ANGALIA LIVE NEWS

Friday, December 7, 2012

Basi la Princes Muro latekwa, abiria wavuliwa nguo, waporwa

Na Abdallah Amiri, Igunga

BASI la Kampuni ya Princes Muro, lenye namba za usajili T 551 BQP, ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Kahama, mkoani Shinyanga, limetekwa na majambazi usiku wa kuamkia jana katika Kijiji cha Igogo, Wilaya Igunga, mkoani Tabora.

Akizungumza na gazeti hili, abiria wa badi hilo ambaye alijeruhiwa na majambazi hao kichwani, Bw. Brayandi Sangatwa (67), alisema wakiwa njiani kabla ya kufika Kijiji cha Igogo, basi hilo liliharibika ambapo mafundi walianza kulitengeneza hadi saa saba usiku.

“Baada ya matengenezo kukamilika, tulianza safari na baada ya kufika kijijini hapo, tulikuta mawe makubwa yakiwa yamepangwa katikati ya barabara na kuanza kushambuliwa kwa mawe.


“Hawa majambazi walikuwa na fimbo, mapanga pamoja na mawe, abiria wote tuliamuriwa kushuka mmoja mmoja, kuvua nguo zote 
na kulala kifudifudi, majambazi walichukua fedha zetu na simu
za mkononi,” alisema Bw. Sangatwa.

Aliongeza kuwa, yeye alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya 
miguu hivyo aliwaomba majambazi hao ashuke pole pole 
kutoka ndani ya basi hilo.

Alisema jamabazi hao hawakukubaliana na ombi hilo hivyo waliamua kumvuta kwa nguvu, kumtoa ndani ya basi na kumwamuru atoe fedha zote.

“Niliwajibu sina fedha zozote wakaamua kunipiga fimbo kichwani, kuchukua sh. 80,000 na kuniachia simu ya mkononi ambayo nilikuwa nimeilalia katika mkono wa kushoto,” alisema.

Alidai baada ya majambazi hao kufanya unyama huo, walitokomea kusikojulikana wakiwa na simu pamoja na fedha walizopora kwa abiria na kuwaacvhia nuo zao.

Mganga Mfawidhi wa Hospital ya Wilaya ya Igunga, Godfrey Kisila, alisema walipokea majeruhi watano saa 10 usiku ambao walikuwa na majeraha sehemu mbalimbali za miili yao.

Alisema kati ya majeruhi hao, wanne walitibiwa na kupewa ruhusa, lakini Bw. Sangatwa, bado anaendelea kupatiwa matibabu na amelazwa katika wodi namba nane hospitalini hapo.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Elibariki Kingu, alithibitisha kutekwa kwa basi hilo na kudai kuwa, kiwango cha fedha na simu zilizoibiwa na majambazi hao bado hakijajulikana na juhudi za kuwasaka wahusika waliofanya kitendo hicho zinaendelea.

Aliwaomba wananchi kutoa ushirtikiano kwa Jeshi la Polisi ili wahusika waweze kukamatwa na kufunguliwa mashtaka. Basi 
hilo lilikuwa linaendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina 
la Bw. Makiselu Madi.

Aliliagiza jeshi hilo wilayani humo kuhakikisha mabasi yote hayatembei usiku ambapo dereva yoyote ambaye atakiuka 
agizo hilo akamatwe na kuchukuliwa hatua.

Majira

No comments: