ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, December 2, 2012

MAMA SALMA KIKWETE ASAIDIA KIKUNDI CHA MWAMBAO FISHING GROUP MKOANI LINDI

Mashine ya Boti, pamoja na vifaa mbalimbali vya uvuvi ambavyo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Wilaya ya Lindi Mjini Mheshimiwa Mama Salma Kikwete amevikabidhi kwa kikundi cha Ujasiriamali cha Mwambao Fishing Group kilichopo Mkoani Lindi.
M-NEC wa Wilaya Ya Lindi Mjini Mama Salma Kikwete akikaribishwa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mjini, Dk. Hamid Nassor katika Eneo na Kivukoni ambapo Mama Salma alikabidhi Vifaa mbalimbali vya uvuvi kwa kikundi cha ujasiriamali cha MWAMBAO FISHING GROUP.
Baadhi ya Vifaa mbalimbali zikiwemo Nyavu, Matanga, Maboya, Mitungi ya Gesi pamoja na Mashine za Boti zilizotolewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Ya CCM Wilaya ya Lindi Mjini, Mama Salma Kikwete.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Lindi Mjini, ndugu Mukhseen Rafii akisalimiana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, katika Uzinduzi wa Kikundi cha Ujasiriamali Cha Mwambao Fishing Group.

(PICHA NA BASHIR NKOROMO, LINDI)

Na Bashir Nkoromo, Lindi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Lindi Mjini, Mama Salma Kikwete aetoa misaada mbalimbali ya vifaa vya uvuvi kwa kikundi cha ujasiriamali cha uvuvi kinachoitwa Mwambao Fishing Group kilichopo Wilayani Humo. Mama Salma amefanya zoezi hilo jana alasiri katika eneo la Kivukoni ambapo ndipo kikundi hiko kilipoweka masikani yake.

Mama Salma alitoa misaada hiyo zikiwemo nyavu, maboya, matanga na mashine za boti kwa kikundi hicho akiongozana na Mawaziri na Manaibu Waziri wa Wizara mbalimbali waliokuwa mkoani humo kuhudhuria maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani ambapo kitaifa yalifanyika Mkoani Lindi.

Mama Salma aliwataka wavuvi hao kufanya kazi kwa UMOJA na kushirikiana akiwakumbusha kauli mbiu ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ya "UMOJA NA USHINDI" na kuwaambia kuwa mafanikio yao yatatokana na kujituma kwao na hivyo kukuza kipato chao na kuwa mfano kwa wavuvi wengine. Mama Salma alisema "Nawasihi kujituma kwa bidii kwani hicho ndicho kitu pekee kitakachowasaidia kuendeleza kikundi chenu hiki, tumieni uwezo wenu, fikra zenu na nguvu zenu zote zielekezeni katika kukijenga na kukiimarisha kikundi chenu ili kiweze kuwa ni kikundi cha mfano kwa watu wengine, kitoe msukumo kwa wavuvi na wajasiriamali wengine lakini pia kiwe ni tegemeo na matumaini kwa jamii."

Mama Salma yuko mkoani Lindi kwa Ziara ya siku Tano ambapo ameongozana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Khalfan Kikwete.

No comments: