kimekuwa kikiniuma kama kumuona mtu akimpa machungu mpenzi wake kiasi cha kumfanya awe ni mtu wa kulia kila wakati.
Huwa najiuliza, mwanaume anapomfanyia vituko mpenzi wake kiasi cha kumfanya awe ni wa kutoa machozi kila wakati anafaidika nini?
Anapata raha gani mwanamke ambaye kila siku ni wa kufanya mambo ya ajabu kiasi cha kumfanya mpenzi wake kuwa ni mtu wa kujifuta machozi kila saa?
Mapenzi ni kupendana na huwezi kusema unampenda mtu fulani kama utakuwa unamsababishia machungu moyoni mwake. Utakuwa ni mtu wa ajabu kama umeingia kwenye uhusiano na mtu kisha ukasema umempa nafasi kwenye moyo wako wakati unamsaliti kila wakati na kumfanya aumie.
Kama kweli huyo uliyenaye unampenda basi mfanye siku akitoa machozi yake yawe ni kwa mambo ya furaha uliyomtendea. Kumfanya mpenzi wako awe ni mtu wa kuwa karibu na ‘hanjifu’ yake kwa kuwa kila akikumbuka unayomfanyia anatoa machozi ni kujitafutia dhambi ambazo unaweza kuziepuka
Ni dhambi kwa kuwa, hatukuumbwa ili tuwatese wenzetu. Unapompiga mkeo au mpenzi wako mpaka unamtoa manundu unamuudhi hata Muumba wako na mwisho wake hauwezi kuwa mzuri.
Mimi nadhani ifike wakati uone ni dhambi kubwa sana kumfanya mpenzi wako atoe machozi. Hata kama kakukosea, adhabu yake isiwe ya kumliza.
Unapokuwa ni mtu wa kumliza mpenzi wako kila mara ujue inaweza ikafika wakati akachoka na kuamua kukuacha, uko tayari kwa hilo? Kama uko tayari yeye kukuacha wewe humpendi hivyo bora umuambie kuliko kuendelea kuwa naye.
Lakini katika hili naomba niseme hakuna kitu kinachodhoofisha mapenzi kama kulizana. Mbaya zaidi ni kwamba sasa hivi wanaolizwa si wanawake tu. Wapo wanaume ambao nao wamekuwa ni watu wa kulia kwa sababu ya mapenzi.
Kwa nini wanalia? Ni kwa sababu wanafanyiwa mambo ya ajabu na watu ambao waliwaamini na kuwakabidhi mioyo yao lakini kumbe wameingia ‘choo cha kike’.
Tusiwe watu wa kuwafanya wapenzi wetu wajute kuwa na sisi. Tuyaruhusu machozi ya furaha kwa wapenzi wetu lakini machozi ya huzuni kwao iwe ni pale inapobidi na isiwe ndiyo mfumo wetu wa maisha ya kila siku.
Ni hayo tu kwa leo.
Chanzo: Global Publishers
No comments:
Post a Comment