Abdallah Zombe
Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ilikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaachia huru Zombe na wenzake katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam.
Rufaa hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana na Jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, lakini ilishindikana kutokana na kuugua kwa Jaji Kaijage ambaye ni mmoja wa majaji katika jopo hilo, na kulazimika kuahirishwa.
Mbali na Jaji Kaijage, ambaye amechukua nafasi ya Jaji William Mandia aliyekuwa mmoja wa majaji katika jopo la awali, majaji wengine katika jopo hilo ni Nathalia Kimaro, ambaye ndiye kiongozi wa jopo na Katherine Oriyo.
Taarifa za kuugua kwa Jaji Kaijage zilitolewa na Jaji Kimaro kwa pande zote katika rufaa hiyo, wakati akiahirisha usikilizwaji wa rufaa hiyo.
Akiahirisha usikilizwaji wa rufaa hiyo, Jaji Kimaro alisema kuwa rufaa hiyo itasikilizwa kwa tarehe nyingine itakayopangwa na msajili na kwamba wadaiwa wote watajulishwa, tarehe hiyo mpya itakapokuwa imepangwa.
Katika kile kilichoonekana kuwa ni kujizatiti zaidi, jana upande wa mrufani (Jamhuri) ulikuwa na jumla ya mawakili saba na upande wa wajibu rufaa ulikuwa na jumla ya mawakili watano.
Jopo la mawakili wa Serikali liliongozwa na Wakili wa Kujitegemea, kutoka mkoani Tabora, Mutaki akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Angaza Mwipopo ambao wote waliendesha kesi ya msingi.
Wengine ni Alexander Mzikila, ambaye pia alikuwa ni mmoja wa mawakili wa Serikali walioendesha kesi ya msingi, lakini kwa sasa ni wakili wa kujitegemea.
Mbali na mawakili hao waliokuwepo kwenye kesi ya msingi, jana Serikali iliongeza nguvu kwa kuongeza mawakili wengine wanne ambao ni Timon Vitalis, Edwin Kakolaki, Prudence Rweyongeza, wote wakiwa ni Mawakili wa Serikali Wakuu na Peter Njike, Wakili wa Serikali Mwandamizi.
Jopo la mawakili wa wajibu rufaa liliongozwa na Wakili Richard Rweyongeza, anayemtetea mrufaniwa wa kwanza, (Zombe), Gaudioz Ishengoma, kwa mrufani wa pili, Christopher Bageni, Majura Magafu kwa warufani wa Denis Msafiri.
Zombe na wenzake walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa makusudi wafanyabiashara hao Sabinus Chigumbi, maarufu kwa jina la Jongo na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi.
Walikuwa wakidaiwa kutenda kosa hilo Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, Jijini Dar es Salaam, baada ya kuwatia mbaroni eneo la Sinza Palestina na kuondoka nao wakiwa hai wakiwatuhumu kuwa ni majambazi.Hata hivyo, Septemba 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwaachia huru washtakiwa wote ikisema kuwa baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za mawakili wa pande zote imeridhika kuwa washtakiwa hawakuwa na hatia ya mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.
Jaji Salum Massati (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufani), aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hapo bila kuacha mashaka.
Hata hivyo siku chache baada ya kuachiwa huru, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu, akidai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao.
DPP katika rufaa hiyo namba 254/2009, iliyofunguliwa Oktoba 6, 2009, amebainisha sababu 11 ambazo zimemfanya apinge hukumu hiyo yote, akidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, washtakiwa wote walikuwa na hatia.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment