Ni vyombo vya starehe kwa kila atakayejitokeza mbele yake, kwa nini? Eti hana mvuto, hana thamani, hakuna ambaye atakuwa tayari kuunganisha naye familia. Hayo ni mawazo tasa rafiki zangu.
Kujishusha thamani ni jambo baya sana maishani. Lazima ujijue na uitambue thamani yako ndipo mwingine naye ataweza kuona thamani yako. Nilianza wiki jana kwa kueleza jambo la kwanza, ambapo nilisisitiza suala la kujijali. Hebu sasa twende tukaone mambo mengine ya msingi katika sehemu hii ya mwisho.
JAMBO LA PILI
Hapa nitakazia suala la kujiamini. Hili ni tatizo lingine ambalo kwa kweli ni la kisaikolojia zaidi kwa sababu kuna baadhi ya watu wanakosa kujiamini. Kuna mwingine anaweza akakaa kwenye kioo kwa saa kadhaa na kuanza kujitoa kasoro katika mwili wake.
Hujiona mbaya asiyevutia na ambaye hana thamani kabisa katika ulimwengu wa mapenzi, hujiona hawezi kupata mpenzi katika maisha yake yote baada ya kujitoa kasoro hizo.
Nani amekuambia kuwa una kasoro ndugu yangu, mshukuru Mungu kwa kukuumba jinsi ulivyo, amini kuwa Mungu ana makusudi yake kukuumba kama ulivyo. Heshimu uumbaji wake na jiamini kwamba umekamilika.
Kujitoa kasoro na kutojiamni ni kosa baya kwa kuwa unakuwa unajiathiri kisaikolojia na kujiona hufai kabisa kupedwa mwisho wa yote unakuja kumparamia mtu yeyote kwa nia ya kujiondolea mkosi na akishakutumia anakuacha solemba unabaki na machungu moyoni na kujiongezea matatizo zaidi.
Naamini baada ya kujipenda wewe mwenyewe na kujiamini kuwa unavutia, utakuwa katika hali ya kawaida kisaikolojia na wakati mwingine sasa anaweza akajitokeza akupendaye na kukuomba hifadhi ya moyo katika moyo wako.
Sababu ya kukaa muda mrefu bila mpenzi au kutamkiwa kuwa unapendwa isiwe chanzo cha kupata maumivu mapya ya moyo. Acha papara, tulia, pata wasaa wa kumchunguza huyo anayedai anakupenda kwa muda wa kutosha kwa kuwa inawezekana naye akawa ni mmoja kati ya wale wanaotaka kukufanya chombo cha starehe!
Baada ya kukuomba muwe pamoja kimapenzi unatakiwa kumchunguza kwanza na hata baada ya kumchunguza usiruhusu aujue mwili wako kabla ya kuelewa nia yake hasa kwako ni ipi, starehe ya muda mfupi au anakuhitaji kimaisha.
Usifanye mambo kwa papara, unahitaji utulivu wa kutosha ili uweze kumpata yule ambaye ni muhimu kwa ajili yako. Ukijiamini na kuwa makini ni wazi kuwa utampata yule anayekupenda kwa dhati. Bila shaka tumeelewa.
Ahsanteni sana marafiki kwa kunisoma. Hadi wiki ijayo katika mada nyingine kali, USIKOSE!
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment