Tutakuwa na kila sababu ya kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba kuna ambao licha ya leo kuwa wazima wanaweza wasiuone mwaka huo na yawezekana kabisa kati yao wakawemo mimi na wewe! Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe kati ya wale watakaouona mwaka huo wakiwa wazima.
Endapo dua yetu itakubalika, tutakuwa na kila sababu ya kuhakikisha tunayaangalia upya maisha yetu ya kimapenzi. Tutatakiwa kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba, mapenzi yana nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku.
Kwa maana hiyo endapo tutaingia mwaka mpya tukiwa na wapenzi ambao ni ovyo hata maisha yetu kwa mwaka huo yatakuwa ya ovyo.
Hivyo basi, itakuwa ni jambo la busara kila mmoja kujiangalia na kuona kama mpenzi aliye naye anafaa au hafai kuingia naye katika mwaka huo ambao yawezekana umejiwekea malengo yako ambayo ili kuyatimiza lazima uwe na mtu sahihi.
Natambua wapo ambao mwaka 2012 umekuwa ni mchungu kwao. Wapo waliotoa machozi na kujuta kwa nini walipenda. Wapo waliokosa kabisa muda wa kuyafurahia maisha na wapenzi wao. Muda wao mwingi umekuwa ni wa huzuni huku wakiziona chembechembe za furaha kwa mbali sana.
Hii yote yawezekana ni kwa sababu waliingia katika mapenzi na watu ambao si sahihi. Huenda ulitokea kumpenda sana mtu f’lani ukiamini na yeye anakupenda lakini kwa bahati mbaya ukakuta tofauti, hiyo huwatokea wengi na wala si jambo la ajabu.
Lakini sasa umeshabaini kwamba umempenda mtu ambaye hana mapenzi na wewe, kuna sababu gani ya msingi ya kuendelea kumpa nafasi katika moyo wako? Unadhani ukimuacha utakufa au maisha yako yatayumba?
Elewa kwamba, kuendelea kumng’ang’ania mtu wa dizaini hiyo hakutakuwa na faida yoyote katika maisha yako badala yake utakuwa unajiongezea matatizo ambayo mwisho wake utalia na asitokee wa kukufuta machozi.
Ndugu zangu, ulimwengu wa sasa si wa kutafuta heshima ya kwamba una mpenzi au una mume hata kama hana vigezo vya kuwa naye. Nasema hivyo nikiwa na maana yangu.
Kuna baadhi ya wanawake ambao licha ya kwamba wapo katika uhusiano wa kimapenzi na wanaume ambao ni wakorofi, wasio na mapenzi ya kweli kwao, bado hawako tayari kuwakosa eti tu kwa sababu wanasema, kuwa na mtu ni heshima kuliko kuitwa ‘nungayembe’.
Kwa dhana hiyohiyo ndiyo maana ukijaribu kuchunguza utagundua kuwa wanawake wengi walio katika uhusiano wa kimapenzi iwe wameolewa au wako katika uhusiano wa kawaida, wanavumilia mengi kutoka kwa wapenzi wao hata katika yale ambayo hawastahili kuyavumilia. Ukiwauliza watakuambia hawako tayari kukosa heshima ya ‘kuwa na mtu’.
Mwanamke atakuwa tayari kuvumilia kipigo anachokipata kutoka kwa mumewe kila siku eti kwa sababu hataki kuikosa ile heshima ya kwamba ni mke wa mtu.
Wapo wasichana ambao wapenzi wao wanaonesha wazi kutowajali, kutowaheshimu na kuwafanyia kila aina ya vituko lakini wanavumilia eti kwa sababu wanahisi wakiachwa wanaweza kukosa wengine wa kuwapenda.
Jamani, hebu tujiulize, kuna raha gani ya kuwa na mpenzi ambaye hakupi kile ambacho ulikitarajia kutoka kwake? Mapenzi ni furaha na ukiwa na mtu ambaye hakupatii furaha hiyo, huyo si wa kumpa nafasi katika mwaka huu ujao, muweke pembeni huku ukiamini kuwa, kumuacha kwako ndiko kutampa nafasi yule mwenye mapenzi ya dhati kuwa na wewe.
Wengi wetu tunajizibia riziki hivihivi, unampa nafasi mtu ambaye unaona wazi hakupendi wakati yawezekana yuko mwingine pembeni ambaye ndiye aliyepangwa kuwa wako na anachosubiri ni umuache huyo uliye naye ili yeye achukue nafasi yake.
Niseme tu kwamba mapenzi ni sawa na kamari, unaweza kuwekeza penzi lako kwa mtu fulani matokeo yake ukaambulia mateso au kinyume chake.
Kwa maana hiyo tusiogope kucheza kamari katika mapenzi. Ukibaini umeingia kwa mtu ambaye hana mapenzi na wewe, si suala la kujilaumu bali chukulia poa kisha jipange upya.
Ni hayo tu kwa leo, niwatakie mwaka mpya mwema wenye mafanikio hasa katika maisha yako ya kimapenzi.
Chanzo:Global Publishers
1 comment:
Ushauri mzuri sana umenigusa!
Post a Comment