Ni lazima itatokea mara chache kutofautiana kwa maana ninyi si malaika. Mantiki ni kwamba hata kama mnapendana kiasi gani, haiwezekani kila siku wote mkawa mna mawazo ya aina moja, hivyo mtapingana, japo kutokana na mapenzi ya kweli, mtapata suluhu mapema.
Kuna kukosea, kwa hiyo kibinadamu kuna wakati utamkosea mwenzi wako. Ila uwepo wa penzi la kweli, utasababisha mpate muafaka mapema. Utaguswa kuomba msamaha, naye atahamasika kukusamehe. Mvuto wako ndani yake, utamfanya asichelewe kupitisha msamaha. Hayo ndiyo mapenzi.
Ukiona wewe na mwenzi wako mnatofautiana, suluhu inakuwa ngumu kupatikana, siku zinapita hamzungumzii tatizo lililowafanya mkawa kwenye sura ya mfarakano, hapo maana yake kuna mambo makuu matatu, na moja lazima ndilo litakuwa sahihi.
Mosi; inawezekana umemkosea kitu kikubwa sana mwenzi wako. Alikuamini mno na hakutaraji kwamba utamfanyia hicho ulichotenda. Kutokana na moyo wake kuingiwa ganzi, inakuwa vigumu kwake kuketi mezani kutafuta suluhu, kwani anakosa imani aliyokuwa nayo awali.
Hapa nikupe angalizo kwamba ni bora uwe huaminiki au imani ya watu kwako iwe ya wastani. Endapo watu watakuwa na imani kubwa kwako, siku wakigundua una nyendo chafu za siri, heshima yako hupotea kabisa. Kama huaminiki, watu watasema ni kawaida yako. Waliokuamini wastani nao watanena hukuwa ukiaminika asilimia 100, hivyo halitakuwa gumzo.
Unapokuwa unaaminika kwa asilimia 100, maana yake hakuna shaka yoyote kwa watu juu yako. Hivyo basi, unapoboronga, heshima yako itashuka kwa kasi. Mitaani simulizi itakuwa wewe, kwani ni jambo geni na halikuwahi kutabiriwa kwako. Tafadhali, ishi maisha yako, usiishi maisha bandia. Utaumbuka.
Vivyo hivyo kwenye mapenzi. Mpenzi wako anayekupenda na kukuamini kupita kiasi, siku ukimtenda ndivyo sivyo, atakaa na maswali mengi kwa muda mrefu. Utageuka kinyaa mbele yake, kwa hiyo hata kukusamehe atapenda kufanya hivyo lakini atachelewa kwa sababu heshima yako kwake, imeondoka kabisa.
Pili; mapenzi yenu ni kama mnalazimisha. Hampendani kabisa au yeye hakutaki, kwa hiyo anaona hiyo ni fursa ya kukuadhibu. Utashangaa umemkosea jambo dogo lakini anavyolisimamia utadhani umeua mtu. Kama sura ya aina hiyo, inajiri kwenye uhusiano wake, jaribu kutazama mbele kwa matumaini. Hakupendi, atakupotezea muda.
Tatu; mapenzi yake kwako ni ya wastani. Ulivyo kwake, ukiwa naye ni sawa na hata usipokuwa naye.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment