ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 12, 2012

UNAPOPEWA, JIULIZE UNATOA NINI? USIENDEKEZE MAPENZI YA KIZAMANI -4

WIKI iliyopita nilikushauri ujaribu kuishi kwa mtindo wa kula na kipofu. Unapomshika mkono unamfanya agundue ubaya wako. Unampiga mizinga sana, yeye hata faraja kutoka kwako hapati. Matokeo si mengine zaidi ya kuachana.

Inakuwaje uombe vocha ya simu lakini akikupa, simu unawapigia wengine. Akupigie yeye tu. Nani kakudanganya kwamba yeye ni zezeta wa kiwango hicho? Atakuacha katika kipindi ambacho wewe umetunga kiburi kwenye kichwa chako kuwa hawezi kufurukuta mbele yako.
Ni utani kuamini kuwa hana ujanja mbele yako. Asilimia kubwa walioweka kiburi cha namna hiyo, mwisho walipata shida baada ya kuachwa. Mapenzi hujengwa na vimelea vyake ambavyo ni upendo, heshima na utu. Kama kimoja kati ya hivyo hakuna, hayatafika popote. Yatakufa!
Atakupenda kama nawe unampenda. Anapokuwa anaonesha upendo wa hali ya juu kwako lakini yeye humpi, itafika kipindi atakuona hufai. Ataanza kupunguza, mwisho atachoka kabisa. Hii ndiyo sababu ya kukwambia ‘unapopewa, jiulize nawe unatoa nini’. Zingatia kuwa mapenzi ya upande mmoja ni ya kizamani.
Usitarajie heshima kutoka kwa mwenzi wako ikiwa wewe humheshimu. Namna unavyomtendea ndivyo unavyokaribisha uhusika wake kwako. Atakuheshimu mno kama nawe unamuonesha utiifu. Hata wasaliti wengi, wamejikuta wakisalitiwa baada ya kuwaonesha wenzi wao jinsi wasivyo waaminifu.
Onesha utu ili uendelee kufaidi upendo na huduma. Mwenzi wako amekuwa akitumia fedha nyingi kukuhudumia, jambo unalodaiwa kwake ni utu. Hakikisha unampa faraja mpaka hajutii kile anachokitoa kwake. Faraja siyo mapenzi ya kitandani peke yake.
Unapaswa kutuliza akili na ujue mwenzi wako anahitaji nini kutoka kwako. Ukishakifahamu, ni juhudi yako kuhakikisha hakikosi. Kufanya hivyo ndiyo utu na ndivyo utakavyoweza kumteka zaidi na zaidi. Atakapokuwa anakutendea lakini maombi yake huyapokei vizuri, unakuwa unamkatisha tamaa.
Kadiri unavyomkatisha tamaa ndivyo unavyoelekea kumvunja moyo. Tambua kwamba moyo unapovunjika inakuwa ni ngumu mno kuurejesha kwenye hali yake ya kawaida. Kwa maana hiyo unakuwa umepoteza upendo na huduma zote ulizokuwa unazipata kutoka kwake.
Mapenzi ni mchezo wa nipe nikupe. Nipe upendo na wewe nikupende. Inawezekana yeye ndiye alianza kukupenda ndiyo maana akafanya juu chini mpaka mkawa pamoja. Baada ya hatua hiyo ni muhimu kwako kuhakikisha unaonesha upendo kwa sababu mmekubaliana kupendana.
Kupenda siyo maigizo, kusema utamfanyia magirini mwenzi wako ili utimize matakwa yako fulani. Kila aliyeingia kwenye uhusiano kwa malengo tofauti na upendo alifeli. Unaposoma makala haya, ikupe njia nzuri ya kutimiza wajibu wako kwenye mapenzi halafu umuache naye atimize kwa upande wake.
Unapokuwa unatimiza wajibu wako, hebu jiulize naye anafanya nini? Ni hatari sana kuendelea kuonesha unampenda na kumjali, wakati yeye hakujali kwa chochote. Mapenzi siyo tu kwamba yapo, ila yamekuwepo kwa ajili ya kupeana faraja.
Kama mwenzi wako hakufariji maana yake unatakiwa uhame hapo ulipo. Jinsi utakavyokuwa unazidisha upendo, haitakusaidia, kwani ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa. Badala ya kukushukuru, yeye atakuona zezeta uliyekufa kwake. Unatakiwa kuutetea moyo wako.
Naomba nikushauri kuwa akili yako iwe hai kila siku. Uwekezaji wako uendane na kile ambacho wewe unakipokea kutoka kwa mwenzi wako. Kufanya zaidi au pungufu ni kosa kubwa. Kufanya zaidi maana yake unakuwa unaunyanyasa moyo wako na pungufu unakuwa humtendei haki mwenzio.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: