Rais wa Chama cha Soka cha Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya,
Mwanasoka bora wa zamani wa Afrika ambaye sasa ni Rais wa Chama cha Soka cha Zambia (FAZ), Kalusha Bwalya, amesifu kiwango cha juu kilichooneshwa na timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) wakati wa mechi yao ya kimataifa ya kirafiki waliyoshinda 1-0 dhidi ya Zambia (Chipolopolo) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam juzi.Goli la Stars lilifungwa katika dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza na winga Mrisho Ngassa aliyeinasa pasi safi ya kiungo Mwinyi Kazimoto na kuchomoka na mpira kwa kasi kabla ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa Danny Munyao na kuwazima mabingwa hao wa Afrika.
Akizungumza na NIPASHE, Bwalya (49) alisema kuwa licha ya kuvutiwa na kiwango cha Stars, kamwe hajashangazwa na matokeo hayo kwani anajua kuwa Tanzania inazidi kupiga hatua kisoka katika siku za hivi karibuni.
Bwalya ambaye alitwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 1988, alisema Tanzania ina wachezaji wengi nyota, akiwamo mfungaji wa goli (Ngassa) na viungo Salum Aboubakar 'Sure Boy' na Kazimoto, ambao alikiri kuwa waliipa shida ngome ya Chipolopolo wakati wa mechi yao ya juzi.
“Sijashangazwa na matokeo ya leo (juzi) kwa sababu wachezaji wa Tanzania wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na najua kuwa hivi karibuni walikuwa kwenye michuano ya Chalenji, Uganda,” alisema Bwalya.
“Wamecheza vizuri, hasa katika kipindi cha kwanza na kuibuka na goli lililowapa ushindi. Wana kikosi kizuri, naamini siku zijazo watafanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa,” aliongeza mzaliwa huyo wa Mufulira, Zambia.
Kalusha aliitetea timu yake (Zambia) kupoteza mechi hiyo kwa madai kuwa nyota kadhaa wa kikosi cha kwanza hawakuwapo uwanjani na badala yake, walijaribu kuwapa nafasi vijana wengi ambao anaamini kuwa baadaye wataendelea kuifanya timu yao iwe moto wa kuotea mbali.
“Hatuwezi kuibeza Tanzania kisa sisi ni mabingwa. Wapinzani wetu wamecheza vizuri. Benchi letu la ufundi litaangalia makosa yaliyojitokeza ili tuwe na timu nzuri katika michuano ya kimataifa itakayoanza mwezi ujao,” alisema Bwalya.
“Kitu kikubwa ambacho nimekiona kimeigharimu Chipolopolo katika mechi ya leo (juzi) ni kuchezesha wachezaji wengi ambao hawana uzoefu wa mechi za kimataifa.
“Najua walimu (kocha Herve Renard na msaidizi wake Patrice Beaumelle) wana malengo maalum na hawa vijana na ndiyo maana wakawapa nafasi,” alisema Bwalya.
Mshindi wa Tuzo ya BBC ya Mwanasoka Bora wa Afrika, Christopher Katongo na beki wa kikosi cha nyota 11 wa Afrika, Stopilla Sunzu walikuwamo uwanjani wakati mabingwa wa Afrika wakiumbuliwa na Stars kutokana na goli la Mrisho Ngassa. Miongoni mwa nyota ambao Zambia hawakuwatumia katika mechi yao ya juzi ni kiungo Rainford Kalaba wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Emmanuel Mayuka wa Southampton ya Ligi Kuu ya England.
Hata hivyo, Stars pia haikuwatumia nyota wake John Bocco wa Azam, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaosumbuliwa na majeraha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment