Advertisements

Friday, December 21, 2012

Matokeo Darasa la Saba hadharani

Beatrice Moses na Ibrahim Yamola
SERIKALI imetangaza matokeo ya darasa la saba mwaka huu, huku takwimu za matokeo hayo zikionyesha kuwa zaidi ya nusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 ni wale waliopata asilimia 40 ya alama kwenda chini katika matokeo hayo.

Katika matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa wananfunzi 294,833 sawa na asilimia asilimia 52.58  waliopata daraja ‘D’ wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.


Hao wanaungana na wenzao 265,873 waliopata madaraja ya A,B na C ambao ni sawa na asilimia 47.41. Kwa mujibu wa taratibu za mitihani ya darasa la saba, jumla ya alama zote ni 250 ambazo zimegawanywa katika madaraja matano ambayo ni A mpaka E.

Mchanganuo wa madaraja hayo ni alama 201 hadi 250 kwa daraja la A, alama 151 – 200 kwa daraja B, alama 101 hadi 150 kwa daraja C, alama 51 – 100 kwa daraja D na alama 0 – 50 kwa daraja E.

Waziri Kawambwa alisema wanafunzi 560,706 walichaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kati ya 865,534 waliofanya mtihani huo wa siku mbili; Septemba 19 na 20 mwaka huu na kwamba mwaka huu wasichana wamefanya vizuri katika mtihani huo kuliko wavulana.

“Wasichana waliofaulu ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 ya  wanafunzi 560,706 wakati wavulana waliofaulu ni 279,246 sawa na asilimia 49.80,” alisema Kawambwa alipokuwa akitangaza matokeo hayo na kuongeza:

“Matokeo yanaonyesha kuwa jumla ya wahitimu 3,087 walipata daraja A, wakati 40,683 walipata daraja la B. Wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja C wakati  526,397 walipata daraja D. Watahiniwa waliobaki 73,264 walipata E”.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi  waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013, imeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi 515,187 waliochaguliwa mwaka jana.


“Mtihani wa mwaka huu, kwa mara ya kwanza watahiniwa walifanya kwa kutumia teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) na ulisahihishwa kwa kutumia kompyuta,” alisema.  

Alisema matokeo haya yanaonyesha alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.

Kabla ya matokeo, wasichana waliofanya mtihani walikuwa 456,082 sawa na asilimia 52.68 na wavulana ni 409,745 sawa na asilimia 47.32,” alisema Dk Kawambwa.

“Watahiniwa 29,012 sawa na asiliamia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo na ugonjwa,” alisema.

Dk Kawambwa alisema, kati yao, ambao hawakufanya mtihani wasichana walikuwa 12,501 sawa na asilimia 2.67 na wavulana ni 16,511 sawa na asilimia 3.87.

Waziri huyo  alisema,  udanganyifu katika mitihani kwa mwaka huu umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na idadi ya mwaka jana.

“Waliofutiwa matokeo mwaka huu ni watahiniwa 293 ikilinganishwa na watahiniwa 9,736 waliofutiwa matokeo yao kwa udanganyifu mwaka jana,” alisema Dk Kawambwa.

Hata hivyo, itakumbukwa serikali ilionya mwaka jana kuwa mwanafunzi atakayebainika kujiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi hizo, Mwalimu Mkuu wa shule alikotokea mwanafunzi huyo na Msimamizi wa Mtihani wakumaliza elimu ya msingi watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Katika mkutano huo wa jana na Waandishi wa Habari, Dk Kawambwa hakutaja  viwango vya ufaulu kwa kila somo kama ambavyo imezoeleka katika mitihani iliyotangulia wala mkoa uliofanya vizuri au vibaya.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo alipotangaza matokeo ya mwaka jana aliweka wazi viwango vya ufaulu wa masomo ya Kiingereza, Sayansi na Hisabati, ikilinganishwa na mwaka juzi.

Mulugo alisema viwango hivyo vilikuwa vimepanda kwa mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2010 ambavyo ni Kiingereza kutoka asilimia 36.47 hadi asilimia 46.70, Sayansi asilimia 61.33 kutoka asilimia 56.05 na Hesabu asilimia 39.36 kutoka asilimia 24.70.

Waziri Kivuli wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo akizungumzia matokeo hayo jana alisema: “Hili janga, kwa sababu ukifanya uchambuzi wa haraka utabaini kuwa wanafunzi waliopata alama za daraja la A ni asilimia 0.35 tu”.

Lyimo ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema upo uwezekano mkubwa kukawa na idadi kubwa ya wanafunzi wasiojiweza waliochaguliwa kwenda Sekondari, hivyo akashauri iandaliwe program maalum ya kuwawezesha wanafunzi hao kumudu masomo ya kidato cha kwanza.

“Kama wanafunzi zaidi ya nusu waliochaguliwa kwenda sekondari ni wale wa daraja la D, hapo kuna kazi kubwa sana, tunaweza kuwa na mbumbubu wengi Sekondari kwahiyo nashauri Serikali iandae walau mpango wa wiki mbili kabla ya shule kufunguliwa ili kuwasaidia hawa watoto,”alisema.

Lyimo alisema ofisi yake itaendelea kufanya utafiti ili kubaini sababu za kufanya vibaya kwa wanafunzi katika mtihani huo na kwamba itatoa taarifa baada ya kupata matokeo ya kitaalamu kuhusu suala hilo.

No comments: