ANGALIA LIVE NEWS
Thursday, November 8, 2012
Wakili wa Serikali akwamisha kesi dhidi ya Makunga
James Magai
WAKILI Mwandamizi wa Serikali, Proseper Mwangamila amekwamisha usikilizaji wa kesi ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Theophil Makunga na wenzake wawili.
Wakili huyo, jana hakufika mahakamani na hivyo kusababisha mashahidi wawili wa upande wa mashtaka, waliokuwa wameitikia wito wa kwenda mahakamani, washindwe kutoa ushahidi wao.
Mashahidi hao ni mpelelezi wa kesi hiyo, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Hiza na Kamishna Msaidizi wa Magereza, George Mwambashi.
Hatua ya Wakili Mwangamila kutokuwepo mahakamani, iliilazimisha mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi Januari mwakani.
Ilipoitwa jana, Wakili wa Serikali, Beatha Kitau aliiambia mahakama kuwa Mwangamila ameshindwa kufika kwa kuwa ana udhuru na akaomba mahakama ipange siku nyingine ya kuendelea na usikilizaji.
Upande wa utetezi haukuwa na pingamizi na Hakimu Lema aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 14 mwakani.
Hakimu Lemapia alisema kesi hiyo itatajwa Desemba 6 mwakani.
Makunga ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, anakabiliwa na shtaka la kutumia mitambo ya kampuni yake, kuchapisha gazeti la Tanzania Daima likiwa na makala inayodaiwa kuwachochea askari wa majeshi mbalimbali nchini kutokuitii Serikali.
Wakati gazeti hilo lilipochapiswa likiwa na makala hiyo yenye kichwa cha habari “Waraka Maalumu kwa askari wote.” Makunga alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Sam Sholei kumaliza muda wake.
Mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Samson Mwigamba, mwandishi wa makala hayo na mshtakiwa wa pili ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media inayochapisha gazeti hilo, Absalom Kibanda.
Kibanda anadaiwa kuruhushu makala hayo kuchapishwa katika gazeti lake.
Shahidi wa kwanza upande wa mashtaka katika kesi hiyo ni Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Magazeti, Raphael Hokororo.
Katika ushahidi wake alioutoa Oktoba 22 mwaka huu, Hokororo alidai kuwa Novemba 30 mwaka 2011, alipokea magazeti mbalimbali likiwemo gazeti la Tanzania Daima, ambalo katika safu ya Kalamu ya Mwigamba, lilikuwa na makala “Waraka maalumu kwa askari wote”.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, Hokororo alidai kuwa waraka huo ulikuwa maalumu kwa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza na kwamba yalikuwa yakiwashawishi askari wakatae kutii amri za wakuu wao.
Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee ukurasa uliodaiwa kuwa ni wa gazeti hilo wenye makala hiyo inayobishaniwa ili uwe kielelezo cha usahidi.
Hata hivyo Mawakili wa upande wa utetezi, Isaya Matambo na Gabriel Mnyele anayemtetea Makunga akisaidiana na Frank Mwalongo, waliupinga wakidai kuwa ukurasa huo hauonyeshi sifa ya kuwa gazeti na kwamba halijulikani kuwa ni gazeti gani.
“Upande wa mashtaka lazima utoe gazeti zima ambalo Hokororo alilipokea na kulisoma, hilo siyo gazeti na kuna uwezekano wa kuwa upande wa mashtaka ulichapa kitu kingine kwenye chapisho hilo,” alidai Mnyele.
Baada ya pingamizi hilo, Wakili Mwangamila aliliondoa ombi la kuwasilisha nakala ya gazeti hilo kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo na kwamba atakitenda mtu mwingine baadaye.
Makunga alipandishwa kizimbani na kusomewa shtaka linalomkabili kwa mara ya kwanza Machi 26 mwaka huu.
Akimsomea shtaka hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Elizabeth Kaganda alidai kuwa Makunga alifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 32 (1) (c) na 31 (1) (a) cha sheria ya magazeti sura ya 229 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kaganda alidai kuwa Novemba 30, 2011, Makunga akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications aliruhusu mitambo ya kampuni hiyo kuchapisha waraka wenye kichwa cha habari, “Waraka Maalumu kwa askari wote” ulioandikwa na Samson Mwigamba, kwenye gazeti la Tanzania Daima toleo la 2553.
Hata hivyo Makunga alikana shtaka hilo na aliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment