ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 2, 2012

JK:Tutapunguza maambukizi VVU hadi kufikia sifuri 2015

RAIS Jakaya Kikwete ameeleza mikakati ya Serikali yake kuwa ni kuhakikisha inamaliza kabisa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi ifikapo mwaka 2015.
Akilihutubia taifa kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani Rais Kikwete alisema: “Tunataka tupunguze maambukizi na ikiwezekana mpaka 2015, kuwe na maambukizi sifuri kabisa. Huu mradi tumeshauanza, ila leo ni kama tunauzindua upya.”
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kitaifa mkoani Lindi, Kikwete alitaja mikakati mbalimbali aliyosema Watanzania hawana budi kuifuata ili kufikia kwenye hatua hiyo.
Miongoni mwa miakakati hiyo ni kuhamasisha watu kupima, waathirika kutumia Dawa za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARV), kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, elimu ya Ukimwi kutolewa shuleni na kwamba Serikali yake itahakikisha waathirika wanapata dawa bila malipo.
Alisema kwamba Serikali itahakikisha inaliingiza somo la kujikinga na Ukimwi katika mitalaa ya elimu nchini na kuongeza kuwa atatafuta fedha, ili kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa watoto hao.
Rais Kikwete alifafanua kuwa katika mpango huo wa kutoa elimu ya Ukimwi kwa wanafunzi,  Serikali imeweza kuwafikia asilimia 65 ya wanafunzi wa shule za msingi na asilimia 75 wa shule za sekondari.
“Wapo wanaosema  tunawafundisha watoto tabia mbaya, lakini hao wanaosema hivyo, ndiyo wamekuwa vinara wa kuwapeleka watoto wao Jando na Unyago,” alisema na kuongeza:
“Mangariba  wanatakiwa kuwapa watoto hawa elimu juu ya Ukimwi,  jinsi ugonjwa huu unavyoambukizwa na jinsi ya kujikinga.”
Aliwataka pia wazazi kutoona aibu kuwafundisha watoto wao jinsi ugonjwa huo unavyoambukizwa na kwamba wakifanya hivyo watakua wameokoa vifo na kumaliza maambukizi mapya.
Kikwete alisema pia kwamba kuna mradi wa kutokomeza maambukizi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ambapo aliwataka wajawazito kupima afya zao ili waweze kupewa ushauri wa jinsi ya kumkinga motto ili azaliwe bila kuwa na maambukizi.
Alitaja jambo jingine muhimu kuwa ni kuwahimiza Watanzania kupima afya zao kwa hiari na kwamba hadi sasa watu 17 milioni nchini wameshapima.
Ukimwi unapungua
“Mapambano dhidi ya Ukimwi ni makubwa na bado yanaendelea, miaka ya nyuma kila watu 100 ishirini ndio walikuwa na Ukimwi, ila hivi sasa katika kila watu 100 watano ndio wameambukiwa ugonjwa huu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza;
“Jamani Ukimwi sio sawa na hukumu ya kifo mahakamani, mtu mwenye virusi vya ugonjwa huu akifuata masharti anaishi kwa muda mrefu na hivyo kuendelea kufanya shughuli zake kama kawaida.”
Alieleza mpango mwingine kuwa ni ule wa Serikali kuingia mkataba wa miaka mitatu wa Dola 308milioni na Shirika la Maendeleo la Global Fund, kwa ajili kupatiwa  dawa za kurefusha maisha, vipimo vya afya na vifaa mbalimbali vya afya.
Ngoma zachangia Ukimwi
Katika hatua nyingine, uchunguzi umebaini kuwa sherehe za ngoma zinazokesha zinazohamasishwa na tamaduni za jamii za mikoa ya Pwani kuwa ni moja ya mambo yanayochangia maambukizi mapya ya Ukimwi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime alieleza hayo jana alipokuwa akitoa hotuba yake kuhusu sababu mbalimbali zinazochangia kuenea kwa ugonjwa huo wilayani humo.
“Yapo mambo mengi yanayo changia maambukizi ya VVU katika Manispaa yetu. Miongoni ni ngoma zinazokesha, utumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga, biashara ya ngono, ngono ya wanaume kwa wanaume,ulevi na kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja,” alisema Fuime.
Takwimu za kuanzia Julai 2011 hadi Juni 2012 zinaonyesha kuwa, Jiji la Dar es Salaam ni la pili kwa maambukizi hayo likiwa na wastani wa asilimia 9.3 wakati Wilaya ya Ilala ikiwa na asilimia 8.3.
VVU Iringa inatisha
Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma amewataka wakazi wa Mikoa ya Iringa na Njombe kuchukua hadhari ya kupambana na maambukizi ya Ukimwi katika maeneo yao kwakuwa bado yako juu ikilinganishwa na mikoa meingine nchini.
Alisema: “Utafiti wa hali ya Ukimwi nchini uliofanyika mwaka 2007/2008 unaonyesha kuwa maambukizi ya Ukimwi katika Mkoa wa Iringa kabla ya kugawanywa  yameongezeka kutoka asilimia 13.4 mwaka 2003/2004 hadi 15.7 katika mwaka 2007/2008. Kiwango hiki ni kikubwa ikilinganishwa na wastani wa maambukizi ya Ukimwi kitaifa ambayo ni asilimia 5.7 kwa mwaka,”alisema Dk Ishengoma na kuongeza:
“Ndugu, hali hii inatisha, madhara ya maambukizi ya Virus vya Ukimwi na Ukimwi ni makubwa sana, madhara haya ambayo huanzia katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla .”
Dk Ishengoma alitaja madhara mengine kuwa ni vifo, kuongeza idadi ya watoto yatima  ambao wanahitaji msaada wa elimu, malazi,chakula na matibabu.
Alisema takwimu zinaonyesha tangu mwaka 2004 hadi juni 2012 watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi ni 97,138 na kati yao 56,781 sawa na asilimia 58 waatumia ARV.
Maadhimisho ya siku ya Ukimwi mkoani humo yalikwenda sambamba na utoaji huduma ya ushauri na saa na kupima.
Habari hii imeandikwa na, Fidelis Butahe,Julius Mathias na Geofrey  Nyang’oro, Iringa

No comments: