ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 24, 2012

Polisi wajipanga kuwakabili wahalifu Krismasi

Mkuu wa Jeshi la Polisi Said Mwema 

JESHI la Polisi Nchini, limesema limejipanga vilivyo tayari kwa kudhibiti vitendo vya uvunjaji wa sheria katika Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanasherehekea siku hizo kwa amani na utulivu.

Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alisema hayo jana katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.

Alisema hata hivyo ingawa jeshi limejipanga, ni vizuri pia wananchi wakatoa ushirikiano wanapohisi kuwa kuna vitendo vya uvunjifu wa amani.Alisema wananchi wanapaswa kuwa makini kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu kwani maeneo hayo yanaweza kutumiwa na watu kufanya vitendo vya uhalifu.
“ Ulinzi utaimarishwa kwenye maeneo yote ya ibada, fukwe za bahari na sehemu za starehe na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu,” alisema.

Senso aliwatahadharisha watumiaji wa barabara kuwa makini kwa kufuata sheria za usalama, ikiwemo kuacha kwenda kwa mwendo kasi. Jeshi hilo pia limewataka wamiliki wa kumbi za starehe, kuingiza watu kulingana na uwezo wao.

“Wamiliki wa kumbi waache tamaa, waingize watu kulingana na uwezo wa kumbi zao na si kuzidisha,” alisema.

Taarifa hiyo pia iliwakumbusha wazazi kutowaacha watoto pekee yao kwani wanaweza kupata ajali za barabarani.

Jeshi hilo limeziomba taasisi za Serikali na madhehebu ya dini kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wananchi wanasherehekea sikukuu kwa amani.

No comments: